Yanga yafumua kikosi

Muktasari:

KUFANYA vizuri kwa Simba kwenye Ligi Kuu Bara na michuano ya kimataifa kumeizindua Yanga na mabosi wake, na sasa wameamua kuja na jambo moja tu ambalo linaweza kuacha vilio kwa wengine ndani ya kikosi cha sasa cha timu hiyo inayoongoza msimamo kwa tofauti ya alama mbili tu.

KUFANYA vizuri kwa Simba kwenye Ligi Kuu Bara na michuano ya kimataifa kumeizindua Yanga na mabosi wake, na sasa wameamua kuja na jambo moja tu ambalo linaweza kuacha vilio kwa wengine ndani ya kikosi cha sasa cha timu hiyo inayoongoza msimamo kwa tofauti ya alama mbili tu.

Hakuna siri kwa sasa kama kuna kundi lililokaliwa kooni Jangwani, basi ni wachezaji na wakati kesho wakitarajiwa kurudi uwanjani kuvaana na Biashara United taarifa mbaya kwa baadhi yao ni kwamba kuna panga kubwa linakuja mbele yao la kutaka kuundwa kwa kikosi bora cha msimu ujao.

Yanga inashuka Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam kesho kuikaribisha Biashara iliyokubali kulala nyumbani kwenye mchezo wao uliopita dhidi ya Coastal Union ya Tanga, huku nyota wake wakiwa na presha kubwa kutokana na matokeo mabaya kwa siku za karibuni.

Yanga inaongoza msimamo ikiwa na alama 51 baada ya mechi 24, ikifuatiwa na Simba iliyocheza mechi 21 ikiwa na pointi 49, huku Azam FC inayoshuka uwanjani leo ikiwa na pointi 47 na kutishia ufalme wa vijana wa Jangwani kama watapata matokeo mazuri wikiendi hii, huku Yanga ikiteleza.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi ya Yanga, Dominic Albinius ‘Baba Paroko’ amesema wanatambua kwamba kuanguka kwa timu yao kunatokana na changamoto ya ubora wa wachezaji walionao hivi sasa, hivyo wanataka kutembeza panga ili hata kama watapata nafasi ya uwakilishi wa nchi mwakani wasiaibike.

Albinius alisema wameshalijua tatizo hilo na sasa wanakwenda kufanya kazi ya kutulia na kuboresha idara zote za kikosi chao.

“Tulifanya usajili mkubwa, lakini sioni sababu ya watu kuanza kulaumu sana kwani usajili ni kama kamari na hili halitokei Yanga tu,” alisema Albinius.

“Tunaweza kujifunza hata kwa wenzetu klabu kama Real Madrid ilisajili mchezaji waliyeamini angeweza kuwapa kikubwa, Eden Hazard, lakini haikuwa hivyo. Hata hapa kwetu hili linaweza kutokea, nitoe mfano kwa kiwango ambacho alikionyesha mshambuliaji wetu Michael Sarpong kwa misimu miwili mfululizo pale Rwanda hakikuwa kitu ambacho unaweza kukibeza.”

Albinius aliongeza kwa kusema; “Tuliamini angekuja hapa na kuendeleza moto huo zaidi, lakini haikuwa hivyo, hakuna mchezaji tuliyemsajili kwa mikanda ya video kama watu wanavyodai, kila mchezaji tulimfanyia kazi katika kujiridhisha.”

Alisema usajili mpya utazingatia eneo la ushambuliaji, kiungo na ulinzi wa timu hiyo ambao umeonyesha changamoto kubwa.

Katika dirisha lililopita Yanga imewasajili Fiston Abdulrazack, Saido Ntibazonkiza, Tuisila Kisinda, Mukoko Tonombe, Farid Mussa, Yacouba Songne na Carhlinos ambao ni wenye rekodi nzuri katika timu walizotoka - baadhi wakicheza soka Ulaya, japo bado hawajaibeba timu hiyo mpaka sasa.

Aidha, Albinius alifichua siku sio nyingi watamtambulisha kocha wao mpya ambaye wamelazimika kumleta mapema ili asimamie usajili huo kutokana na uwezekano wa timu yao kucheza mashindano ya Afrika msimu ujao. “Tuna nafasi kubwa ya kucheza mashindano ya CAF msimu ujao, lakini hautaweza kushindana vyema ukiwa na ubora wa namna hii, lazima tuboreshe kikosi. Ndio maana siku chache zijazo tutamleta kocha mpya hapa, tumeshamaliza naye karibu kila kitu, imebaki hatua ya kuja hapa tu, anakuja kushirikiana na viongozi katika mchakato wa usajili,” alimalizia Albinius bila kumtaja kocha huyo, japokuwa Mwanaspoti linafahamu tayari Yanga imeshamalizana na Mfaransa Sebastian Migne.

Migne mwenye uzoefu mkubwa katika soka la Afrika akiwahi kuinoa timu ya taifa ya Kenya, anakuja kuchukua nafasi ya Cedric Kaze aliyefurushwa baada ya mfululizo wa matokeo yasiyoridhisha kwa mabingwa hao wa kihistoria wa Tanzania ambao wana misimu mitatu mfululizo hawajabeba taji la Ligi Kuu Bara.