Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Yanga yachanua Mapinduzi

Wachezaji wa Yanga wakishangilia moja ya mabao yao wakati wa mchezo wao wa ufunguzi wa michuano ya kombe la Mapinduzi dhidi ya mafunzo, uliochezwa jana jumapili kwenye uwanja wa Amaan, Zanzibar na Yanga kushinda mabao 3-0. Picha na Khatimu Naheka.

Muktasari:

Pambano hilo lililopigwa Uwanja wa Amaan, visiwani humu, lilishuhudia Mafunzo, mabingwa wa Ligi Kuu Zanzibar, wakizidiwa kila idara na Yanga iliyopata mabao mawili kipindi cha kwanza na jingine dakika za majeruhi.

MABINGWA wa Tanzania Bara, Yanga jana Jumapili ilianza vyema michuano ya Kombe la Mapinduzi kwa kuichapa Mafunzo ya Zanzibar mabao 3-0 katika mchezo wa ufunguzi.

Pambano hilo lililopigwa Uwanja wa Amaan, visiwani humu, lilishuhudia Mafunzo, mabingwa wa Ligi Kuu Zanzibar, wakizidiwa kila idara na Yanga iliyopata mabao mawili kipindi cha kwanza na jingine dakika za majeruhi.

Donald Ngoma alianza kuiandikia Yanga bao dakika ya 31 akimalizia krosi pasi kutoka kwa kiungo Thabani Kamusoko aliyewatoka walinzi wa Mafunzo na Mzimbabwe mwenzake huyo kutumbukiza kwa shuti la karibu.

Kabla ya hapo Yanga ilikosa mabao mengi ya wazi likiwamo la Amissi Tambwe aliyesalia na kipa na kupiga mpira uliotoka pembeni.

Wakati Mafunzo ikitafuta mbinu za kurejesha bao, dakika ya 34 ilishtukizwa kwa bao jingine lililofungwa na Ngoma aliyemaliza pasi ya kupenyezewa ya Kamusoko aliyefunika katika mchezo huo.

Kipindi cha pili, Mafunzo ilirudi kivingine kwa kuibana Yanga, huku ikifanya kosa kosa kadhaa hadi kupata penalti dakika ya 81 baada ya Juma Abdul kumchezea rafu Shaaban Seleiman, lakini mkwaju wa Heir Heir ulipanguliwa na kipa Deo Munishi.

Mabadiliko ya dakika za lala salama yaliyofanywa na Kocha Hans Pluijm yaliisaidia Yanga kuandika bao la tatu baada ya mtokea benchi, Paul Nonga kumalizia shuti la Geofrey Mwashiuya baada ya kutemwa na kipa wa Mafunzo dakika ya 90.

VIKOSI VILIVYOKUWA;

Yanga: Deo Munishi, Juma Abdul, Oscar Joshua, Pato Ngonyani, Kelvin Yondani, Mbuyu Twite, Simon Msuva, Thabani Kamusoko, Amissi Tambwe, Donald Ngoma na Deud Kaseke.

Mafunzo:Khalid Mahadh, Juma Mmnanga, Samih Nuhu, Said Shadan, Heir Heir, Hassan Juma, Abdul Hassan, Allu Hassan, Sadick Rajab, Mohammed Rahim na Ally Mmanga.

BOCCO AIOKOA AZAM

NAHODHA John Bocco ‘Adebayor’ ameendelea kuwa mhimili wa Azam baada ya usiku wa jana kufunga bao la kusawazisha lililoikoa timu hiyo kulala mbele ya Mtibwa Sugar katika mechi ya pili ya kundi B la michuano ya Kombe la Mapinduzi.

Bocco alifunga bao kwa mkwaju wa penalti baada ya kuangushwa baada ya kuguswa mpira wake wa kwanza akitokea benchi katika dakika ya 73 na kuipa timu yake sare ya bao 1-1 katika mchezo huo uliokuwa mkali uliochezwa kwenye Uwanja wa Amaan, huku ikishuhudiwa bao tamu la kichwa la Shiza Kichuya la dakika za lala salama likikataliwa na mshika kibendera kwa madai mfungaji alikuwa amezidi.

Hussein Javu alitangulia kuifungia Mtibwa bao dakika ya 60 baada ya David Mwantika kujichanganya na kuporwa mpira na Kichuya aliyetoa pasi kwa mfungaji huyo.