Yanga yatesti kwa JKT Tanzania leo

NYOTA wa Yanga wanashuka uwanjani leo kujipima dhidi ya maafande wa JKT Tanzania iliyopo Ligi ya Championship ili kujiweka fiti kabla ya kuvaana na Azam wikiendi hii, huku kiiungo wake, Mukoko Tonombe akituma salamu mapema msimu huu Jangwani wana jambo lao.

Yanga iliingia kambini Ijumaa iliyopita na Kocha Nasreddine Nabi alikaririwa akisema anaujua ugumu wa mchezo dhidi ya Azam na kutaka mechi kama mbili za kutesti mitambo kabla ya kuvaana na wanalambalamba hao ambao juzi waliong’olewa katika Kombe la Shirikisho Afrika na Pyramids.

Kikosi hicho kitashuka uwanjani kwenye uwanja wao wa mazoezi wa Avic ikiwa na kumbukumbu ya ushindi wa mabao 2-0 wa ugenini dhidi ya KMC katika Ligi Kuu Bara.

Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh alisema jana, kocha amehitaji mchezo huo ili kubaini mapungufu na ubora wa nyota wake kabla ya mchezo dhidi ya Azam na watavaana na JKT. Saleh alisema wachezaji wote wapo fiti na kila mmoja anaonyesha morali ya juu na benchi la ufundi litatumia muda huu kuhakikisha wanayafanyia kazi baadhi ya makosa yaliyojitokeza nyuma.

Katika hatua nyingine, kiungo Mukoko ambaye amekuwa akijifua ili kuprejesha namba yake kikosi, amewatumia salama wapinzani wengine ndani ya Ligi Kuu Yanga msimu huu ni wao.

Mukoko aliandika kwenye akaunti yake Instagram; “Asante GSM, Wananchi msimu huu tutashinda ubingwa wa Ligi, tuseme ameen.” Ujumbe huo unarejea mahojiano yake na Mwanaspoti wikiendi iliyopita kwa mziki uliopo Jangwani haoni cha kuwazuia wasirejeshe taji la ligi hiyo waliolikosa kwa misimu minne mfululizo.