Yanga yavunja mwiko Mkwakwani

Yanga yavunja mwiko Mkwakwani

Yanga imefanikiwa kupata ushindi mzuri wa mabao 2-0 lakini kikubwa kikawa kufanikiwa kuvunja mwiko wa kutopata matokeo ya ushindi kwa miaka mingi.

Yanga imepata ushindi huo wakifunga bao katika kila kipindi kimoja ambapo dakika 41 za kipindi cha kwanza walipata bao lao kupitia mshambuliaji Fiston Mayele akimalizia kwa kichwa krosi safi ya beki wake wa kulia Djuma Shaban.

Hata hivyo Yanga ilitawala kipindi chote cha kwanza wakitengeneza mashambulizi mengi makali lakini wakikosa umakini wa kuzitumia.

Coastal Union licha ya kuanza kwa kasi wakitengeneza shambulizi zuri katika dakika ya nne tu lakini wakapotea na kumaliza dakika 45 za kipindi cha kwanza bila hata shuti lililolenga lango.

Kipindi cha pili timu zote zilifanya mabadiliko mara tatu lakini kuingia kwa Farid Mussa kuliipa faida Yanga wakipata bao la kukamilisha ushindi dakika ya 90 likifungwa na mkongwe Said Ntibazonkiza.

Bao hilo la Ntibazonkiza limetokana  na mkongwe huyo kugongeana vyema na Farid kisha kufumua shuti kali la juu lililoihakikishia ushindi Yanga.

Ushindi huo unaifanya Yanga kuendelea kukaa kileleni wakifikisha pointi 32 baada ya kucheza mechi 12.