Yanga yaachana na Bigirimana, yaanza usajili wa CAF

YANGA imeachana na usajili wa kiungo nyota wa Kiyovu ya hapa Rwanda, Abeid Bigirimana, Mwanaspoti limeambiwa. Lakini usajili wa beki wa kushoto wa Uganda, Mustafa Kizza uko kwenye hatua nzuri.

Vinara hao wa Ligi Kuu Bara wiki chache zilizopita walimfungia safari Bigirimana (pichani) na kuja hapa kumuona laivu akicheza mechi za Ligi yao lakini wameamua kufanya uamuzi mgumu. Habari za uhakika kutoka ndani ya Kiyovu na Yanga ni kwamba klabu hizo zimeshindwa kuafikiana baada ya mazungumzo ya muda mrefu.

Habari zinasema kwamba staa huyo wa Burundi alikuwa na nia ya kwenda Yanga lakini mkataba wake wa mwaka mmoja ukatoa nafasi kwa klabu yake kupanda dau kubwa na ambalo walilishikilia msimamo.

“Huyu mchezaji gharama yake imekuwa kubwa sana mpaka viongozi wakasema wakienda Congo wanaweza kupata wachezaji zaidi ya mmoja kwa hiyo gharama,” alidokeza mmoja wa viongozi wa Yanga. Hapa Kigali kwenye dili hilo Yanga ilimtuma Kocha Msaidizi, Cedrick Kaze na Hersi Saidi Kiongozi wa kamati ya usajili.

Habari zinasema kwamba Kiyovu baada ya kuona Yanga wana uhitaji mkubwa kwa mchezaji huyo walishikilia msimamo wa kutaka zaidi ya Sh350 milioni za Tanzania ambazo Yanga hawakuwa tayari kutoa kwa mchezaji mmoja.

Yanga ambayo inataka kusuka kikosi chake mapema tayari kwa michuano ya kimataifa badae mwaka huu ilimtaka Bigirimana kama mbadala wa Sureboy ambaye anacheza staili ya ‘Box kwa box mwenye mapafu ya mbwa’

Kiufundi usajili wa Bigirimana ulimaanisha benchi la ufundi la timu hiyo lilitaka kuimarisha kiungo cha kati ambacho kwa sasa anacheza Khalid Aucho, Abubakar Salum ‘Sure Boy’, Zawadi Mauya na Yannick Bangala.