ZA CHINICHINI: Sven akichomoka hapa, aisee akatambike

Friday October 30 2020
sven pic

HUKO Msimbazi mambo sio shwari, kwani mabosi wa klabu ya Simba wameanza kupangusa benchi lao la ufundi kwa kuwaondoa kocha wa makipa, Mwarami Mohamed ‘Shilton’ na meneja wao, Patrick Rweyemamu huku Kocha Mkuu, Sven Vandenbroeck akiwekwa mtegoni na wasaidizi wake.

Wazee wa redio za mbao, wamepenyeza za chini chini kwamba safari hii, Mbelgiji huyo akichomoka kwenye mtego huo, eti atakuwa ameaga kwao vizuri.

Wanyetishaji hao wamedai siku za Sven zinahesabika Msimbazi, kwani inaonekana vigogo wa klabu hiyo, walikuwa wakimwinda kwa siku nyingi, ila hawakuwa na mtego wa kumkamatia, lakini matokeo mabaya ya mechi mbili mfululizo zimewapa bakora ya kumchapi kocha huyo.

Simba ya Sven ilikumbana na vipigo hivyo ikianza kunyooshwa na Tanzania Prisons kwa kucharazwa bao 1-0 mjini Sumbawanga kisha kupapaswa tena na Ruvu Shooting bao 1-0.

Inasemekana mabosi wa Simba wamemtega Sven katika michezo miwili ijayo kabla ya kuvaana na Yanga Novemba 7, akitakiwa kupata ushindi dhidi ya Mwadui na Kagera Sugar.

Kitendo cha kuifunga Mwadui halafu wakapoteza dhidi ya Kagera inaelezwa pia kuwa ni hatari kwake.

Advertisement
Advertisement