Yanga wamebaki watano tu

Kikosi cha Yanga mwaka 2012
Muktasari:
Ukweli ni kwamba Mwombeki alipokuwa akishangilia bao hilo mashabiki waliendelea kuzimia, kazi ilikuwa nzito kwa watoa huduma ya kwanza kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
WAKATI straika wa zamani wa Simba, Betram Mwombeki anafunga bao la tatu la kusawazisha, Simba na Yanga zilipotoka sare ya mabao 3-3 Oktoba 20 mwaka jana, alikamilisha orodha ya mashabiki 20 waliopoteza fahamu kwenye mchezo huo.
Ukweli ni kwamba Mwombeki alipokuwa akishangilia bao hilo mashabiki waliendelea kuzimia, kazi ilikuwa nzito kwa watoa huduma ya kwanza kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Tukio hilo ni ishara kuwa mechi za Simba na Yanga ni mechi ambazo zina hamasa kubwa sana nchini. Ni mechi pekee zinazoweza kujaza sehemu kubwa ya Uwanja wa Taifa.
Tuachane na ya mwaka jana, Mei 2012 ulikuwa ni mwezi mchungu kwa mashabiki wa Yanga baada ya timu yao kushuhudia kipigo cha mabao 5-0 kutoka kwa watani wao Simba. Mashabiki wengi walilala njaa siku hiyo huku wengine wakishindwa kutekeleza majukumu yao mengine ya kifamilia, sababu ikiwa ni matokeo hayo.
Ni miaka miwili imepita sasa na maisha yamebadilika. Kikosi cha Simba kilichotoa kipigo hicho kimebakiwa na wachezaji wanne pekee. Hao ni beki Nassoro Masoud ‘Chollo’ na washambuliaji Uhuru Suleiman na Emmanuel Okwi. Jonas Mkude naye alicheza dakika chache kwenye mechi hiyo kwani alikuwa bado ni chipukizi.
Kikosi cha Yanga wamebaki wachezaji watano pekee. Mwanaspoti inakuletea orodha ya wachezaji wa Yanga waliocheza mchezo huo na mahali walipo kwa sasa;
Nsajigwa Shadrack
Kwenye kikosi hicho, Shadrack Nsajigwa alicheza beki ya kulia kabla ya kufanyiwa mabadiliko baadaye na kuingia Godfrey Taita. Nsajigwa alistaafu soka msimu uliofuata na sasa ni kocha msaidizi wa Yanga inayonolewa na Mbrazili Marcio Maximo.
Taita naye aliondolewa kwenye kikosi hicho msimu uliopita na sasa anaichezea Villa Squad ya Dar es Salaam inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza. Nsajigwa alipata wakati mgumu kumzuia Okwi na alisababisha moja kati ya penalti zilizoipa Simba mabao manne kipindi cha pili.
Oscar Joshua
Beki wa kushoto wa Yanga, Oscar Joshua naye alikuwemo kwenye kikosi cha Yanga kilichokumbana na kimbunga cha Simba mwaka huo. Joshua bado ana namba kwenye kikosi cha Yanga cha sasa kutokana na uwezo wake wa kukaba na kupandisha mashambulizi. Beki huyo anayesifika kwa nguvu za kukaba na kupandisha timu pia amekuwa akijumuhishwa kwenye kikosi cha Taifa Stars.
Nadir Haroub ‘Cannavaro’
Beki mkongwe zaidi Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ alisimama kama beki wa kati wa timu hiyo ambapo kasi ya washambuliaji wa Simba akiwemo Okwi ilionekana kumshinda. Cannavaro bado yumo kwenye kikosi cha kwanza cha Yanga mpaka sasa na amekuwa akijumuishwa pia kwenye kikosi cha Taifa Stars. Kwa sasa beki huyo amefanikiwa kutengeneza ukuta imara kwenye kikosi cha Yanga akishirikiana na beki mwenzake Kelvin Yondani ‘Vidic’ ambaye alikuwa Simba kwenye mechi hiyo.
Haruna Niyonzima,
Kiungo Mnyarwanda, Haruna Niyonzima wakati huo jina lake la utani la Fabregas likitamba aliishuhudia timu yake ikipigwa mabao 5-0 akiwemo kwenye kikosi cha kwanza. Alikuwa mmoja wa wachezaji walioumizwa na kipigo hicho na kila alipojaribu kuisaidia timu yake uwanjani mipango yote haikutimia.
Huo ulikuwa msimu wa kwanza wa Niyonzima kucheza Yanga baada ya kujiunga na kikosi hicho Julai 2011.
Kiungo huyo bado amekuwa na namba kwenye kikosi cha Yanga hadi hii leo na pia amekuwa akijumuishwa mara kwa mara akiwa nahodha wa kikosi cha timu ya Taifa ya Rwanda.
Hamisi Kiiza
Mshambuliaji wa Yanga, Hamis Kiiza raia wa Uganda naye alikuwemo kwenye kikosi hicho cha Yanga mwaka huo. Kiiza bado yupo kwenye kikosi cha Yanga lakini amekuwa hapati nafasi kwenye kikosi cha kwanza tangu kuwasili kwa Kocha mpya Marcio Maximo.
Awali kulikuwa na taarifa za kutemwa kwa mshambuliaji huyo kwenye usajili wa msimu huu lakini baadaye Yanga ililazimika kuachana na Emmanuel Okwi ambaye pia ni raia wa Uganda.
WENGINE
Yaw Berko/Said Mohamed,
Siku ya mechi hiyo golini alianza kipa Mghana, Yaw Berko ambaye baadaye alifanyiwa mabadiliko baada ya kuumia bega japokuwa habari zinasema alichungulia mechi na kuona kuna mvua ya mabao inakuja.
Yanga ilimtoa Berko wakati wa mapumziko akiwa amefungwa bao moja tu na kumwingiza kipa namba mbili, Said Mohamed lakini bado mabadiliko hayo hayakusaidia kwani mvua ya mabao iliendelea kwenye lango lao.
Makipa wote wawili walitemwa Yanga msimu uliofuata. Mohamed kwa sasa anaidakia Mtibwa Sugar wakati Berko yupo kwenye moja ya klabu za Ghana baada ya kutemwa na Simba aliyoichezea msimu uliopita.
Juma Seif ‘Kijiko’
Kiungo Juma Seif ‘Kijiko’ ndiye aliyecheza katikati akiwa kiungo mkabaji akiwasaidia mabeki wa kati waliopangwa siku hiyo ambao ni Athuman Idd ‘Chuji’ na Cannavaro. Sasa Kijiko hayupo Yanga, yupo Ruvu Shooting ya Pwani inayonolewa na Mkenya Tom Olaba.
Siku ya mchezo huo, Kijiko hakuweza kuhimili nafasi yake na kutoa mwanya mkubwa kwa viungo wa Simba wakiongozwa na marehemu Patrick Mafisango kufanya wanavyotaka na kupata ushindi wa mabao 5-0. Alijitahidi kupambana lakini hakuweza kuwa na mbinu za ziada mbele ya viungo wa Simba.
Athumani Iddi ‘Chuji’
Fundi, Athuman Idd ‘Chuji’ naye alikuwemo kwenye kikosi hicho cha Yanga kilichoshuhudia kipigo kutoka kwa Simba.
Chuji ambaye amewahi kucheza pia Simba alicheza kama beki wa kati akisaidiana na Cannavaro kwenye mechi hiyo na kuna wakati alituliza mashambulizi ya Simba lakini baadaye alizidiwa na mabao yakatiririka langoni kwao lakini sababu kubwa ilikuwa kumuachia Okwi aingie na mpira hadi katika eneo lao la hatari na kusababisha penalti. Chuji hakuweza kuwazuia viungo wa Simba ambao ni Mafisango, Mwinyi Kazimoto na Haruna Moshi ‘Boban’ walioonekana kuwa moto kwenye mchezo huo.
Chuji kwa sasa hayupo Yanga na siku kadhaa zilizopita alirejea nchini akitokea Oman alipokwenda kujaribu bahati ya kucheza soka la kulipwa. Sasa amejisajili Mwadui FC ya Shinyanga inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza.
Nurdin Bakari
Kiungo Nurdin Bakari naye alikuwa miongoni mwa wachezaji waliounda kikosi cha kwanza cha Yanga siku hiyo lakini hayumo tena kikosini hapo. Kiungo huyo aliondoka Yanga msimu uliofuata baada ya kusumbuliwa na majeraha ya goti yaliyosababisha kiwango chake kuanza kushuka. Bakari kwa sasa anaichezea Villa Squad ya Dar es Salaam inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza.
Davies Mwape/Kenneth Asamoah
Straika Mzambia, Davies Mwape alikuwemo kwenye kikosi cha Yanga kilichocheza mchezo huo kabla ya kufanyiwa mabadiliko na kuingia kwa Mghana, Kenneth Asamoah. Mwape alisajiliwa na Yanga kutoka klabu ya Konkola Blades ya Zambia. Asamoah alikuwa akiichezea Yanga kwa msimu wake wa kwanza. Mastraika hao wote wawili walitemwa kwenye kikosi hicho baada ya kumalizika kwa msimu.
Kwa kifupi wote wawili licha ya kuwa mashujaa katika baadhi ya mechi za watani, siku ya mchezo huo walionekana hawana jipya na hawakuweza kuisaidia timu hata kidogo na kusababisha minong’ono kwa mashabiki waliohoji kuhusu uwezo wao.
Rashid Gumbo
Kiungo mshambuliaji Rashid Gumbo alicheza pia kwenye mechi hiyo lakini baada ya kumalizika kwa msimu alitolewa kwa mkopo Mtibwa Sugar aliyoichezea kwa msimu mmoja. Gumbo alijiunga Yanga msimu huo akitokea Simba ambayo iliwaadabisha siku hiyo. Mshambuliaji huyo baada ya kumaliza mkataba wake na Yanga 2013 aliamua kwenda kucheza soka la kulipwa Shelisheli ambako yupo hadi sasa.
Kikosi cha Simba siku hiyo
Simba siku hiyo iliwakilishwa na Juma Kaseja, Nassor Masoud ‘Chollo’, Amir Maftah, Shomari Kapombe, Kelvin Yondan, Patrick Mafisango/Obadia Mungusa, Uhuru Suleiman, Mwinyi Kazimoto/Jonas Mkude, Felix Sunzu/Edward Christopher, Haruna Moshi ‘Boban’ na Emmanuel Okwi.