Yanga yaitaka fainali CAF

Wakati mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara wakitarajiwa kuondoka leo kwenda Cairo, Misri kwa ajili ya mchezo wa marudiano dhidi ya Al Ahly wa hatua ya makundi, Ofisa habari wa Yanga, Ali Kamwe amesema inachotaka timu hiyo ni kufika fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kikosi cha Yanga leo kitaondoka saa 11:00 jioni, katika uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere na msafara huo umegawanyika katika makundi matatu.
Watasafiri wachezaji 24, benchi la ufundi watu 13 pamoja na viongozi 23 huku wakiongeza na viongozi wa TFF.
Yanga inaenda Misri kucheza mchezo wa marudiano dhidi ya Al Ahly, ambao mchezo wa kwanza zilitoka nao sare ya 1-1 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam.
Meneja Habari na Mawasiliano Yanga, Ali Kamwe amesema kikosi chao kinaondoka leo kikitumia Ndege ya Ethiopian Air na wanatarajia kufika Cairo kesho saa saba Usiku.
Kamwe amesema Yanga ambayo ilijiwekea malengo ya kufuzu hatua ya makundi ilikosubiri kwa miaka 25 kufikia hatua hiyo, ilitinga robo fainali baada ya kuichapa CR Belouizdad mabao 4-0 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, sasa wanachotaka ni kumchapa mwarabu kwao ili kuweka rekodi mpya na kutinga hatua ijayo wakiwa kileleni.
Amesema Al Ahly wajiandae kwani 'Bleech' inahamia Cairo na hakuna mchezaji aliyebadilisha nywele zake, huku akiwashukuru waandishi wa habari kwa kuongeza hamasa kwenye mchezo dhidi ya Belouizdad.
Amesema wanakwenda Cairo ili kuongoza kundi ili kuwa timu ya kwanza Tanzania kucheza na timu za nafasi ya pili.
“Si jambo jepesi kushinda kwenye ardhi ya Al Ahly, lakini uongozi unataka kuweka rekodi ya kuifunga kwao kama ilivyoseti na tutapambana kumaliza nafasi ya kwanza," alisema Ally na kuongeza mchezo huo utaonyeshwa kwenye runinga kubwa itakayofungwa kwenye viwanja vya Jangwani yaliko makao makuu ya klabu hiyo ili wanachama na wapenzi wa Yanga wajumuike pamoja kuona mchezo huo na kabla ya kuanza mchezo huo, wachezaji na viongozi walioko Cairo watazungumza mubashara na mashabiki walioko Jangwani.
Amesema hawajui watapangwa na nani kwenye mechi zijazo za robo fainali za nyumbani na ugenini lakini dhamira yao ni kupambana na kufika mwisho wa michuano hii.
"Hatuiogopi timu yoyote hata Mamelodi Sundown iletwe tu, maana hakuna tunayoihofia ila tunaiheshimu tu kwani wanaamini ubora wao."
Timu hizi mbili zilizoko kundi moja, kundi D katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika zimepishana poiti moja tu, huku Ahly akiwa na tisa na Yanga nane.