Yanga waivuruga Simba kitajiri

Muktasari:
HUWEZI kuamini, lakini ndivyo ilivyo. Wakati wa zoezi la usajili mabosi wa Simba na Yanga walituliza vichwa na kuamua kumwaga fedha ili kunasa wachezaji walioamini wangewasaidia katika Ligi Kuu Bara.
HUWEZI kuamini, lakini ndivyo ilivyo. Wakati wa zoezi la usajili mabosi wa Simba na Yanga walituliza vichwa na kuamua kumwaga fedha ili kunasa wachezaji walioamini wangewasaidia katika Ligi Kuu Bara.
Matajiri wa klabu hizo walipigana vikumbo, mmoja akiibukia Kusini, mwingine Kaskazini, ilikuwa pita huko nipite huku ili mambo yaende sawa na ghafla kipyenga cha ligi hiyo kikapulizwa Septemba 12 , 2015.
Kila timu iliibukia kutoka kwenye ‘chimbo’ lake lakini sasa kama hujui hadi juzi Jumapili, ilithibitika kuwa, mabosi wa Yanga walikuwa wajanja, walitumia fedha kunasa wakali wanaoibeba kwa sasa tofauti na Simba.
Jangwani inaonekana kuivuruga Simba, hata kama vijana wa Kocha Jackson Mayanja wapo kileleni wakiongoza msimamo wa ligi kwa tofauti ya pointi nne.
Nyota wa wanne pekee wa kikosi hicho cha Yanga ambao usajili wao uliigharimu klabu hiyo zaidi ya Sh 220 milioni wameitesa kweli Simba baada ya kufunga jumla ya mabao 43 ambayo ni sawa na mabao yaliyofungwa na kikosi kizima cha Simba. Mastraika Amissi Tambwe na Donald Ngoma, winga Saimon Msuva na kiungo Thabani Kamusoko ndio walioamua kuivuruga Simba. Nyota hao ambao kila mmoja amecheza mechi zaidi ya 19 msimu huu, huku Ngoma aliye mshambuliaji ghali zaidi katika kikosi cha Yanga akitua klabuni hapo kwa dau la Dola 50,000 (Sh 100 milioni kwa wakati huo) akitokea FC Platinum ya Zimbabwe, tayari ameifungia mabao 14 msimu huu. Anazidiwa ujanja na washambuliaji wawili tu ligi kuu; Hamis Kiiza wa Simba na Tambwe.
Tambwe ambaye mwaka jana alisaini mkataba mpya wa miaka miwili kuendelea kuichezea Yanga akichota Sh 40 milioni, tayari ameifungia timu hiyo mabao 18 msimu huu akishika nafasi ya pili ya wafungaji bora nyuma ya Kiiza aliyesajiliwa na Simba kma mchezaji huru kwa dau la Sh 35 milioni aliyefunga jumla ya mabao 19.
Nyota wengine wa Yanga walioivuruga Simba ni Ras Kamusoko aliyetua Yanga Dola 30,000 (Sh 60 milioni wakati huo) tayari ameifungia Yanga mabao matano.
Naye Msuva ambaye punde tu baada ya kufeli majaribio katika klabu ya Bidvest Wits ya Afrika Kusini mwaka jana, aliongeza mkataba wa kucheza Yanga kwa miaka miwili zaidi kwa dau la Sh 25 milioni, ameifungia mabao sita msimu huu. Ukichukua mabao yote ya nyota hao wanne utapata jumla ya mabao 43 ambayo ndiyo yaliyofungwa na kikosi kizima cha Simba, yakijumuisha mpaka mabeki wao Hassan Kessy, Mohammed Hussein Tshabalala na Juuko Murshid.
Katika msimamo wa ligi ulivyo Yanga imecheza mechi 22, mbili pungufu ya Simba ikiwa imefunga mabao 54, huku Azam iliyo nafasi ya tatu ina mabao 38 tu katika mechi 22.
Funika bovu
Katika hatua nyingine, mastraika watano wa Yanga wameonekana pia kuwatesa mastraika tisa wa Simba ambao takwimu zinaonyesha kuwa kwa ujumla wao wamefunga mabao 33 msimu huu, ikiwa ni wastani wa mabao 3.5 kwa kila straika idadi ambayo ni pungufu ukilinganisha na watano hao wa Yanga.
Mastraika watano wa Yanga, Ngoma, Tambwe, Matteo Antony, Malimi Busungu na Paul Nonga wamefunga mabao 35 msimu huu idadi ambayo imeipiku ya mabao 33 ya Simba iliyofungwa na mastraika tisa.
Simba msimu huu imekuwa na mastraika tisa; Kiiza, Mussa Mgosi, Hija Ugando, Ibrahim Ajib, Danny Lyanga, Joseph Kimwaga, Pape Nd’aw, Raphael Kiongera, Boniface Maganga.
Nd’aw aliachwa wakati wa usajili wa dirisha dogo akiwa hajafunga bao hata moja sambamba na Maganga aliyepelekwa kwa mkopo Mtibwa Sugar.
Mastraika wengine, Kiongera na Mgosi hawajaifungia timu hiyo bao lolote ligi kuu. Mabao ya Simba yaliyofungwa na mastraika yametokana na kazi ya Kiiza aliyefunga 19, Ajibu (9), Lyanga (3) na Ugando na Kimwaga wenye bao moja moja.
Kwa upande wa Yanga Tambwe amefunga mara 18, Ngoma 14, Busungu mara mbili, Matteo akifunga bao moja huku Nonga akiwa hajafunga bao lolote ligi kuu tangu atue Yanga mwishoni mwa mwaka jana.