Bosi Gor Mahia atuhumiwa kuongeza muda wa madaraka

Muktasari:
- Akizungumza wakati wa kumtambulisha kocha mpya wa timu hiyo Sinisa Mihic, Rachier alithibitisha Klabu hiyo itafanya uchaguzi ndani ya muda wa siku 90 uliowekwa kulingana na uamuzi wa mahakama.
MWEKA hazina wa Gor Mahia FC, Dolphina Odhiambo amemshutumu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Ambrose Rachier kwa kuchelewesha uchaguzi makusudi ili kuongeza muda wa kuhudumu kinyume cha sheria.
Kulingana na Odhiambo, klabu hiyo ilipaswa kufanya uchaguzi Agosti 2024, lakini Rachier ilidaiwa kusimamisha mchakato na kusalia mamlakani.
Hata hivyo, uamuzi wa hivi majuzi wa Mahakama ya Mizozo ya Michezo (SDT) uliamuru mabingwa hao wa Ligi Kuu Kenya (FKF PL) kufanya uchaguzi ndani ya siku 90, uamuzi ambao Odhiambo amekubaliana nao.
Odhiambo amesisitiza mahakama hiyo imeweka wazi njia ya uchaguzi, hivyo Rachier anafaa kung'atuka na wala sio kugombea tena, akiwa tayari amemaliza muda wake wote, pia alikosoa uongozi wake, akisema Gor Mahia imedumaa tangu achukue hatamu mwaka wa 2008.
“Uchaguzi wa Gor Mahia ulifaa kufanyika mwaka jana Agosti, lakini mwenyekiti alichelewesha makusudi kuongeza muda wake kinyume cha sheria."
“Kwa miaka 16, klabu imetatizika karibu kila nyanja, maendeleo, uthabiti wa kikosi na usimamizi wa fedha. Tumekuwa na mzunguko usio na mwisho wa makocha na kesi zilizorudiwa za FIFA juu ya uvunjaji wa mikataba," alisema Odhiambo.
Amesisitiza zaidi uamuzi wa mahakama ya STD unatoa ramani ya wazi ya mabadiliko ya Klabu, kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa uwazi na kwa mujibu wa katiba ya Klabu.
"Wanachama wote wa Gor Mahia wana hamu ya kuona uchaguzi ukiendelea kama ilivyoelekezwa ndani ya siku 90 tunatarajia mchakato huo kuwa wa kidemokrasia na wa uwazi na kuleta uongozi mpya wa kuiongoza Klabu."
Licha ya ukosoaji wake, Odhiambo alikubali mchango wa Rachier, akisema, "Uongozi wake umesaidia klabu kukabiliana na changamoto nyingi, lakini ni wakati wa maono mapya ya kuielekeza Gor Mahia katika sura yake inayofuata."
Huku uchaguzi ukikaribia, maswali yameibuka kuhusu kustahiki kwa Rachier kuwania, hasa baada ya mahakama ya STD kuamua muhula wake ulikamilika Agosti 8, 2024 na Odhiambo ametangaza kuwania nafasi ya mwenyekiti.
"Nitawania uenyekiti wa Gor Mahia. Nashukuru uchaguzi unaandaliwa, lakini mahakama imeamua mwenyekiti huyo hastahili kugombea tena.Ikiwa atang'ang'ania kugombea, tuko tayari kukabiliana. naye kwenye kura," ameongeza
Akizungumza wakati wa utambulisho wa kocha mkuu mpya Sinisa Mihic, Rachier amethibitisha klabu hiyo itafanya uchaguzi ndani ya muda wa siku 90 uliowekwa kulingana na uamuzi wa mahakama hiyo.
"Tuko tayari kikamilifu kutii agizo la Mahakama, Jumanne tutafika mbele ya mahakama hiyo kwa ajili ya kutajwa na kisha tutatangaza ramani ya uchaguzi iliyo wazi na kuwaalika wagombea wanaotaka uchaguzi," alisema Rachier.
Hata hivyo, Rachier amewataka wanachama wote wa timu hiyo kutanguliza masilahi ya klabu badala ya siasa, wakati huu ambao Gor Mahia inawania kutetea tena ubingwa wake wa Ligi Kuu Kenya.
"Hatuwezi kuruhusu masuala ya uchaguzi kufunika lengo letu kuu, ambalo ni kushinda ligi. Kila kitu kinapaswa kushughulikiwa kwa uwajibikaji," aliongeza.
STD imeruhusu kamati kuu ya sasa kusalia ofisini kwa muda hadi uchaguzi ufanyike. Pia iliagiza wanachama waliosajiliwa kufikia tarehe 31 Desemba 2024 pekee ndio watastahiki kupiga kura, kuhakikisha mchakato wa haki na wa kuaminika.