Yanga yasimamisha shughuli Msimbazi, yatamba na makombe yao

Muktasari:
- Barabara zote za mtaa wa Msimbazi zilisimamisha zoezi la kupitisha magari kwa muda kutokana msongamano mkubwa wa watu uliotanda barabarani.
PAREDI la Yanga limesimamisha mwendokasi eneo la Msimbazi baada ya kusimama kwa muda wakati gari iliyobeba mataji, wachezaji na viongozi wa timu hiyo lilipofika eneo la jengo la watani zao Simba.
Barabara zote za mtaa wa Msimbazi zilisimamisha zoezi la kupitisha magari kwa muda kutokana msongamano mkubwa wa watu uliotanda barabarani.
Jengo la Simba ambalo limepangishwa wafanyabiashara pia limejaa mashabiki wa Simba na Yanga kila mmoja anatoa ishara yake wapo wanaofurahisha na wanachokifanya mashabiki huku wengine wakizomea.
Magorofa marefu yaliyopo pembezoni mwa barabara biashara zimesimama kwa muda kutokana na mashabiki kupanda juu kushuhudia paredi hilo, huku Clatous Chama ambaye aliwahi kuichezea Simba akipewa kombe anyanyue juu.
Kwenye jengo la Simba bendera za timu hiyo zilinyanyuliwa huku mashabiki wengine waliovaa jezi za Simba wakionyesha ishara ya kuzomea na kupepea skafu za timu yao juu.
Hata hivyo msafara ulipofika maeneo ya Msimbazi ulisimama huku Afisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe akionyesha makombe matano kwa mashabiki wa Simba kuanzia lile la Toyota cup, Ngao ya jamii, Ligi Kuu Bara na lile la FA.
Yanga imefanya paredi kusherehekea mafanikio yao ya msimu huu baada ya kutwaa makombe matano, ikitwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara, Kombe la Shirikisho la CRDB, Kombe la Toyota, Ngao ya Jamii pamoja na ubingwa wa Kombe la Muungano.