Yanga yapania Afrika

TAKWIMU zisizovutia ugenini za Al Hilal zimewapa jeuri mabosi wa Yanga ambao wamepanga kuhakikisha wanaimalizia shughuli dhidi ya Wasudan hao katika mchezo wa kwanza nyumbani huku wakiahidi kuwa kwa gharama yoyote ile safari hii Yanga ni lazima ifuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Takwimu za mechi 10 zilizopita za hivi karibuni za Ligi ya Mabingwa, zinathibitisha kuwa Al Hilal wamekuwa si lolote pindi wawapo ugenini kwani katika idadi hiyo ya michezo, wameibuka na ushindi mara moja tu, wakitoka sare tatu huku wakipoteza michezo sita.
Kana kwamba haitoshi, safu yake ya ulinzi imekuwa na hulka ya kuruhusu bao pindi inapokuwa ugenini na kudhihirisha hilo, katika mechi hizo 10 zilizopita, wamefungwa jumla ya mabao 13 ikiwa ni wastani wa bao 1.3 katika kila mechi.
Na katika kuhakikisha hilo linatimia habari za uhakika ambazo gazeti hili linazo ni kwamba miongoni mwa mikakati ambayo Yanga imeiweka ili kuhakikisha Al Hilal hawatoki ni kumpa Nabi vielelezo vyote lakini kuweka viingilio vya chini katika mechi yao ya hapa nyumbani ili umati mkubwa wa mashabiki ujitokeze uwanjani kuipa sapoti timu yao.
“Kwenye mchezo wa marudiano utakaofanyika Sudani, Nipende kuwataarifu kwamba maoni yenu tumeyapokea na tunayafanyia kazi. Viongozi wameniagiza nifatilie utaratibu, muda utakapofika tutawataarifu,” alisema kaimu katibu mkuu wa Yanga, Saimon Patrick.
Makamu wa Rais wa Yanga, Arafat Haji, alisema,”Lengo ni makundi, hatua moja tumevuka macho yote hatua inayofuata.”