Alama aliyoiacha Raila Odinga Gor Mahia siku chache kabla ya kifo
Muktasari:
- Mbali na kuwa mpigania demokrasia kwa muda mrefu na mwanasiasa mwenye urithi mkubwa wa kisiasa, Raila pia alikuwa mpenzi wa soka wa kweli, mwenye uhusiano wa karibu sana na mchezo huo nchini Kenya.
Habari za kifo cha kiongozi wa upinzani mwenye uzoefu mkubwa, Raila Odinga, zimeitikisa Kenya na kuacha taifa likiwa katika huzuni. Taarifa za kifo chake zimetolewa leo Jumatano, Oktoba 15, 2025, ambapo amefikwa na umauti akiwa anatibiwa nchini India.
Mbali na kuwa mpigania demokrasia kwa muda mrefu na mwanasiasa mwenye urithi mkubwa wa kisiasa, Raila pia alikuwa mpenzi wa soka wa kweli, mwenye uhusiano wa karibu sana na mchezo huo nchini Kenya.
Timu yake pendwa ilikuwa Gor Mahia, klabu inayoshiriki Ligi Kuu ya Soka Kenya. Kwa Raila, tofauti na wanasiasa wengi waliomtangulia au waliomfuata, soka halikuwa burudani tu bali lilikuwa sehemu ya maisha yake. Mara nyingi alinukuliwa katika mazungumzo yake akiuzungumzia mchezo huo katika hotuba zake au mazungumzo ya kirafiki.
Bila kujua, uhusiano wake wa mwisho na klabu yake pendwa hiyo ulitokea muda mfupi kabla ya kusafiri kwenda India kutibiwa.
Kabla ya kusafiri kwenda India, Raila alitoa mchango wa shilingi milioni 10 za Kenya kusaidia shughuli za kiutawala na usafiri za Gor Mahia kwa msimu wa 2025-2026, tukio lililogeuka kuwa la kihistoria na la kugusa mioyo ya mashabiki.
Katika kipindi cha takriban miongo miwili akiwa mlezi wa Gor Mahia, Raila alikuwa na jukumu kubwa katika kuunda historia ya klabu hiyo.
Timu hiyo, maarufu kama K’Ogalo, ina umuhimu mkubwa wa kisiasa na kijamii nchini, hasa miongoni mwa jamii ya Waluo. Kama mlezi, Raila mara kwa mara aliwakaribisha viongozi wa timu nyumbani kwake Karen kwa mikutano ya kuwapa hamasa kabla na baada ya mechi muhimu.
Derby ya Mashemeji
Mapenzi ya Raila kwa michezo hayakuishia Gor Mahia pekee. Alikuwa pia shabiki wa Harambee Stars, timu ya taifa ya Kenya, na mara kadhaa alionekana akishiriki furaha na mashabiki katika mechi kubwa, ikiwemo Derby ya Mashemeji kati ya Gor Mahia na AFC Leopards.
Zaidi ya mipaka ya Kenya, Raila alikuwa mfuasi mkubwa wa klabu ya Arsenal ya Ligi Kuu ya England. Alifanya safari kadhaa kwenda London, akiwa amevalia jezi za timu hiyo na kuhudhuria mechi kwenye Uwanja wa Emirates.
Kifo cha mwanasiasa huyo mkongwe kimeashiria mwisho wa enzi muhimu, lakini urithi wake katika soka la Kenya, kupitia juhudi zake za kuinua ustawi wa wachezaji, kukuza michezo ya ndani na kuhamasisha mashabiki utaendelea kuishi milele.