Polisi Kenya yapasuka, ila yasonga mbele
Muktasari:
- Polisi inayonolewa na kocha Etienne Ndayiragije ilijikuta ikifungwa mabao 2-0, lakini ushindi wa 3-1 iliyopata ugenini wiki iliyopita umewabeba kwani matokeo ya jumla yamekuwa sare ya 3-3, lakini maafande hao wa Kenya wamefuzu kwa faida ya bao la ugenini dhidi ya wapinzani wao hao.
MABAO mawili ya Mogadishu City ya Somalia yameweza kuizima Polisi Kenya ikiwa ardhi ya nyumbani, lakini haikuweza kuisaidia kuing'oa katika mechi ya marudiano ya raundi ya jkwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Polisi inayonolewa na kocha Etienne Ndayiragije ilijikuta ikifungwa mabao 2-0, lakini ushindi wa 3-1 iliyopata ugenini wiki iliyopita umewabeba kwani matokeo ya jumla yamekuwa sare ya 3-3, lakini maafande hao wa Kenya wamefuzu kwa faida ya bao la ugenini dhidi ya wapinzani wao hao.
Mabao ya Marsis katika dakika ya 33 na jingine la penalti iliyopigwa na Ibrahim Bangura yalitosha kuifanya Mogadishu kulipa kisasi mbele ya wenyeji na kuonekana kama ingepindua meza, lakini ilishindwa kutumia nafasi ilizotengeneza kuongeza bao jingine ambao lingeweza kuwavusha.
Kwa matokeo hayo Kenya Polisi imeungana na Nairobi United iliyoiwakilisha nchi hiyo katika Kombe la Shirikisho Afrika kutinga raundi ya pili baada ya ndugu zao hao kupenya jana mbele ya NEC ya Uganda pia kwa faida ya bao la ugenini kutokana na matokeo ya jumla kuwa pia 3-3.
Nairobi ilitoka sare ya 2-2 ugenini wiki iliyopita kabla ya jana kulazimisha pia sare ya 1-1 baada ya wageni wao kutangulia kupata bao na Dancun Omala kuchomoa kipindi cha pili na kuivusha timu hiyo.
Kwa mujibu wa ratiba ya michuano hiyo kwa sasa Polisi Kenya itakutana na mshindi wa mechi kati ya Jamus na Al Hilal, huku Nairobi United ikitarajiwa kuvaana na Etoile du Sahel ya Tunisia, mechi za mkondo wa kwanza zitapigwa kati ya Oktoba 17-19 na zile za marudiano zitapigwa Oktoba 24-26.