Yanga yapaa kwenda Mbeya, yawaacha wawili Dar

Muktasari:
- Yanga itavaana na Prisons kwenye Uwanja wa Sokoine, jijini humo keshokutwa Jumatano ikiwa ni moja kati ya mechi tati ilizokabiwa nazo kabla ya kufunga msimu, huku ikiwa katika mbio za kusaka ubingwa kwa msimu wa nne ikichuana na Simba wanaoshika nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi.
KIKOSI cha Yanga kimeondoka jioni hii kutoka jijini Dar es Salaam kwenda Mbeya tayari kwa mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Tanzania Prisons huku ikiwabakiza mjini wachezaji wawili tu miongoni mwa nyota wa kikosi hicho kinachonolewa na kocha Miloud Hamdi.
Yanga itavaana na Prisons kwenye Uwanja wa Sokoine, jijini humo keshokutwa Jumatano ikiwa ni moja kati ya mechi tati ilizokabiwa nazo kabla ya kufunga msimu, huku ikiwa katika mbio za kusaka ubingwa kwa msimu wa nne ikichuana na Simba wanaoshika nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi.
Kikosi hicho cha Hamdi, kimeondoka ikiwa na nyota wote isipokuwa straika Kennedy Musonda na beki wa kulia Yao Kouassi ambao ni majeruhi. Yao anajiuguza goti lililofanyiwa upasuaji hivi akribuni, wakati Musonda akipata majeruhi.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mratibu wa Yanga, Hafidh Saleh amesema wameondoka na wachezaji wote isipokuwa wawili ambao ni majeruhi na mikakati yao ni kuhakikisha wanaibuka na ushindi ili kujihakikishia nafasi ya kutetea taji.
"Ni wachezaji wawili tu ambao hatujasafiri nao ambao ni Yao na Musonda wameachwa kwa sababu ni wagonjwa lakini wengine wote wapo tayari kwa safari na kuipambania timu yetu kutetea taji Jumatano dhidi ya Tanzania Prisons," amesema Hafidh.
Katika mechi ya kwanza ikipigwa jijini Dar es Salaam, Yanga ikiwa nyumbani Desemba 22 mwaka jana iliibuka na ushindi wa mabao 4-0 yaliyowekwa kambani na Bacca ambaye alifunga mabao mawili, mwingine yalifungwa na Prince Dube na Clement Mzize.
Nyota waliosafiri ni makipa; Djigui Diarra, Abuutwalib Mshery na Khomeiny Aboubakar, huku mabeki wakiwa ni; Nickson Kibabage, Kibwana Shomari, Dickson Job, Bakari Mwamnyeto, Ibrahim Bacca na Chadrack Boka, wakati viungo walikuwa Maxi Nzengeli, Khalid Aucho, Pacome Zouzoua, Mudathir Yahya, Aziz Andambwile, Salum Abubakar na Duke Abuya.
Wengine ni Clatous Chama, Jonas Mkude na Denis Nkane, ilihali washambuliaji waliopaa na timu ni Clement Mzize na Prince Dube na wachdezaji kutoka timu ya vijana.