Kocha mpya Gor aanza kuchocha

Kocha mpya Gor aanza kuchocha

PALE Gor Mahia, imekuwa kawaida kuona sura mpya za makocha tena wazungu ambapo kwa kipindi cha miaka miwili wamepita makocha zaidi ya 10 wazungu.

Wiki hii walimleta mwingine, Jonathan McKinstry, aliyewahi kuwa kocha wa timu ya taifa ya Uganda Cranes.

Na kama tu watangulizi wake, McKinstry katua Gor kwa vishindo, tayari ameanza chocha kwa kusema kikosi alichoridhi hakiko poa sana.

Baada ya kushuhudia mechi ya kiraifiki kati ya Gor dhidi ya Mombasa Combined, kwenye mechi yao ya kwanza ya maandalizi ya msimu mpya, McKinstry ameona mapungufu kibao. Hii ni licha ya kuwa timu ndio mwanzo imengia mazoezini hivi majuzi baada ya kuwa na likizo ya zaidi ya mwezi mmoja tangu msimu 2021/22 ulipomalizika.

“Kwa nilichokiona siwezi kusema kikosi sio kizuri lakini katika idara kuna kazi nyingi ya kufanya ili kuiboresha timu. Naamini ndani ya wiki chache tulizonazo kabla ya msimu mpya kuanza, nitakuwa nimerekebisha mapungufu yote niliyoyaona,” McKinstry alisema.

Kocha huyo amekwenda zaidi na kuwaonya wachezaji wake akiwataka waonyeshe viwango lao sivyo atalazimika kufanya usajili mpya kujaza nafasi zao endapo hawatambamba.

“Kila kocha mpya hutaka kufanya usajili wa wachezaji wapya, wachezaji anaoamini wataendana na filosofia yake. Ila mimi nipo tofauti kidogo, napenda kuwapevusha wachezaji nilionao na kwasababu tuna marufuku ya kufanya usajili, basi nafikiri hawa waliopo wana muda wa kutosha kujitahidi kuniridhisha,” alisema McKinstry.

Gor wapo kwenye marufuku ya kutosajili hadi dirisha kubwa la usajili 2023 baada ya kukiuka maaagizo ya FIFA kuwalipa fidia wachezaji wao wawili pamoja na kocha wa zamani Steven Pollack waliovunjiwa mikataba yao pasipo kufuata utaratibu.