Yanga yaja na mkakati mpya, Gamondi afunguka

Muktasari:

  • Yanga ambayo imepangwa kundi D na timu za CR Belouizdad, Al Ahly ya Misri na Medeama ya Ghana, itashuka Desemba 2, mwaka huu ikiwa kwenye uwanja wake wa nyumbani Mkapa

YANGA Jumamosi itarudi Kimataifa. Itakuwa uwanja wa Mkapa kuwakabirisha Al Ahly na kocha Miguel Gamondi amesema anakazi kubwa kuhakikisha washambuliaji wake wanatumia vyema nafasi za kufunga ili kuwarudisha kwenye mstari baada ya kupoteza mabao 3-0 ugenini dhidi ya CR Belouizdad.

Lakini mabeki wake nao wana mkakati wao. Gamondi ameliambia Mwanaspoti kuwa; “Mchezo uliopita umekuwa darasa hatutaki kurudia tena makosa tunahitaji kutumia vyema uwanja wetu wa nyumbani kwa lengo la kuhakikisha tunarudi kwenye ushindani japo haitakuwa rahisi kwani hatua tuliyopo inahitaji pointi kwa kila timu kujihakikishia nafasi ya kusonga.”

“Benchi la ufundi, wachezaji na mashabiki wetu wanatambua ugumu wa huo mchezo tunaendelea kujiweka imara ili kuhakikisha tunasawazisha makosa tuliyoyafanya mchezo uliopita na kujihakikishia nafasi ya kusonga hatua inayofuata,” alisema.

“Kuna kazi kubwa inahitajika kufanyika kwa wachezaji wangu ili tuweze kupata matokeo nyumbani naamini hilo litafanikiwa kutokana na maelekezo ya kiufundi niliyo wapatia;

“Malengo yetu ni kusonga hatua inayofuata na hilo naamini litawezekana kama wachezaji wangu watacheza kwa malengo na ushindani, kukosa matokeo kwenye mchezo wa kwanza haiwezi kuwa sababu ya kutukatisha tamaa bado tuna nafasi ya kufanya vizuri hasa tukianza na matokeo mazuri nyumbani,” alisema Gamondi.

Yanga ambayo imepangwa kundi D na timu za CR Belouizdad, Al Ahly ya Misri na Medeama ya Ghana, itashuka Desemba 2, mwaka huu ikiwa kwenye uwanja wake wa nyumbani Mkapa.


MABEKI WAPANIA JUMAMOSI

Dickson Job alisema kupoteza kwao dhidi ya Belouizdad ya Algeria haina maana kwamba wametoka kwenye mashindano.

“Tunarudi kucheza dhidi ya timu bora Afrika na tunawaheshimu, ila hatuwezi kuwaogopa kwani mchezo ni dakika 90 na wachezaji wa pande zote wana uwezo mkubwa wa kucheza.

“Tutaongeza umakini wa kupata matokeo lakini pia kuhakikisha sisi kama mabeki hatuwapi nafasi wapinzani kufunga,” alisema Job.

Aliongeza kuwa haitakuwa rahisi kwao kupoteza mara mbili hasa uwanja wa nyumbani. Lomalisa Mutambala, alisema kwenye kundi lao kila aliyecheza nyumbani kwake ameshinda na wao wanarudi nyumbani kutengeneza ushindi wao kwanza.

Aliongeza kuwa ana uzoefu mkubwa kwenye mechi kama hizi amecheza dhidi ya Al Ahly mara nyingi anajua wanahesabu gani wakiwa wanacheza ugenini atawashauri wenzake kwenye maandalizi yao na hata kwenye mechi

Lomalisa alisema kwenye maandalizi yao yanayoanza leo watasikiliza kwanza makocha wao wanakuja na mipango gani dhidi ya Al Ahly lakini mashabiki wao wasivunjike moyo waje uwanjani

“Hata msimu uliopita wapo waliosema tutapoteza mbele ya Mazembe lakini  tulishinda mechi zote hivyo tutawashangaza,” alisema Lomalisa.