Baraza: Mimi sipangwigwi

MKUFUNZI mpya wa Police FC, Francis Baraza, hacheki na mtu. Kocha huyo aliyeridhi mikoba ya Sammy ‘Pamzo’ Omollo, ametoa tahadhari kwa mabosi wake.
Kufuatia tetesi kuwa Pamzo na msaidizi wake Musa Otieno walijiuzulu nyadhifa zao kutokana na kutengenezewa mazingira magumu ya kikazi na mabosi wa klabu, Baraza ametishia kufanya jambo.
Pamzo na Otieno walidai kunyimwa uhuru wa kukipanga kikosi huku kila mara wakipata presha kutoka kwa mabosi wao kuhusu wachezaji wapi waunde First 11.
Sasa Baraza ambaye aliipata kazi hiyo siku chache baada ya kutemwa na Kagera Sugar, ametishia kujiuzulu mara moja endapo atakumbana na hali tata kama hiyo aliyokutana nayo Pamzo.
“Nimeyaskia na kuyasoma mitandaoni madai hayo ila sitaki kuyazingatia sana. Mimi mpaka sasa sijaona kero yeyote kwenye utendaji wa kazi zangu. Nimekuwa nikipanga vikao vya mazoezi pamoja na mbinu na kukichagua kikosi bila ya bughdha yeyote,” alisema Baraza.
Hata hivyo ametahadhirisha kuondoka mara moja endapo atahisi wadosi wake wamegeuka kuwa kero.
“Mechi mbili zilizopita ni mimi niliteua kikosi kizima. Mimi ni mtaalamu, naielewa kazi yangu ila kama kuna mtu atataka kunifanyia kazi yangu, basi bora apewe yeye na wala sitasita kujiuzulu wadhifa wangu,” anatishia Baraza.