Black Mamba yala vinono
BLACK Mamba FC walimaliza vyema wikiendi yao kwenye mashindano ya Ligi ya FKF Rabai Sub-County League iliyopigwa uwanja wa Cheupe Rabai kaunti ya Kilifi baada ya kuwalima Mission Boys mabao 4-0.
Ulikua ni ushindi mtamu ukizingatia Black Mamba ilisajili matokeo duni katika mechi zao za mwanzoni lakini sasa wanajiweka pazuri kwenye ligi hiyo.
Kwengineko, vijana wa Lexicon FC walipigishwa sare ya mabao 4-4 na Ganga Sports katika uwanja wa Shule ya Msingi Lugwe.
Usimamizi wa soka katika eneobunge la Rabai umeonyesha kuridhishwa na kiwango cha nidhamu kinachoshuhudiwa katika viwanja mbalimbali tofauti na ilivyokuwa hapo awali.
Mkufunzi wa Talent FC ambaye pia ni sekeretari wa kamati ya michezo Wadi ya Rabai Kisurutini, Ramadhan Karani, aliambia MWANASPOTI kwamba kipindi cha nyuma haikuwa jambo rahisi kwa mechi kumalizika salama katika viwanja vya Rabai kutokana na utovu wa nidhamu.
Anataja kuwa hatua hiyo ni moja ya kuona kuwa mashabiki, wachezaji, marefa na wasimamizi wa vilabu katika eneo hilo wametambua umuhimu wa nidhamu michezoni.