Zimbabwe waaga mashindano Chan

Timu ya Zimbabwe imekuwa ya kwanza kuondoshwa kwenye michuano ya Chan baada ya kupokea vipigo viwili mfululizo katika hatua ya Makundi.
Zimbabwe iliyokuwa imepangwa kundi A pamoja na timu za Cameroon, Burkina Faso na Mali haijashinda mchezo mmoja kati ya miwili iliyocheza ikipoteza kwenye mechi ya ufunguzi dhidi ya Cameroon kwa kufungwa bao 1-0, pia jana imefungwa mchezo wa pili na Burkina Faso kwa bao 3-1.
Katika kundi hilo ambalo timu mbili pekee ndizo zitakazofuzu kuelekea hatua ya robo fainali Zimbabwe anaburuza mkia akiwa amebakiwa na mchezo mmoja mkononi ambao matokeo yeyote atakayopata hayatakuwa na faida katika kusonga mbele.

Kwa tafsiri nyepesi ni kwamba safari ya Zimbabwe kuwania ubingwa wa michuano hiyo inayoendelea nchini Cameroon imekwamia hapo na mchezo wake wa mwisho dhidi ya Mali utachezwa Januari 24.
Mchezo mwingine wa jana ulikua wa vigogo wa kundi hilo (A) kati ya Cameroon na Mali mchezo uliomalizika kwa sare ya bao 1-1.
Michezo mingine ya leo itakuwa ya kundi B ambapo saa 1 usiku wataanza Libya vs D.R Congo na saa 4 usiku ni Congo dhidi ya Niger.