Makipa wazawa upepo sio mzuri

Muktasari:
- Kilionekana kina vijana ambao watarithi vyema mikoba ya kaka zao kina Juma Kaseja, Shaaban Kado, Ivo Mapunda, Shaaban Dihile, Mwadini Ally na wengineo ambao umri ulianza kuwatupa mkono.
HIKI kizazi cha sasa cha makipa wazawa kilikuwa na mwanzo mzuri kuanzia kipindi cha miaka ya 2010 ambapo wengi walianza kuibuka wakiwa watoto hasa katika timu za vijana za Tanzania.
Kilionekana kina vijana ambao watarithi vyema mikoba ya kaka zao kina Juma Kaseja, Shaaban Kado, Ivo Mapunda, Shaaban Dihile, Mwadini Ally na wengineo ambao umri ulianza kuwatupa mkono.
Na bahati nzuri watoto wengi wakapigania nafasi na wakawa na nafasi ya kucheza mara kwa mara kwenye vikosi vya timu zao jambo ambalo lilianza kutupa mwanga kwamba timu yetu ya taifa itakuwa na wigo mpana wa uteuzi wa makipa.
Aishi Manula akawa kipa tegemeo Azam na baadaye Simba, Metacha Mnata akaibukia kuwa mmoja wa makipa wanaotabiriwa kufanya vyema hadi akanaswa Yanga na akawa anacheza akiwa panga pangua kikosini.
Wengine walioibuka na wakawa chaguo la kwanza kwenye timu zao ni kama Aaron Kalambo (Tanzania Prisons), Abutwalib Mshery (Mtibwa Sugar), Wilbol Maseke (Azam), Abubakar Khomeiny (Yanga), David Kissu (Gor Mahia), Soud Dondola (KMC), Rahim Shecky (Mbao FC) na Daniel Mgore (Biashara United).
Lakini ghafla ndani ya miaka michache ya hivi karibuni mambo yameonekana kuwa magumu kwa kundi hilo la vijana lililokuwa linaonyesha mwanga mzuri kwenye ukipa kwani karibia wote wanasotea benchi kwenye timu zao na hawaonyeshi dalili kama watacheza.
Makipa wa kigeni waliopo kwenye timu zao wanaonekana kuaminiwa zaidi na makocha wanaogopa kuwapa nafasi wazawa wetu hata katika mechi dhidi ya timu za kawaida ambazo wanaweza kucheza ili angalau wapate hali ya kujiamini na kulinda viwango vyao.
Kinachouma hata wale wachache ambao angalau walionyesha kufanya vizuri kama Yona Amos na Hussein Masalanga, sasa hivi wameanza kugawana dakika na makipa wa kigeni kwenye timu zao.
Amebakia Yakoub Suleiman wa JKT Tanzania pekee ambaye anaonekana kuwa na muendelezo wa kucheza na imani ya benchi la ufundi kwake huku wengine wakibaki wanatuumiza tu hapa kijiweni kwa kusotea kwao benchi.