Harmonize aachiwa, kupiga shoo Mombasa

Sunday May 01 2022
Harmonize PIC
By SINDA MATIKO

BAADA ya kusotea seli za Polisi Kileleshwa mjini Nairobi toka asubuhi ya leo, Rais wa Konde Gang, Harmonize ameachiwa huru.
Harmonize alikamatwa Jumapili asubuhi baada ya kudaiwa kuzipora hela klabu nne za jijini Nairobi alizotakiwa kupiga shoo lakini akakosa kufanya hivyo.
Mkurugenzi wa Captain Lounge Jor Barsil, ndiye aliyewaitwa maafisa wa usalama na kuwapeleka kumkamata Harmonize.
Hii ilikuwa baada ya Harmonize kutimba kwenye klabu yake  iliyopo Mombasa, Road usiku wa Jumamosi na kutuimbuiza kwa dakika mbili tu na kisha kuondoka.
"Niliwalipa maajenti wa Harmonize Ksh450,000 (Tsh9 millioni)  kuja kutumbuiza kwenye klabu yangu. Alipofika pale, alimaliza dakika tano tu na kutaka kuondoka". "Ndicho kitendo kilichowakasirisha mashabiki na wakataka kumtandika, nilimwokoa lakini nikapelekea akamatwe, alipaswa kutumbuiza kwa lisaa limoja na nusu"

"Nadai anirejeshee Sh450,000, na pia Sh1 milioni nilizotumia kutengeneza jukwaa lakini pia Sh350,000 tulizotumiwa kupromoti," alilalamika Barsil.
Baada ya kushindwa kutwa nzima seli huku Barsil akisisitiza kuwa yupo tayari kumfikisha mahakamani Jumatano, upepo ulibadilika.
Hii ni baada ya Gavana wa zamani wa Nairobi Mike Sonko kufika katika kituo hicho cha polisi majira ya mchana na kumwokoa Harmonize.
"Harmonize kaachiliwa, ni mtu huru na leo usiku atapiga shoo klabu Volume Mombasa pamoja na wasanii wengine wa Mombasa, kilichotokea ni mtafaruku mdogo tu ni mkangayiko wa kimawasiliano" Sonko kasema na kuongeza;

"Harmonize hakusaini mkataba wowote na klabu zozote zile isipokuwa Club Volume sema kuna matapeli wa mjini waliosaini mikataba hiyo kwa kutumia jina lake na alipokosa kutokea kwenye klabu hizo ikazuka sintofahamu tumeyamaliza jamaa yupo huru," Sonko kasema.
Tayari Mwanaspoti imedhibitisha Harmonize kakwea pipa kuelekea zake Mombasa na kupitia Instagram yake ameahidi kutumbuiza nyimbo zisizopungua 25 kwa mashabiki wake.

Advertisement