Yanga yaitawala Simba nje ndani

Muktasari:

  • Mechi ya jana ilianza kwa timu hizo kushambuliana kwa zamu kuanzia dakika ya kwanza ya mchezo ingawa dakika ya nane, Yanga ilipata pigo baada ya beki wake Joyce Lomalisa kuumia na nafasi yake kuchukuliwa na Nickson Kibabage.

Ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu unazidi kuikaribia Yanga na sasa inahitajika kupata ushindi katika mechi tano na sare moja kati ya mechi nane ilizobakiza ili ijihakikishie ubingwa kwa mara ya tatu mfululizo pasipo kutegemea matokeo ya timu nyingine, lakini jingine kubwa ni matokeo ya jumla ya mabao 7-2 na pointi sita ambavyo Wananchi wamevuna dhidi ya Simba kwenye ligi msimu huu.

Ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Simba jana kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, ambao umefuatia ushindi ule mzito wa mabao 5-1 katika mzunguko wa kwanza, umeifanya Yanga kufikisha pointi 58 na kuzidi kujikita kileleni mwa msimamo wa Ligi na sasa inahitaji ushindi katika mechi tano na sate moja ili ifikishe pointi 74, ambazo haziwezi kufikiwa na timu nyingine kwani Simba yenye pointi 46 ikishinda mechi zake tisa zilizobaki itafikisha pointi 73. Azam yenye pointi 51 ikishinda mechi zake zote 7 itafikisha pointi 72

Lakini pia Yanga imerejea kile ilichokifanya misimu tisa iliyopita kwa kupata ushindi katika mechi mbili mfululizo za Ligi Kuu dhidi ya Simba ambapo mara ya mwisho ilifanya hivyo katika msimu wa 2015/2016 ilipokuwa inanolewa na kocha Hans Pluijm.

Mechi ya jana ilianza kwa timu hizo kushambuliana kwa zamu kuanzia dakika ya kwanza ya mchezo ingawa dakika ya nane, Yanga ilipata pigo baada ya beki wake Joyce Lomalisa kuumia na nafasi yake kuchukuliwa na Nickson Kibabage.

Dakika tatu baadaye, Simba ilipata pigo baada ya beki wa kati, Henock Inonga kuumia na nafasi yake kuchukuliwa na Hussein Kazi.

Ubao wa matokeo ulianza kubadilika katika dakika ya 20 kupitia kwa Stephane Aziz Ki kwa mkwaju wa penalti ambayo ilitolewa na refa Ahmed Arajiga baada ya beki Hussein Kazi kufanya faulo ndani ya eneo la hatari la timu yake.

Kazi alijikuta akifanya faulo hiyo baada ya kupoteza mpira ulionaswa na Aziz Ki ambaye alikimbia kwa haraka kuingia ndani ya eneo la hatari la Simba ndipo akafanyiwa faulo na beki huyo iliyozaa penalti hiyo.

Bao hilo lilidumu kwa dakika 18 tu kwani Joseph Guede aliipatia Yanga bao la pili katika dakika ya 38 ya mchezo akimalizia kwa ustadi pasi ya Khalid Aucho.

Guede alivunja mtego wa kuotea uliowekwa na walinzi wa Simba na kunasa pasi hiyo ya juu ya ukuta kutoka kwa Aucho na kisha kumpiga chenga kipa Ayoub Lakred na kuujaza mpira katika lango mtupu.

Hadi mwamuzi Arajiga anapuliza kipyenga cha kuashiria muda wa mapumziko, Yanga ilienda vyumbani ikiwa kifua mbele kwa mabao hayo mawili.


Simba ilikwama hapa

Kipindi cha kwanza Simba ilionekana kukwama kwenye kuhamisha mchezo baada ya kuunasa kutoka kwa Yanga ambapo Wekundu hao walikuwa hawaongezeki haraka mbele wakati timu yao inashambulia.

Simba ilipokuwa inashambulia ilikuwa na wachezaji watatu hadi wanne dhidi ya wale wa Yanga ambao walikuwa kati ya saba na wanane kwenye eneo lao, hali ambayo iliifanya Yanga kuwadhibiti wageni wao kirahisi.

Simba pia iliendeleza tatizo lake la msimu mzima la wachezaji wake kutomalizia vyema nafasi nyingi wanazopika.


Mzize bado

Yanga kama ingekuwa makini ingeweza kuondoka na mabao mengi kipindi cha kwanza, lakini mashambulizi yao mengi yalikwama kwa mshambuliaji wao, Clement Mzize ambaye alikosa utulivu wa kutoa pasi za mwisho kwenye eneo la hatari la Simba.


Mabosi vyumbani

Simba baada ya kwenda mapumziko vyumbani kila mchezaji alionekana kuwa na shauku ya kuzungumza hadi hapo nafasi ilipotolewa kwa nahodha Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ ambaye alizungumza kwa muda na baadaye kocha Abdelhak Benchikha alifuata.

Mwenyekiti wa Simba, Salum Abdallah ‘Try Again’ na wajumbe wengine watano walivamia chumba cha kupumzika wachezaji na kuonekana wakiwatuliza.

Wote sita wakiongozwa na Try Again walipata nafasi ya kuzungumza na baada ya hapo waliamuliwa kuondoka kupisha benchi la ufundi litoe neno kwa wachezaji kabla ya kipindi cha pili kuanza.

Baada ya viongozi hao kutoka, Kelvin Mavunga, mtathimini wa viwango wa klabu hiyo pia alipata nafasi ya kuzungumza kabla ya kocha kutoa neno la mwisho kwa wachezaji tayari kwa ajili ya kipindi cha pili.

Kipindi cha pili kilianza kwa Simba kufanya mabadiliko ya kuwatoa Fabrice Ngoma na Saido Ntibazonkiza na kuwaingiza Fredy Michael na Luis Miquissone katika dakika ya 58.

Dakika nane baadaye, Yanga ilifanya mabadiliko ya kuwatoa Yao Atohoula na Clement Mzize ambao nafasi zao zilichukuliwa na Kennedy Musonda na Bakari Mwamnyeto.

Mabadiliko hayo yalionekana kuiimarisha zaidi Simba ambayo ilichangamka na kuongeza kasi ya mashambulizi langoni mwa Yanga na juhudi zao zilizaa matunda katika dakika ya 74 pale ilipopata bao kupitia kwa Fredy Koublan.

Mshambuliaji huyo alinasa pasi iliyopigwa kiustadi na Clatous Chama na kuwapiga chenga mabeki wa Yanga, Ibrahim Bacca na Dickson Job na kuujaza mpira kimiani.

Baada ya kuingia kwa bao hilo, dakika moja baadaye, Simba ilifanya mabadiliko ya mwisho kwa kuwatoa Babacar Sarr na Kibu Denis ambao nafasi zao zilichukuliwa na Omar Jobe na Mzamiru Yassin na dakika ya 85, Yanga iliwatoa Mudathir Yahya na Maxi Nzengeli ambao nafasi zao zilichukuliwa na Augustine Okrah na Jonas Mkude.

Hata hivyo, mabadiliko hayo hayakuweza kubadili tena ubao wa matokeo na hadi refa Arajiga alipopuliza filimbi ya kumaliza mchezo, ilikuwani Yanga iliyoibuka mshindi wa mchezo huo.

Katika mechi hiyo, wachezaji Dickson Job, Mudathir Yahya, Joseph Guede, Babacar Sarr, Sadio Kanoute, Clatous Chama na Mzamiru Yassin walionyeshwa kadi za njano kutokana na makosa ya kucheza rafu.

Mastaa ukimataifa

Ni mechi iliyothibitisha thamani na ukubwa wa mechi hiyo na hilo linathibitishwa na vikosi vilivyoanza vya timu hizo ambavyo viliundwa na nyota 22 kutoka mataifa 11 tofauti.

Nyota hao 22 walioanza katika vikosi vya kwanza vya timu hizo wanatoka mataifa ya Tanzania, Mali, Senegal, DR Congo, Ivory Coast, Cameroon, Morocco, Zambia, Uganda, Burundi na Burkina Faso.

Watanzania walioanza ni Mohamed Hussein, Israel Mwenda na Kibu Denis kwa Simba wakati kwa Yanga walioanza walikuwa ni Dickson Job, Mudathir Yahya, Clement Mzize na Ibrahim Bacca.

Wageni walikuwa ni Henock Inonga, Maxi Nzengeli na Fabrice Ngoma (DR Congo), Yao Attohoula na Joseph Guede (Ivory Coast), Saido Ntibazonkiza (Burundi), Khalid Aucho (Uganda), Che Fondoh Malone (Cameroon), Djigui Diarra na Sadio Kanoute (Mali), Clatous Chama (Zambia), Babacar Sarr (Senegal), Ayoub Lakred (Morocco) na Stephane Aziz Ki (Burkina Faso).


Arajiga na rekodi

Mwamuzi Ahmed Arajiga aliyechezesha mechi hiyo aliendeleza rekodi yake ya kutokuwepo kwa matokeo ya sare katika mechi zote za watani wa jadi ambazo amewahi kuchezesha.

Kabla ya jana, mechi tatu za nyuma ambazo alishika kipenga baina ya timu hizo, zilimalizika kwa matokeo ya timu moja kupata ushindi na hakukuwepo na sare.

Refa huyo pia mechi zote tano za Yanga alizochezesha msimu huu, timu ya Wananchi imeshinda zikiwamo mbili dhidi ya Simba -- ya jana na ile ya 5-1. 


VIKOSI

KIKOSI YANGA

Djigui Diarra, Yao Attohoula, Joyce Lomalisa, Dickson Job, Ibrahim Hamad ‘Bacca’, Khalid Aucho, Maxi Nzengeli, Mudathir Yahya, Joseph Guede, Stephane Aziz Ki na Clement Mzize.

BENCHI: Aboutwalib Mshery, Kibwana Shomari, Nickson Kibabage, Bakari Mwamnyeto, Jonas Mkude, Salum Aboubakar ‘Sure Boy’, Farid Mussa, Augustine Okrah, Kennedy Musonda.


KIKOSI SIMBA

Ayoub Lakred, Israel Mwenda, Mohamed Hussein ‘Tshabala’, Henock Inonga, Che Malone Fondoh, Babacar Sarr, Fabrice Ngoma, Sadio Kanoute, Clatous Chama, Saidi Ntibazonkiza ‘Saido’ na Kibu Denis.

BENCHI: Ally Salim, David Kameta ‘Duchu’, Hussein Kazi, Mzamiru Yassin, Luis Miquissone, Ladaki Chasambi, Pa Omar Jobe na Freddy Michael.