Gor Mahia yapasuka tena KPL
Muktasari:
- K'Ogalo inayoshuika nafasi ya nne kwa sasa awali ilikuwa imeshinda mechi tatu mfululizo za ligi hiyo, lakini katika mechi ya leo ilikutana na kisiki kwa kulala bao 1-0 kwenye Uwanja wa Kenyatta, shukrani ikienda kwa Erik Michubu aliyekwamisha penalti na kuifanya Gor Mahia ipoteze mechi ya tatu msimu huu.
BAO la mkwaju wa penalti iliyopigwa katika dakika ya sita ya pambano la Ligi Kuu ya Kenya, limewazamisha watetezi wa ligi hiyo, Gor Mahiakwa mara nyingine tena ikicheza nyumbani dhidi ya Bidco United.
K'Ogalo inayoshuika nafasi ya nne kwa sasa awali ilikuwa imeshinda mechi tatu mfululizo za ligi hiyo, lakini katika mechi ya leo ilikutana na kisiki kwa kulala bao 1-0 kwenye Uwanja wa Kenyatta, shukrani ikienda kwa Erik Michubu aliyekwamisha penalti na kuifanya Gor Mahia ipoteze mechi ya tatu msimu huu.
Gor Mahia ilianza kufumuliwa katika ligi ya msimu Oktoba 28 ilipofungwa ugenini mabao 2-1 na Nairobi City iliyomaliza mechi hiyo ikiwa pungufu kisha Bandari FC ikatonesha kidonda Novemba 6 kwa kuwanyuka watetezi mabao 2-0 mechi iliyopigwa pia ugenini.
Kipigo hicho kimeifanya Gor kusaliwa na pointi 17 ilizopata katika mechi 10, wakati Bidco imefikisha pointi 14 na kuchupa kutoka nafasi ya 16 hadi ya 12. Hata hivyo Bidco imecheza mechi 12, ikiwa ni mbili zaidi ya ilizocheza K'Ogalo iliyokuwa imetoka kushinda ugenini mabao 3-2 dhidi ya Talanta.
Katika mechi nyingine zilizochezwa jioni ya leo, Bandari na vinara wa ligi hiyo KCB zilitoshana nguvu kwa kutoka sare ya 1-1, huku Shabana ikiishindilia Talanta kwa mabao 2-1 na Kariobang Sharks ikiwa ugenini iliitambia Posta Rangers kwa bao 1-0.
Kwa mechi za jana Jumamosi, Nairobi City ilitamba nyumbani mbele ya Muranga kwa ushindi wa bao 1-0 kama ilivyokuwa kwa Police iliyoifumua Mara Sugar, huku Sofapaka iliikung'uta Ulinzi Stars mabao 4-1, wakati Tusker ikishinda Mathare Utd mabao 2-0 na Kakamega Homeboyz na Leopards ilitoka sare ya 1-1.
Kwa matokeo ya wikiendi hii, KCB inaendelea kuganda kileleni mwa msimamo ikiwa na pointi 23 kupitia mechi 12, huku Tusker ikiwa nyuma yake na alama zao 21 ikicheza mechi 11 kama iliyocheza Bandari ambayo imekusanya pointi 20 na Gor Mahia ikifuata ikiwa na pointi 17 kama ilizonazo Kariobang Sharks.