Yanga yaivurugia JKT Queens

Muktasari:

  • Awali, mechi hiyo ilitakuwa kupigwa leo uwanjani hapo saa 10:00 jioni lakini kutokana na ratiba kuingiliana na mechi ya Yanga dhidi ya timu ya JKT Tanzania, imesogezwa na itachezwa kesho saa 4:00 asubuhi.

MCHEZO wa Ligi Kuu ya wanawake kati ya JKT Queens na Amani Queens umesogezwa mbele kutokana na muingiliano wa ratiba na mechi ya Yanga na JKT ambayo inapigwa leo kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Mbweni, Dar es Salaam.

Awali, mechi hiyo ilitakuwa kupigwa leo uwanjani hapo saa 10:00 jioni lakini kutokana na ratiba kuingiliana na mechi ya Yanga dhidi ya timu ya JKT Tanzania, imesogezwa na itachezwa kesho saa 4:00 asubuhi.

Mchezo wa Ligi Kuu ya wanaume kati ya JKT Tanzania na Yanga ulitakiwa kuchezwa jana, lakini uliahirishwa baada ya uwanja kujaa maji hivyo kusogezwa hadi leo.

Akizungumza na Mwanaspoti, Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), Clifford Ndimbo alisema wamelazimika kuusogeza mchezo huo kutokana na mvua hivyo mechi hiyo wa Ligi Kuu ya Wanawake itachezwa kesho asubuhi.

"Ni kweli leo wanacheza Yanga na JKT kwenye uwanja huohuo. Ratiba ziligongana. Ile ya wanawake kati ya JKT Queens na Amani Queens sasa watacheza kesho uwanjani hapo," alisema Ndimbo.

Zilipokutana timu hizo Januari 02 mwaka huu kwenye Uwanja wa Ilulu mkoani Lindi, Amani Queens ikiwa nyumbani ilipokea kichapo cha mabao 10-0 kutoka kwa mabingwa hao watetezi wa WPL.