Amza, Ngereka waibeba Bandari Kenya
Muktasari:
- Ngeleka aliyewahi kukipiga Dodoma Jiji iliyopo katika Ligi Kuu Bara, alianza langoni na kufungwa bao la mapema na wageni dakika ya saba tu kabla ya kusimama imara na kuipa Bandari ushindi huo wa kwanza katika ligi hiyo.
NYOTA wa zamani wa Kagera Sugar, kipa Alain Ngeleka na mshambuliaji Moubarack Amza jioni hii wameibeba Bandari FC inayoshiriki Ligi Kuu ya Kenya baada ya timu hiyo wanayoitumikia kwa sasa kushinda nyumbani kwa mabao 3-1 dhidi ya Murang'a Seals kwenye Uwanja wa Mbaraki, mjini Mombasa.
Ngeleka aliyewahi kukipiga Dodoma Jiji iliyopo katika Ligi Kuu Bara, alianza langoni na kufungwa bao la mapema na wageni dakika ya saba tu kabla ya kusimama imara na kuipa Bandari ushindi huo wa kwanza katika ligi hiyo.
Kipa huyo raia wa DR Congo, alishtukizwa kwa bao la Joe Waithira dakila ya saba, kabla ya
Geoffrey Ojunga kusawazisha dakika 19 na dakika 33 Amza ambaye ni raia wa Cameroon aliyewahi kukipiga pia Ihefu (sasa Singida BS) na Namungo akaongeza la pili kwa wenyeji kwa kichwa kikali kama kapiga kwa mguu na kufanya timu ziende mapumziko, Bandari ikiwa mbele kwa mabao 2-1.
Bao lililoihakikishia Bandari ushindi na kuvuna pointi tatu za kwanza katika mechi moja ikifikisha nne baada ya kushuka uwanjani mara tatu, liliwekwa kimiani na Joseph Otieno dakika ya 77.
Matokeo hayo yameifanya Bandari kuchupa kwa nafasi tisa, kutoka ya 14 hadi ya tano, huku Murang'a ikisalia nafasi ya 11 ikiwa na pointi tatu kwa ushindi pekee iliyopata katika mechi tatu ilizocheza hadi sasa.