Baraza apania ushindi back-to-back

KAIMU kocha mkuu wa Bandari FC, John Baraza, ameanza vizuri majukumu yake kwa ushindi mwishoni mwa wiki iliyopita na wikendi hii analenga kuzoa pointi zingine tatu muhimu ili timu ikae pazuri kwenye msimamo wa Ligi Kuu Kenya.

Bandari FC, timu pekee kutoka ukanda wa Pwani inayokipiga FKFPL, inajiandaa kuwavaa vinara Posta Rangers gemu ikipigwa jijini Nairobi.

Baraza alisema wanatambua Rangers chini ya ukufunzi wa John Kamau ni timu ngumu licha ya kupoteza mchezo wa kwanza msimu huu wikendi iliyopita wakichezea kichapo cha mabao 3-1 kutoka kwa FC Talanta.

Kocha huyo chipukizi aliyechukua mikoba ya Twahir Muhiddin, alianza kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya mabingwa mara 12 FKFPL, AFC Leopards, iliyochezwa wikendi iliyopita wakiwa nyumbani ugani Mbaraki Sports Club jijini Mombasa.

“Tulipokutana na Leopards tulikuwa tumepata muda mzuri na wa kutosha kujiandaa na tukafanikiwa kupata ushindi, naamini tutafanya vizuri zaidi tutakapokutana na Rangers ugenini,” alisema Baraza ambaye ni kocha wa zamani wa Sofapaka.

Alisema wanafahamu Rangers sio timu ya kubeza kwasababu wameanza msimu vizuri ila ana matumaini vijana wake wapo tayari kuwapokeza Rangers kichapo cha pili msimu huu.

Baraza alisema wataendelea kumkosa straika Umaru Kasumba ambaye anaamini akipona atatengeneza ushirikiano mzuri na Mganda mwenzake Derrick Nsibambi kwenye safu ya ushambuliaji.

Nsibambi ndiye aliyefunga bao la pekee katika ushindi dhidi ya Leopards katika gemu ambayo kocha Baraza aliwapongeza wachezaji wake kucheza kwa kujitolea na kuwapa mashabiki wao burudani.

“Nina matumaini makubwa wachezaji wataendelea kucheza kwa kujituma ili tuzoe pointi zitakazotuweka kwenye nafasi nzuri katika msimamo wa ligi,” alisema.