Yanga yaitega Azam mbio za ubingwa

SULUHU iliyoipata Azam FC juzi jijini Dar es Salaam dhidi ya Coastal Union imeipunguzia presha Yanga kwenye mbio za ubingwa, kwani sasa Wanajangwani wana mechi 11 (ikiwamo dhidi ya Simba) ambazo wakishinda zote watatwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara walioukosa kwa misimu minne mfululizo iliyopita.
Kati ya mechi hizo 11 ambazo kama Yanga itashinda zote itakusanya jumla ya pointi 33, mechi tisa tu ikishinda itaiengua Azam kwenye mbio hizo za ubingwa na kusalia kuchuana na watetezi, Simba ambayo kama itashinda mechi zake zote ikiwamo ya leo dhidi ya Biashara itafikisha pointi 76.
Ipo hivi. Azam FC tayari imejikusanyia pointi 25 kwenye michezo 16 waliyocheza, sasa ili kuendelea kujihakikishia nafasi ya kutwaa taji msimu huu inatakiwa kushinda michezo yote 14 ikiwamo dhidi ya Yanga na Simba, lakini ikiziombea timu hizo mbili mabaya ili zipoteze michezo isiyopungua sita kati ya 14 iliyonayo Yanga na saba kati ya iliyonayo Simba yenye pointi 31 kwa michezo yao 15.
Azam FC ikishinda michezo yote 14 itafikisha pointi 67 wakati Yanga ikishinda michezo tisa kati ya 14 waliyonayo itafikisha pointi 69 ambapo zitawaondoa kabisa Wana Lambalamba kwenye mbio za ubingwa na kuziacha Simba na Yanga kutunishiana ubavu.
Wanalamba-lamba wana kibarua kingine Jumapili dhidi ya Polisi Tanzania na endapo watapoteza au kupata sare kwenye mchezo huo wataendelea kuishushia presha Yanga ambayo ndio kinara wa Ligi.
Wakati Azam FC ikimenyana na Polisi Tanzania, Yanga atakuwa ugenini dhidi ya Geita Gold, mchezo ambao unatarajiwa kuchezwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Katika michezo iliyobaki kwa timu hizo, Yanga ina mechi nyingi nyumbani, huku Azam FC akiwa na mechi nyingi ugenini hivyo kazi inabaki wa makocha wa timu hizo atakayechanga karata zake vizuri ndiye atakayeweza kutwaa taji. Kadhalika Simba kwenye mechi za duru la pili itacheza mechi nyingi ugenini kulinganisha na nyumbani, lakini inatakiwa kushinda zote huku ikiiombea Yanga ipoteze kadhaa ili itetee taji. Kwa msimu huu Yanga imeonekana moto kwelikweli na kama itashinda mechi zake zote zilizosalia, ina maana itafikisha pointi 84, pointi ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote, lakini ikipata ushindi katika mechi hata 11 tu ikiwamo dhidi ya Simba, basi itatangaza ubingwa mapema kwani itakuwa na uwezo wa kufikisha pointi 75 ambazo hazitaweza kufikiwa na Simba itakayokuwa na uwezo wa kufikisha alama 73, kama itapasuka kwa mtani kwenye mechi itakayopigwa mwezi ujao.
Mechi za Azam FC ikimaliza na Polisi Tanzania Jumapili itaifuata Namungo, Yanga, Geita Gold, Kagera Sugar, KMC, Mbeya City, Mtibwa, Ruvu Shooting, Mbeya Kwanza, Prisons, Dodoma jiji, Simba na Biashara.