Yanga yaizidi akili Simba kambini Pemba

Kikosi cha Yanga.
Muktasari:
Lakini kocha wao Hans Pluijm hataki kabisa kuuza silaha kwa Simba na hata ukifuatilia mazoezi yake amekuwa mjanja sana kwenye safu ya ulinzi ambapo amekuwa akibadili mabeki, ili Simba wasijue picha hali ya ukuta itakavyokuwa Jumamosi.
MASHABIKI wa Yanga wanatambua kwamba, Kelvin Yondani, hatakuwepo katika mchezo dhidi ya Simba na kutamani kujua ukuta wao utakuwaje Jumamosi timu hizo zitakapoumana katika mechi ya Ligi Kuu Bara.
Lakini kocha wao Hans Pluijm hataki kabisa kuuza silaha kwa Simba na hata ukifuatilia mazoezi yake amekuwa mjanja sana kwenye safu ya ulinzi ambapo amekuwa akibadili mabeki, ili Simba wasijue picha hali ya ukuta itakavyokuwa Jumamosi.
Wakiwa mazoezini kwenye Uwanja wa Gombani hapa Chake Chake, Pemba, Pluijm amekuwa akiwabadili mabeki hao ambapo kuna wakati amekuwa akimweka Pato Ngonyani na Mbuyu Twite lakini mara nyingine anamsimamisha Yondani na Nadir Haroub ‘Cannavaro’.
Lakini pia anamchezesha Cannavaro na Vicent Bossou jambo ambalo ni ngumu kubaini ni safu ipi itasimama, lakini Pluijm na msaidizi wake, Juma Mwambusi ukiangalia sura zao zinaonyesha kuna kitu wanakificha.
Katika pacha hizo hakuna hata moja aliyoweza kuirudia mara nyingi ambapo baadaye amekuwa akibadili zoezi tofauti na kupoteza kabisa akili ya kuitambulisha safu hiyo ya ulinzi.
Katika ulinzi beki mmoja tu Juma Abdul ndiye anaonekana kuwa katika sura ya mchezo, lakini hali kama hiyo pia imekuwa katika nafasi ya beki wa kushoto ambapo Oscar Joshua amekuwa akibadilishana nafasi ya Mwinyi Haji aliyerudi huku golini pia nafasi kubwa akionekana kupewa Ally Mustapha ‘Barthez’ambaye tayari alishaonekana kupewa majukumu hayo katika mchezo dhidi ya Simba.
“Kuhusu beki hilo nalijua mimi nitafanya nini na nitampanga nani ili kuweza kuwadhibiti Simba,” alisema Pluijm ambaye ni beki wa zamani wa FC Den Bosch.
UHALISIA
Kwa mujibu wa dondoo za kiufundi na utendaji wa mabeki wa Yanga kwa nyakati tofauti hakuna uwezekano wa Pato kuanza kwenye kikosi cha kwanza wala Oscar.
Hakuna uwezekano wa Mbuyu Twite kuanza na Bossou ingawa kwenye mechi mbili za JKT Ruvu na Prisons walicheza pamoja ila Simba na Yanga ni habari nyingine. Labda Cannavaro aumie mazoezini leo au kesho lakini ana nafasi kubwa ya kuanza na Bossou.
Kushoto atasimama Haji Mwinyi wakati kulia atapadhibiti Juma Abdul na lango Ally Mustapha ‘Barthez’.
KAMBINI NA MAZOEZINI
YANGA hawataki kabisa kufanya makosa, unakumbuka staili yao ya kwanza katika mchezo wa kwanza sasa imejirudia tena wakiongeza umakini zaidi kwa kubana kona zote tena kwa unoko wa nguvu bila kuangalia mtu usoni.
Ukikutana na kiongozi yeyote wa Yanga kuanzia meneja wa timu, Hafidh Saleh, ukimaliza kumsalimia hakuna kingine utazungumza naye baada ya kuambiana kwamba hakuna mtu kuzungumza hali ambayo pia imetokea kwa mabosi wa juu wa klabu hiyo hata yule Jerry Muro mwenye maneno mengi amekaa kimya kama si yeye.
Staili hii pia Yanga waliitumia katika mchezo uliopita wakati wakikutana na Simba ambapo mwisho wa siku kikosi chao kiliibuka na ushindi wa mabao 2-0 na sasa wakanogewa na kuirudia tena wakisema Mnyama anauliwa kimyakimya hautangazi.
Kikosi hicho mbali na basi la wachezaji wanatumia gari moja ndogo aina ya Noah linalomilikiwa na hoteli ya kitalii ya Pemba Misali Sunset Beach waliyofikia ambapo gari hiyo hubeba viongozi wa benchi la ufundi ambalo hutembea kwa karibu na basi la wachezaji kuweka ulinzi kwa nyuma ingawa ndani ya basi kuna mlinzi maalumu.
MAZOEZI
Kama Simba inatarajia suala la kufunga ni la Donald Ngoma au Amisi Tambwe peke yake hiyo imekula kwao Yanga anafunga yoyote ambapo timu hiyo kwa pumzi waliyonayo sasa hata mabeki wamesisitizwa na Pluijm wapande wakafunge. Lakini sharti ni moja tu mpira unapopotea kasi ya kurudi nyuma inahitajika na ole wako uchelewe.
Katika mazoezi hayo ya jana kila mchezaji ameonekana kuwa fiti kwa stamina na pumzi lakini pia ukirudi katika kupiga pasi za ushindi hilo pia halikosekani pasi zinapigwa nyingi na kutengeneza mashambulizi makali.
Mazoezi yao yamekuwa ni mara mbili kwa siku tangu wamefika hapa.