Zahera, Makambo walivyonogesha hafla ya Yanga

Muktasari:

  • Mwanaspoti lilikuwapo ukumbini hapo mwanzo mwisho na linakupa yote yaliyojiri kuonyesha Yanga imezaliwa upya chini ya Mwenyekiti, Dk Mshindo Msolla.

KAMA hujui ni kwamba ile harambee ya Yanga ya kusaka fedha za usajili kwa msimu ujao itafanyika Juni 15, lakini unaambiwa juzi Jumamosi walifanya hafla moja matata ambapo Wakongomani Kocha Mwinyi Zahera na Straika Heritier Makambo waliinogesha kinoma.

Ndio, si mnajua Makambo na Zahera walikuwa gumzo baada ya kusepa kimyakimya Yanga kisha kuibukia Guinea kulipovuja picha za straika huyo akiwa na uzi wa Horoya AC iliyodai imemsainisha mkataba wa miaka mitatu kukipiga katika klabu hiyo maarufu.

Lakinij pale kwenye Hoteli ya Serena, jijini Dar es Salaam mabosi wa Yanga walifanya hafla ya kuwapongeza nyota wao na kuhudhuriwa na mastaa mbalimbali wakiwamo nyota wa zamani wa klabu hiyo na viongozi wapya ya Yanga.

Utamu ulikuwa ni sapraizi ambayo Makambo na Zahera waliyoifanya kwa kuibuka kwenye hafla hiyo ambayo ilihudhuriwa na kikosi kizima cha Yanga cha msimu huu, huku yakiibuka mambo mazito.

Mwanaspoti lilikuwapo ukumbini hapo mwanzo mwisho na linakupa yote yaliyojiri kuonyesha Yanga imezaliwa upya chini ya Mwenyekiti, Dk Mshindo Msolla.

YANGA WAVUNJA MAKUNDI

Katika hafla hiyo hatua kubwa ya Yanga ni wagombea mbalimbali kuvunja makundi ya kambi za uchaguzi uliofanyika Mei 5 mwaka huu.

Ndani ya hafla hiyo wagombea mbalimbali wakiwemo Mbaraka Igangula, aliyewania nafasi ya m,wenyekiti, Yono Kevela aliyegombea makamu mwenyekiti na wote kwa bahati mbaya kura hazikutosha walitangaza rasmi kuvunja makundi kisha kuungana pamoja kuijenga klabu yao.

Hata hivyo, Mwenyekiti wao, Dk. Mshindo Msolla pia alitangaza uamuzi wa kuvunja kambi hiyo umefanywa na aliyekuwa mgombea na mpinzani wake, Dk Jonas Tiboroha ataupa ushirikiano mkubwa, huku akichangia Sh 1 milioni katika zoezi la kukusanya fedha.

“Dk. Tiboroha amenitumia ujumbe huo na kwamba yuko pamoja na Yanga kuhakikisha tunapata maendeleo na kama nilivyosema awali wakati wa kampuni kuwa nitaimarisha umoja hili nitazidi kulisimamia,” alisema Msolla.

MAKAMBO KIVUTIO

Tukio lingine lililokuwa la kuvutia ni uwepo wa Kocha Zahera na mshambuliaji, Heritier Makambo ambao baada ya safari ya Guinea waliwahi tafrija hiyo.

Makambo aliye mbioni kuuzwa alionekana kuwavutia wadau wengi sambamba na Zahera wakishangiliwa zaidi.

Hata hivyo, Zahera alipagawisha zaidi baada ya kusimulia safari yake ya kuachana na klabu ya Buildcon ya Zambia iliyokuwa imepanga kumpa fedha nyingi kisha kuja kujiunga na Yanga.

ZAHERA AMWAGA CHOZI

Wakati akisimulia simulizi hiyo ndefu ya maisha yake ya kutua Yanga, Kocha Zahera alijikuta akiangua kilio alipotamka hana baba wala mama na kwamba uamuzi wake wa kuja Yanga ulitokana na ushawishi wa mdogo wake wa pekee katika familia yao waliyobaki naye ambaye ndiye aliyemshawishi kuja nchini.

Mdogo wake huyo anayefanya kazi na bosi wa Yanga, Hussein Ndama ndiye aliyemshawishi kuachana na Wazambia hao kisha kuja nchini.

JUNI 15 IPO KAZI

Mwenyekiti wa Kamati ya Kuhamasisha Michango, Anthony Mavunde ambaye ni Mbunge wa Dodoma alitangaza rasmi baada ya futari hiyo sasa tukio kubwa la kuzindua harambee kubwa jijini Dar es Salaam sasa itafanyika Juni 15, 2019 Diamond Jubilee.

Alisema katika hafla hiyo inatarajia kuwa na wageni waliikwa wasiopungua 1000 ambao kutakuwa na ada tofauti za kushiriki ambapo lengo ni kukusanya kiasi cha sh 1.5 bilioni.

Awali harambee hiyo ilipangwa kufanyika juzi Mei 18, lakini kuwepo kwa Mfungo wa Ramadhani uliifanya kamati kuisogeza mbele kisha kuandaa hafla ya kuwapa heko vijana wao kwa kuiwezesha Yanga kupambania ubingwa.