Yanga wana jambo lao, uongozi wataja sababu nzito

Sunday October 17 2021
yanga pic
By Thomas Ng'itu
By Clezencia Tryphone

YANGA wana jambo lao. Mashabiki wa Arusha watanuna lakini wale wa Dar es Salaam na mikoa ya jirani watafurahia.

Yanga wameamua kurejesha mechi yake na Azam Jijini Dar es Salaam tofauti na awali ilivyokuwa imepangwa kupigwa Arusha.

Mwanaspoti limebaini kwamba Yanga wamefikia uamuzi wa mechi hiyo ya Oktoba 30 irudishwe kwenye Uwanja wa Mkapa.

Mmoja wa viongozi wa Yanga ameliambia Mwanaspoti kwamba wameamua kurejesha mechi hiyo Dar es Salaam kimkakati kwavile ni moja ya turufu kubwa ya ubingwa wa Tanzania msimu huu. Habari za ndani ya uongozi zinasema kwamba, Yanga machale yamewacheza kwamba wakikomaa mechi hiyo ipigwe Arusha wataambulia majeruhi lakini wanaweza kukumbana na habati mbaya kwenye matokeo na wakaathirika kuelekea katika azma yao ya ubingwa.

Uongozi umejiridhisha kwamba uwanja Sheikh Abeid si salama kwa sasa kwa mastaa wake haswa kwenye eneo la kuchezea.

Mmoja wa viongozi wa Yanga aliliambia Mwanaspoti wameona waendelee kuutumia uwanja wa Benjamin Mkapa baada ya kuona hali ya uwanja wa Arusha sio nzuri ikiwa ni mwanzoni mwa Ligi na kama watalazimisha watapata pancha nyingi ambazo huenda zikawaathiri siku zijazo.

Advertisement

“Tumeona bora tucheze palepale kwa Mkapa kwa sababu tunaweza tukacheza Arusha lakini sasa wachezaji wetu wakapata majeraha, tulikuwa na lengo la kuwapa burudani pia mashabiki wetu wa kule pamoja na kuongeza mapato kwa mauzo ya jezi lakini sasa hakuna namna,” alidokeza mmoja wa viongozi wa Yanga.

Alipotafutwa ofisa habari wa Yanga, Hassan Bumbuli alikiri mchezo utarejeshwa katika Uwanja wa Mkapa lakini hakuwa tayari kufafanua sababu.

“Kweli mchezo utachezwa hapa hapa kwa Mkapa, siwezi kusema sababu ni nini ila we elewa hivyo,” alisema kwa kifupi Bumbuli huku kanuni zikiiruhusu timu kuchagua mchezo mmoja wa kuchezwa nje ya uwanja wake wa nyumbani kwa msimu husika.

Yanga kwasasa wanaendelea na mazoezi katika uwanja wao wa Avic Town kwa ajili ya mchezo wao dhidi ya KMC utakaopigwa Oktoba 19 katika uwanja wa Majimaji, Songea.

Baada ya mchezo huo Yanga watarejea tena jijini Dar es Salaam na kuendelea na mazoezi katika uwanja wao wa Avic Town wakijiandaa na mchezo dhidi ya Azam utakaopigwa saa 1:00 usiku katika uwanja wa Benjamin Mkapa.

WACHEZAJI WAFUNGUKA

Beki wa zamani Yanga, Bakari Malima alisema kitendo ambacho wamefanya viongozi wa Yanga ni kizuri kutokana na kuangalia zaidi afya za wachezaji wao.

“Jambo zuri kurejesha mchezo kwenye uwanja mzuri, kucheza katika uwanja ambao hauna afya nzuri kwa wachezaji sio jambo zuri kwa sababu unaweza ukasababisha wachezaji wapate majeraha,” alisema Malima.

Naye mshambuliaji wa zamani Yanga, Hery Morris alisema: “Viongozi watakuwa wameufatilia uwanja na kuona haupo vizuri, pale napafahamu vizuri na kipindi kama hichi cha kiangazi ndio utakuwa mgumu , mimi naufahamu sana bora ule wa Kirumba.”

Advertisement