Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Yanga wampa Mkwasa silaha za hatari

Muktasari:

Hata hivyo, taarifa ambazo Mwanaspoti limezinasa na kwa namna ilivyokifanyia tathimini kikosi cha Yanga, Mkwasa atahitaji kuweka nguvu zake kwenye maeneo matatu. Maeneo hayo ni kusajili mshambuliaji wa kati mmoja ama wawili wenye kujua kufunga kama ilivyokuwa kwa Heritier Makambo.

SIKU chache baada ya mabosi wa Yanga kumfuta kazi Kocha Mwinyi Zahera na benchi lake la ufundi, mchakato wa kuisuka upya umeanza kushika kasi.

Kikosi hicho kimewekwa chini ya uangalizi wa katibu mkuu na mchezaji wa zamani, Charles Boniface Mkwasa, ambapo kesho Jumatano atawasilisha rasmi ripoti yake kuhusiana na mambo anayotaka yafanyike.

Mkwasa ambaye taarifa za ndani ambazo Mwanaspoti linazo, atakuwa kocha msaidizi wakati mchakato wa kumpata kocha mkuu utakapokamilika, ataweka hadharani mapendekezo yake kwa namna alivyokiona na anavyotaka kikosi chake kiwe ili kuendeleza moto kwenye Ligi Kuu Bara.

Hata hivyo, taarifa ambazo Mwanaspoti limezinasa na kwa namna ilivyokifanyia tathimini kikosi cha Yanga, Mkwasa atahitaji kuweka nguvu zake kwenye maeneo matatu. Maeneo hayo ni kusajili mshambuliaji wa kati mmoja ama wawili wenye kujua kufunga kama ilivyokuwa kwa Heritier Makambo.

Pia, mawinga wawili-kulia na kushoto ambao ni halisia wenye kasi na uwezo wa kupiga krosi na pasi za mwisho kwa washambuliaji.

Wamo pia beki wa kushoto na kiungo mshambuliaji kwa ajili ya kuongeza uhai kwa nahodha Pappy Kabamba Tshishimbi, ambaye kwa sasa anaonekana kuelemewa na mzigo wa kuchezesha timu na wakati huo huo kukaba.

Ripoti ya Mkwasa inatua mezani kwa mabosi wa Yanga wakati dirisha dogo la usajili likitarajiwa kufunguliwa kuanzia Ijumaa ya Novemba 16 hadi Desemba 15, mwaka huu, ambapo imethibitika Yanga itaingia sokoni kufanya maboresho pamoja na kuwafungulia mlango baadhi ya nyota wake.

Mshambuliaji

Kwa misimu miwili iliyopita Yanga ilikuwa ikiwategemea Makambo na Amissi Tambwe kufanya kazi ya kupachika mabao nyavuni, lakini kwa sasa wote hawapo na wababe hao wa Jangwani wanapata tabu sana.

Licha ya kufanya usajili mkubwa kwenye dirisha lililopita ikiwanasa David Molinga (mwenye mabao mawili), Sadney Urikhob (bao moja) Yanga bado haionyeshi uhai kutokana na nyota hao kushindwa kuifanya vyema kazi hiyo.

Licha ya Molinga na Sadney kuchezeshwa mara kwa mara, lakini bado wameshindwa kuonyesha ubora hivyo kuanza kutiliwa shaka kama wanaweza kuvaa viatu vya Tambwe na Makambo.

Mawinga halisia

Unaweza kushangaa kwamba, mpaka sasa Yanga bado inawategemea Mrisho Ngassa kucheza winga ya kulia sambamba na Mapinduzi Balama, Deus Kaseke na Patrick Sibomana. Hata hivyo, bado uwanjani nyota hawa hawajawa na matokeo yanayorodhisha na hapo ndipo mahali ambapo, kwa mujibu wa habari za ndani, Mkwasa amepatolea macho akiajindaa kusaka mawinga wenye kazi na uwezo wa kuingiza mipira ndani. Balama, ambaye amesajiliwa Yanga akitokea Alliance FC amekuwa akionyesha ubora wa juu anaposimama kama kiungo mshambuliaji tofauti na anapopangwa kucheza kama winga.

Kwa Mnyarwanda Patrick Sibomana, ambaye mpaka sasa hajaonyesha uwezo mkubwa katika kutengeneza nafasi za mabao, japo amekuwa akifunga mabao muhimu kwa kutumia mipira aya adhabu.

Mpaka sasa ameshaifungia Yanga mabao matatu kwenye michuano ya Caf na Ligi Kuu Bara kwa kutumia mipira ya adhabu, lakini hakuna krosi wala assisti ya bao aliyopiga mpaka sasa.

Kiungo mshambuliaji

Nafasi ya kiungo mshambuliaji nalo bado imekuwa changamoto kubwa tangu kuondoka kwa Haruna Niyonzima na Ibrahim Ajibu Yanga, ambao wameacha rekodi tamu za kuzalisha mabao kwa washmbuliaji.

Kwa mambo yalivyo, Yanga ya sasa itahitaji kupata mtu sahihi katika kuongeza ubinifu wa kuzalisha pasi za mabao na kupandisha mashambulizi kwa kasi kwenda lango la timu pinzani.

Msikie Mayay

Mchambuzi wa soka Ally Mayay amekubaliana na hoja hizo za Mwanaspoti akisema Yanga bado haina mtu sahihi wa kumalizia nafasi ambazo Inatengeneza. “Ni kweli kabisa, kwa uhalisia mpaka sasa katika mechi ambazo Yanga imecheza hakuna yule ambaye ana uhakika kama atapata mipira miwili au.” mitatu anaweka mbili au moja. Hili ni eneo ambalo Inahitaji kutulia,” alisema Mayay.

“Tangu Tambwe aondoke ambaye anajua kazi yake ni kufunga tu au Makambo bado haIjapata mtu sahihi, Sadney sio mshambuliaji wa ubora huo wala Balinya (Juma) yule ni mshambuliaji wa nyuma ya mshambulaiji wa mwisho au ashambulie kutokea kushoto kama alivyokuwa anatumika katika klabu yake ya nyuma.

Mayay, ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Ufundi alisema pia Yanga inatakiwa kutafuta winga halisia, ambaye kwa staili ya soka soka lake atakuwa akitengeneza nafasi za mashambulizi mengi.

“Yanga haina winga mwenye makali, hii ni asili ya Yanga kuwa na mawinga wakali tangu enzi za kina Lunyamila (Edibily) hadi alipotokea Msuva (Simon), baada ya hapo haina mtu wa ubora huo itafute winga wa kulia.

“Pia itafute winga wa kushoto sioni kama Sibomana ni winga halisi labda iwe inamtumia kulingana na mfumo ili aweze kushambulia akitokea kati, lakini ninavyoona itafute mtu kama Singano (Ramadhan) au Kichuya (Shiza).

“Sijaona tatizo katika nafasi nyingine za ulinzi naona waliopo sasa wanatosha kuhimili kasi hiyo,” alisema.

Uongozi unasubiri ripoti ya Mkwasa

Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Fredirick Mwakalebela licha ya kuridhika na mwanzo mzuri wa Mkwasa, alisema wanasubiri ripoti yake ambayo itapatikana kesho Jumatano. Mwakalebela alisema kwa sasa kikosi chao kimewapa imani kwa kubadilika na kucheza soka la kutafuta ushindi na watahakikisha wanafanyia mapendekezo na mahitaji yote ya benchi la ufundi.

“Tumeona mabadiliko madogo ambayo kama uongozi yametupa imani kuwa tunaweza kufanya kitu, Yanga haikuwa na ubora wa kucheza namna ile zaidi ya kujilinda.

“Wakati tunaendelea na mchakato wa kutafuta kocha tunamsubiri Mkwasa ambaye kimsingi ndiye atakuja kumsaidia kocha mkuu atupe ripoti ya awali ya kipi tukifanyie kazi zaidi katika dirisha la usajili linalokuja.

MKWASSA HUYU HAPA

Kwa upande wake, Mkwasa amesema kwa muda aliokaa na timu amegundua Yanga ina kikosi kizuri na kuna upungufu mdogo ambao kama utafanyiwa kazi dirisha dogo la usajili basi watafanya makubwa.

Hata hivyo, alisema hawezi kuweka wazi upungufu huo hadi atakapokabidhi ripoti kwa uongozi ili ifanyiwe kazi huku akiweka wazi kuwa, anaendelea kukisoma kikosi na Jumapili anatarajia watakuwa na mchezo wa kirafiki dhidi ya Ruvu Shooting Uhuru.