Yanga yazizuga Azam, Simba

Kikosi hiki cha Simba kilicheza mechi ya kirafiki na Mtibwa Sugar, Desemba mwaka jana
na kupigwa mabao 4-2 pale Azam Complex. Ikiwa imepita miezi 11 tu, ni nyota wanne
waliosalia kikosini hapo ambao ni Said Ndemla (jezi namba 13), Awadhi Juma (jezi namba
16), Ibrahim Ajibu (jezi namba 23) na Hassan Isihaka (jezi namba 5). Hata hivyo ni Ndemla
na Isihaka tu wenye nafasi katika kikosi cha kwanza cha sasa.
Muktasari:
Yanga na Azam zimeweka wazi kwamba hazitasajili ingawa viongozi wa Simba waliozungumza na Mwanaspoti wiki hii walionyesha kuwa na wasiwasi na hilo wakidai kwamba Yanga ni kawaida yao kuzuga, lakini lazima watasajili mtu mmoja hata kabla ya kumalizika kwa Kombe la Chalenji nchini Ethiopia.
DIRISHA dogo la usajili wa Ligi Kuu Bara litafunguliwa kesho Jumapili ambapo litakuwa wazi hadi Desemba 15 litakapofungwa ikiwa ni siku mbili baada ya mechi ngumu ya Simba na Azam itakayopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Desemba 12.
Yanga na Azam zimeweka wazi kwamba hazitasajili ingawa viongozi wa Simba waliozungumza na Mwanaspoti wiki hii walionyesha kuwa na wasiwasi na hilo wakidai kwamba Yanga ni kawaida yao kuzuga, lakini lazima watasajili mtu mmoja hata kabla ya kumalizika kwa Kombe la Chalenji nchini Ethiopia.
Simba inaamini kwamba Azam na Yanga hazitasajili mastaa wengi, jambo ambalo huenda likawapunguzia mzigo wa kuwapata wachezaji kwa bei chee kwa vile hawatakuwa na ushindani mkubwa.
Klabu hiyo imesama itajikita kwenye mapendekezo ya kocha, Dylan Kerr, ambaye hata hivyo ana nafasi ndogo ya kurejea Msimbazi kwa vile klabu hiyo iko kwenye mazungumzo na Mrundi, Kaze Cedrick ambaye ana rekodi kubwa kuliko Kerr.
Kerr alipendekeza Simba isajili beki na straika. Tayari Simba imefanya mazungumzo na Bryan Majegwa, Farouk Miya, Erissa Sekisambu wote wa Uganda, Laudit Mavugo, Kelvin Ndayisenga wote wa Burundi lakini mpaka sasa ina uhakika wa kumrejesha Raphael Kiongera wa Kenya. Ilimletea pia Dar es Salaam, Nova Lufugo wa African Sports kwa ajili ya mazungumzo, lakini ikampotezea na kumwambia arudi kwao watamwita tena.
Yanga ambayo itashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika, tayari imeanza mazoezi jijini Dar es Salaam. Imeanza na wachezaji sita tu wa timu kubwa ingawa staa wa kigeni aliyetangulia kuripoti mpaka sasa ni kiungo rasta Thabani Kamusoko.
Wachezaji wengine ambao tayari wamesharipoti ni makipa Deogratias Munishi ‘Dida’,Benedicto Tinoco mabeki Patrick Ngonyani,Oscar Joshua huku viungo wakiwa Geofrey Mwashiuya na Deus Kaseke. Wengine wapo kwenye timu za Taifa huku baadhi wakiwa na matatizo binafsi.
YANGA WAANDAA
BILIONI
Yanga imefanya tathimini yake katika ushiriki wa Ligi ya Mabingwa Afrika na kuweka bajeti ya maana ya utangulizi.
Katibu Mkuu wa Yanga, Dk. Jonas Tiboroha, alisema wanataka kuingia katika mbio za ushiriki wa Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kishindo ambapo katika hatua ya awali kabla ya kufikia hatua ya mtoano wamepanga kutumia kiasi cha Sh1.5 bilioni.
Tiboroha ambaye kitaaluma pia ni kocha wa soka, amesema katika msimu uliopita kikosi chao kilitumia kiasi cha Sh1.2 bilioni mpaka kinaondolewa na Etoile du Sahel ya Tunisia ambapo sasa wanataka kutafuta nguvu hiyo kuweza kuleta upinzani wa kweli katika vigogo watakavyokutana navyo.
Alisema kiasi hicho cha fedha kitatumika katika kuiandaa timu yao katika maandalizi ya kabla ya kuanza kwa michuano ambapo wamepanga kuwa na kambi fupi ya wiki mbili huku pia wakisaka makampuni mbalimbali katika kutunisha fungu hilo.
“Katika Ligi ya Mabingwa tutakutana na timu ngumu kidogo, kwa tathimini yetu kikosi chetu kinaweza kabisa kushindana endapo kitaandaliwa vyema na wachezaji kushika kile wanachofundishwa na kocha wetu Hans (Pluijm) ambaye uzoefu wake ni mtaji mzuri kwetu,”alisema Tiboroha.
“Msimu huu uongozi wetu kuanzia Mwenyekiti (Yusuf Manji) tumedhamiria kufika mbali katika kuwania hili taji kubwa, sasa katika safari zetu zote tunajipanga tuwe tunasafiri kwa ndege maalumu katika safari zetu tena siku moja au mbili kabla ya mchezo na mechi inapokwisha turudi.”
Kama Yanga itafanikiwa kunusa hatua ya makundi ya michuano hiyo itakuwa imejihakikishia si chini ya dola 400, 000 (Sh800 milioni).