Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Angachi ataja sababu ya kuchagua jeshi na kukacha soka la kulipwa Ulaya

Muktasari:

  • Mwaka wa 2021, Angachi mwenye umri wa miaka 24 alihamia Ulinzi Starlets kutoka Gaspo Women baada ya klabu yake ya zamani kushushwa daraja kutoka Ligi Kuu ya Soka ya Wanawake ya Shirikisho la Soka Kenya (FKF-WPL).

Wakati wachezaji wengi wa soka wanaota kucheza soka la kulipwa nje ya nchi, kiungo wa Ulinzi Starlets na Harambee Starlets, Sherly Angachi Andibo amechagua njia tofauti akijiunga na jeshi ili kujihakikishia maisha baada ya soka.

Mwaka wa 2021, Angachi mwenye umri wa miaka 24 alihamia Ulinzi Starlets kutoka Gaspo Women baada ya klabu yake ya zamani kushushwa daraja kutoka Ligi Kuu ya Soka ya Wanawake ya Shirikisho la Soka Kenya (FKF-WPL).

Ingawa awali alifikiria kucheza nchini Ugiriki, ofa ya kazi Jeshi la Ulinzi ilimshawishi kubaki.

"Tulikuwa tumekubaliana kwamba kama hawatatimiza ahadi zao za kazi ndani ya muda fulani, ningetafuta klabu Ugiriki. Nashukuru waliheshimu ahadi yao," amesema.

Angachi amekamilisha mafunzo ya kijeshi kwa miezi sita katika Shule ya Mafunzo ya Askari (RTS) huko Eldoret na sasa ni ofisa katika Kambi ya Kahawa huko Nairobi. Pia anasomea kozi za upishi.

"Niliingia Ulinzi sio tu kwa nafasi ya kucheza, bali pia kwa kazi waliyonipa baada ya kumaliza shule ya upili," ameelezea.


Tangu alipojiunga na Ulinzi, ameshinda vikombe vinne, ikiwemo Kombe la Wanawake la FKF na Super Cup ya FKF mwaka 2021 na 2023.

Alikuwa mshambuliaji awali, lakini aligeuka na kuwa kiungo na tangu wakati huo ameonyesha uwezo mkubwa, jambo ambalo limesababisha kuvutiwa na klabu ya Simba Queens ya Tanzania na Kenya Police Bullets.

"Sina mpango wa kuondoka Ulinzi hivi karibuni," amesema.

Angachi alisajiliwa na kocha hayati Joseph Wambua, ambaye alichukua jukumu muhimu katika maendeleo yake kabla ya kufariki Septemba iliyopita baada ya kupigana na saratani ya utumbo mpana.

"Kifo chake kiliniacha na maumivu; ilichukua muda kukubaliana. Lakini tumeshapiga hatua na tunarudi kushinda katika ligi," amesema.

Sasa akiwa nahodha wa timu, Angachi ameiongoza Ulinzi Starlets kufika nafasi ya nne kwenye msimamo wa FKF-WPL kwa alama 23 katika mechi 14, ikiongozwa na Kenya Police Bullets kwa alama sita.

Sifa za uongozi wake zimepigiwa chapuo na kocha mkuu Collins Oduor.

"Nilimchagua kuwa nahodha nilipojiunga na timu. Anaweza kuwahamasisha wachezaji na kuwasukuma kuwa na ujasiri," amesema.

Angachi alianza kuitumikia timu ya Taifa mwaka 2017 alipoichezea timu ya taifa ya Kenya ya U-20 kwenye michuano wa kuwania kufuzu Kombe la Dunia la Wanawake.

Baadaye alicheza kwa timu ya wakubwa kwenye mashindano ya kuwania kufuzu kwa Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON) mwaka 2018.

Mwaka 2023, katika mashindano ya kuwania kufuzu kwa WAFCON 2024 dhidi ya Botswana, alijizolea umaarufu alipoingia kama mchezaji wa akiba huku akinyoa nywele zake zote.

Mabadiliko hayo makubwa yaliwashangaza watazamaji, lakini yalitokana na mafunzo yake ya kijeshi katika RTS na sasa anajiandaa kwa michuano ya kuwania kufuzu WAFCON 2026 dhidi ya Tunisia.

"Kufuzu WAFCON kwa mara ya piliu haitakuwa rahisi, lakini kwa maandalizi bora na mwongozo kutoka kwa makocha wetu wenye ujuzi, naamini tunaweza kufuzu tena," amesema.

Akiwa na msukumo kutoka kwa aliyekuwa nahodha wa Starlets Doreen Nabwire, Angachi anaendelea kuwa kiongozi ndani na nje ya uwanja, akionyesha kwamba kujitolea na ustahimilivu vinaweza kufungua njia ya mafanikio.