Geay aelezea alichomfanya Kipchoge

Mwanariadha Gabriel Geay amevunja ukimya na kueleza namna alivyopambana na magwiji wa marathoni wa dunia hadi kuibuka mshindi wa medali ya fedha kwenye mbio za Boston marathoni, Jumatatu iliyopita.
Mtanzania huyo alimaliza wa pili akitumia saa 2:06: 04 akiachwa kwa sekunde tisa na bingwa raia wa Kenya, Evans Chebet aliyetumia saa 2:05:54.
Mwanariadha mwenye kasi zaidi duniani kwenye marathoni, Eliud Kipchoge alimaliza wa sita akitumia saa 2:09:23 katika mbio hiyo ya kongwe ya pesa nchini Marekani.
Akizungumza na Mwanaspoti, Geay alisema ushindi wake alianza kuutengeneza kilomita ya 32 alipompiku Kipchoge na kuona kumbe inawezekana.
"Ilikuwa ni mbio yenye presha kutokana na wakimbiaji tuliokuwa pale, lakini maandalizi niliyofanya, kujituma na jitihada ndizo zilinipa matokeo haya," alisema.
Alisema walipoanza mbio, wengi walikuwa wakimtizama Kipchoge kutokana na rekodi yake, lakini katika kundi la kwanza walikwenda sambamba hadi walipofika kilomita ya 32 wakaanza kuachana.
"Pale ndipo nilimpita Kipchoge, tukabaki kwenye kundi lililotoa bingwa, Chebet tulikwenda naye sambamba hadi kilomita ya 40, ndipo aliongeza kasi na kumaliza bingwa," alisema Geay.
Alisema kulikuwa na changamoto nyingi za upinzani, na kila mmoja kwenye mbio ile alipambana ili kufanya vizuri na Chebet kwa kuwa ni bingwa mtetezi alitumia mbinu ya kutoka na kuongeza mwendo wakiwa wamesalia na kilomita mbili kumaliza mbio.
"Nilimfuata, tageti yangu ilikuwa ni dhahabu, lakini alimaliza wa kwanza na sekunde chache nikamaliza ile mbio," alisema Geay ambaye ni mara ya pili anachuana kwenye mbio hiyo ambayo bingwa aliondoka na kitita cha Sh351 Milioni.
Akizungumzia mipango yake baada ya Boston, Kocha wa Geay, Thomas Tlanka alisema kabla ya mashindano ya dunia, atachuana kwenye mbio ya kimataifa ya nusu marathoni.
"Bado hatujapanga ni wapi, lakini atakimbia nusu marathoni ili kuimarisha kasi yake kabla ya kwenda kwenye mashindano ya dunia kisha atarudi kujiandaa na Olimpiki," alisema.
Geay ni miongoni mwa wanariadha wawili waliofuzu pia kushiriki Olimpiki ya 2024 huko Paris Ufaransa, mwingie ni Alphonce Simbu ambaye hivi karibuni alimaliza wa tatu kwenye mbio ya nusu marathoni nchini China.
Nyota hao ambao ni miongoni mwa wanamichezo watano nchini wanaopewa ufadhili na Kamati ya Olimpiki ya Kimataifa (IOC) kupitia kitengo chake cha misaada cha (Olympic Solidarity) kwa uratibu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) wana tiketi ya kushiriki Olimpiki 2024 na mashindano ya dunia 2023.