Yanga, Simba zapewa mchongo kufuzu nusu fainali CAF

WAZIRI wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Damas Ndumbaro amesema Serikali itakutana na Shirikisho la Soka nchini na klabu za Simba na Yanga ili kuona inatoa mchango gani kuhakikisha timu hizo zinafanya vizuri robo fainali na kusonga mbele.

Waziri Ndumbaro amesema hayo leo Machi 13, 2024 wakati akichangia mjadala wa Mwananchi Space, uliandaliwa na Mwananchi Communications Ltd, wenye mada isemayo 'Ipi nafasi ya Simba, Yanga kwenye vita ya kusaka nusu fainali Ligi ya Mabingwa Afrika.

Ndumbaro amesema pamoja na mambo mengine, amewataka mashabiki kuacha kuwapokea mashabiki na wafahamu mechi hizi za robo fainali ni kufa na kupona na kinachotakiwa ni kuhakikisha timu zetu zinashinda.

Amesema Serikali itakula sahani moja na mashabiki wa Simba na Yanga ambao wataenda kupokea wageni uwanja wa ndege na kuwasapoti.

"Wiki iliyopita tulitoa tamko, Serikali tunataka kukaa na Simba, Yanga na TFF, ili watuambie kama serikali, tunahitaji kutoa mchango gani ili timu kushinda robo fainali na ziingie nusu fainali. Tunaweza kukutana Jumanne wiki ijayo ili kupanga mikakati."

Kuhusu mashabiki amesema; "Watanzania niwaombe sana najua kuna utani wa jadi, lakini kwenye mechi hizi za robo fainali ni mechi za kufa na kupona, hatutegemei kuona Mtanzania yeyote akienda kupokea wageni uwanja wa ndege, ama kuvaa jezi za timu za wageni."

"Kwa hiyo wewe Mtanzania ambaye utaweka kimbelembele kwenda kupokea wageni uwanjani wa ndege, kuwasapoti kwa namna yeyote, hatutakuelewa na tutadili na wewe kwa vile ambavyo tunaona inafaa."

"Tumekuwa nchi pekee iliyofanikiwa kuingiza timu mbili mwaka huu, lakini ukishapata mafanikio haupaswi kutumia muda mwingi sana kushangilia hayo mafanikio, unatakiwa uangalie unafanya nini ili kuendelea kupata mafanikio zaidi."

Ushirikiano utasaidia

Makamu wa rais wa Yanga, Arafat Haji ameunga mkono kauli ya Waziri Ndumbaro kuhusu mashabiki wa Simba na Yanga kuacha kushabikia wageni na kutaka ushirikiano ili kuzisaidia kufuzu, huku akimshukuru kwa kukemea ushabiki huo usiofaa kwenye jambo la kitaifa.

"Msimu uliopita tukiwa uwanja Algeria zilikuwa zinapigwa fataki nyingi sana, unajiuliza zimeingiaje, lakini ukiangalia pembeni unaona askari wanawapa mashabiki wapige zaidi ingawa hilo siyo zuri sana kwa usalama," amesema na kuongeza;

"Hivyo tunapaswa kujifunza kushirikiana, kwenye jambo la kitaifa kuangalia masilahi mapana ya taifa letu, mashabiki  wabadilike, tuachane na chuki, nilishangaa baada ya kuona kipande cha video kikionyesha baadhi ya watu wakishangilia Yanga kupangwa na Mamelodi Sundowns, sasa tuzingatie kauli ya waziri Ndumbaro.

"Pia niwashukuru Mwananchi kuwa sehemu ya hamasa ya timu zetu, kujiandaa na niwaombe mwendelee na mnachokifanya inasaidia kuendeleza maendeleo ya soka nchini."

Pia Arafat amesema kuwa na mipango itasaidia iwe ni ya muda mfupi au mrefu; "Uwezekano wa kufika mbali upo na ni mkubwa sana lakini huwezi kufika hapo bila yakuwa na mipango ya muda mfupi na mrefu."

"Berkane na Algers hizi ni timu ambazo zilikuwa na mipango ambayo inabadilika kulingana na hatua.

Hivi ndivyo sisi Yanga tunavyokwenda, tulikuwa na mipango ya awali ya kufika hatua ya makundi, hiyo ilikuwa ni mpango wa muda mfupi lakini tumefanikiwa kufuzu na sasa tupo robo.

"Wenzetu huwa na umoja sana linapokuja suala la timu zao kwenye michuano ya kimataifa, kwa mfano wale waliobahatika kwenda na Yanga kwenye mchezo wa fainali waliona ni jinsi gani wenzetu walivyokuwa, natamani kuona timu za Tanzania zikicheza fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika."

"Nafikiri pia jambo muhimu kwa timu zetu ni suala la saikolojia, ukiangalia timu ambazo tumepangwa nazo zimekuwa bora Afrika, Mamelodi na Al Ahly zilizobeba taji la michuano hii. Simba pia haina takwimu mbaya mbele ya Al Ahly."

Zina nafasi ya kufuzu
Wakizungumza kwa nyakati tofauti kwenye mjadala huo, wadau mbalimbali wa michezo wametoa maoni yao huku wakizipa nafasi timu hizi kutokana na ubora wao kwa miaka ya karibuni na hata miamba hiyo ya soka na nyingine zinaziogopa timu hizo.

Meneja Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Yanga, Ally Kamwe amesema nafasi ya kutinga nusu fainali ipo wazi, kwani klabu yao imejadiliwa ndani na nje kama timu tishio inayoweza ikaisapraizi Mamelodi Sundowns.

"Kauli iliyosemwa na viongozi wa Yanga inaonyesha wanaheshimu wapinzani, lakini niwaambie ndugu zangu kuwaleta wachezaji kama Stephane Aziz Ki, Max Nzengeli, Djigui Diarra, Pacome Zouzoua na wengine wengi, hawakuja kushinda mechi dhidi ya Ihefu pekee," amesema na kuongeza;

"Labda niwaachie swali, mkiangalia kikosi cha Yanga kuna wachezaji wangapi ambao wanaweza wakaingia kwenye kikosi cha Mamelodi Sundowns, mkipata jibu basi mtajua Yanga itakuwa na mchezo gani dhidi yao."

Mwandishi wa habari kutoka Afrika ya Kusini, Dube Mthoko amesema Kocha wa Mamelodi Sundowns, Rhulani Mokwena Hloae anaiogopa Yanga kuelekea mchezo wao wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika utakaopigwa kati ya Machi 29-30.

"Yanga ni timu kubwa, nilipata bahati ya kuzungumza na kocha Mokwena jioni hii akanambia anaiogopa Yanga, akanambia anaifahamu Yanga vizuri, anafahamu ubora wa Kocha Miguel Gamondi na ameangalia baadhi ya mechi."

"Lakini bado Mamelodi ni moja ya timu bora sana, wamewekeza sana kupitia mmiliki wao Patrice Motsepe, wanaonekana kudhamiria kutaka kushinda taji lao la pili la Ligi ya Mabingwa."

"Kawaida ukiwa unacheza na Mamelodi halafu ukawa unataka kumiliki mpira muda mwingi, utakuwa kwenye hatari sana ya kupoteza mechi."

Mwandishi wa Mwananchi, Charles Abel amefafanua nafasi za timu hizo hatua ya robo fainali na amesema ili zifuzu nusu fainali zinatakiwa zijipange hasa kiufundi.

"Nina matumaini na timu za Tanzania, zamani timu zetu zilikuwa zinaangushwa na vitu nje ya uwanja, ila kwa sasa vitu vingi vinaamuliwa uwanjani, hivyo Simba na Yanga zijipange zaidi kiufundi, zinaweza zikasogea katika hatua inayofuata.

"Kocha wa Yanga, Ángel Gamondi analijua soka la Afrika na wachezaji wazuri, vivyo hivyo kwa kocha wa Simba, Abdelhak Benchikha kachukua ubingwa akiwa na  AS Alger na ubingwa wa Super Cup, hivyo Simba na Yanga zina makocha bora wanaoweza wakaziongoza timu vyema."

Mwandishi wa Habari na mchambuzi wa michezo, ameongezea kuhusu mipango ya timu akiitolea mfano Mamelodi ambayo mipango yake ya muda mrefu imeipa mafanikio na sasa ni tishio Afrika ingawa kwenye mchezo na Yanga haoni kama imepishana sana na Yanga.

Amesema hata kwa Simba ina nafasi kwani msimu huu Al Ahly haijawa na kiwango kizuri na imekuwa ikiruhusu wapinzani kufika langoni kwao.

"Simba ina nafasi ya kufanya vizuri, kwani mpinzani wake Al Ahly anafanya makosa na inaruhusu mpinzani kufika golini kwao, hivyo timu zote mbili zijipange zina nafasi ya kutinga hatua nyingine," amesema na kuongeza;

"Ikumbukwe msimu wa 2014/15 Mamelodi Sundowns FC ilipata ubingwa chini ya Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi, hivyo ana uwezo wa kufanya makubwa, akiwa na Wanajangwani."

Mwanachama wa Yanga, Ndembo Jafar amesema, "Mamelodi ina uwekezaji mkubwa lakini sisi tuna nafasi ya kupita ikiwa tutatumia vizuri uwanja wetu wa nyumbani."

"Mimi naamini kocha wetu Miguel Gamondi amekuwa akitupa matokeo mazuri anaifahamu Mamelodi vizuri na anafahamu wachezaji wake na anajua nani anafaa kucheza kwa muda gani, kwa hiyo naamini timu yetu inaweza kupita na naona mchezo tutaumalizia hapa hapa nyumbani na kujipa uhakika wa kuingia nafasi nyingine."

Kocha wa Dodoma Jiji, Francis Baraza amesema Simba na Yanga, zina nafasi kubwa za kutinga nusu fainali Ligi ya Mabingwa Afrika, zijipange.

"Nimecheza na Simba na Yanga kwa mechi za Ligi Kuu, pia nimefuatilia timu zao pinzani, kwa maana ya Mamelodi Sundowns na Al Ahly, zinafungika ni makocha kufanyia marekebisho kwenye vikosi vyao," amesema na kuongeza;

"Yanga ina kikosi kizuri, hivyo ina uwezo wa kupambana na hao Mamelodi Sundowns, lakini vile vile Simba imecheza mara nyingi na Al Ahly, ikicheza nyumba wafunge mabao dakika za mwanzo angalau mawili na kuendelea, naiona hatua ya kutinga nusu fainali."
 
Jambo lingine alilolizungumzia Baraza ameliomba Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kushirikiana na klabu hizo ili ziweze kufanikiwa kupata ushindi nyumbani.

"TFF ni muhimu kuziunga mkono klabu hizo, ili ziweze kufanya vizuri, zinapocheza uwanja wa nyumbani na hilo linawezekana," amesema.

Mchambuzi wa Soka, Farhan Kihamu amesema Simba na Yanga zitazame namna ya kucheza mechi zao za robo fainali katika muda ambao wapinzani wao hawajazoea ili kuongeza uwezekano wa kufuzu hatua ya nusu fainali.

"Awali changamoto kubwa ilikuwa ni ubora wa wachezaji na ugeni wa michuano kwa sababu mara zote tulikuwa tunatoka kwenye hatua za awali, mwaka 2019 wakati Simba inakutana na Al Ahly katika kipindi ambacho Simba ndio ina uwekezaji mpya, ilifungwa mabao matano kule Cairo, hapa Dar es Salaam Ahly ikafungwa moja, mwaka 2021, Simba ilifungwa moja ugenini Cairo, Al Ahly ikafungwa moja hapa Tanzania na mechi za mwisho kwenye African Football League, hivyo ukiangalia kila siku ule utofauti unapungua."

"Ni kweli Al Ahly na Mamelod ni timu kubwa, lakini kwenye michuano hii katika hatua za mtoano unakuwa unacheza kwa malengo na sio kucheza ilimradi kucheza, kwangu nikiwatazama Simba wanapoenda kucheza na Ahly, inahitaji ushindi kwa sababu tayari imeshapunguza ule utofauti kutokana na matokeo."