Yanga, Simba kutangulia dabi nyingine tano duniani wikiendi hii

Muktasari:

  • Simba na Yanga zinakutana katika mchezo wa duru la pili wa ligi baada ya ule wa kwanza kumalizika kwa Simba kuchapwa mabao 5-1.

Wikiendi hii kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam kutakuwa na Dabi ya Kariakoo, ikiwa ni dabi ya tano Afrika kwa ukubwa, macho na masikio ya kundi kubwa la mashabiki wapenda soka yatakuwa hapo.

Simba na Yanga zinakutana katika mchezo wa duru la pili wa ligi baada ya ule wa kwanza kumalizika kwa Simba kuchapwa mabao 5-1.

Pambano hilo linalokuwa la 112 kwa timu hizo za Kariakoo kukutana tangu kuasisiwa kwa Ligi ya Bara mwaka 1965 limeshikilia nyoyo za mashabiki wengi kutokana na kuwa ni pambano la Watani wa Jadi wa soka nchini.

Upinzani wa timu hizo umetokana na asili ya kuasisiwa kwao, kwani Simba imezaliwa kutoka mgongoni mwa Yanga mwaka 1936, mwaka mmoja tangu kuanzishwa kwa Yanga na ushindi wa mchezo wa leo kwa kila utaziweka katika nafasi nzuri ya mbio za ubingwa.

Ushindi kwa Yanga utazidi kuiweka katika mazingira mazuri ya kuusogelea zaidi ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu, huku kwa Simba itarejesha matumaini ya kupambana kwenye mbio hizo zinazoihusu pia Azam FC.

Lakini wakati watu wakisubiria kwa hamu kutazama mechi hii, sehemu nyingine duniani pia kutakuwa na dabi kali.

Hapa tumekuorodheshea baadhi ya dabi hizo zinazopigwa wikiendi hii.

NKANA v POWER DYNAMOS

Hii dabi nyingine kali inayopigwa leo Jumamosi, jijini Kitwe ikiwakutanisha wababe hao wa Zambia, huku wenyeji wakiwa na rekodi tamu ya kushinda michezo minne mfululizo kati ya mitano ya Ligi Kuu tangu 2021.

Dabi hii ni moja ya dabi kali katika Ukanda wa Kusini mwa Afrika, ukiachia ile ya Soweto Dabi ya Kaizer Chiefs na Orlando Pirates.

Mechi hii itapigwa saa 2:00 usiku mara baada ya kumalizika kwa Kariakoo Dabi na Wazambia watakuwa bize kutaka kuona Nkana iliyopo nafasi ya 11 katika msimamo itaendelea kuburuza na wapinzani wao hao wanashika nafasi ya tatu.

MASHEMEJI DABI

Hapo kwa majirani zetu wa Kenya, kutapigwa Dabi ya Mashemeji itakayozikutanisha Gor Mahia na AFC Leopards.

Wakenya wanapenda kuiita Mashemeji dabi kutokana na upinzani wa soka la nchi hiyo linalopigwa Jumapili ya wiki hii kuanzia saa 9:00 mchana kwenye Uwanja wa Nyayo, jijini Nairobi Kenya.

Gor maarufu K’Ogalo inaingia katika mchezo huu ikiwa ndio kinara wa Ligi Kuu Kenya kwa pointi zao 54, huku Leopards inayofahamika kama Ingwe ikiwa katika hali mbaya ikishika nafasi ya nane na pointi zao 38.

Mchezo wa duru la kwanza Gor Mahia iliibuka na ushindi wa mabao 2-1.

EL CLASICO

Huko Hispania, Barcelona itakuwa ugenini kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu kuvaana na wapinzani wa jadi, Real Madrid.

Mchezo wa kwanza baina ya timu hizi ulimalizika kwa  Madrid kushinda mabao 2-1 na mechi hii ya marudiano inaonekana kuwa na presha kubwa kwa Barca kwani ikipoteza itakuwa inajiweka katika mazingira magumu ya kumaliza kwenye nafasi nne za juu.

Kwa sasa Barca inashika nafasi yapili ikiwa na pointi 70, na Madrid ina pointi 78, hivyo kama Madrid ikipoteza Barca itakuwa imefufua matumaini ya ubingwa wakati huu ambapo ligi imebakisha mechi saba kabla ya kumalizika. Mchezo huu unatarajiwa kupigwa Jumapili  hii kuanzia saa 4:00 usiku.

Bahati mbaya El Clasico hii imekuja wakati Real Madrid ikiwa imetoka kufuzu nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, huku wapinzani wao waking’olewa na PSG ya Ufaransa. Madrid iliitoa Manchester City kwa penalti baada ya pambano hilo kuchezwa kwa muda wa dakika 120 na kumalizika kwa sare ya 1-1 na kufanya matokeo ya mwisho kuwa mabao 4-4.

CRYSTAL PALACE VS WEST HAM

Pale jijini London, vijana wa kutoka mitaa ya Selhurst watakuwa nyumbani wakiwaalika West Ham na kocha wao David Moyes kutoka mitaa ya Stratford ndani ya Jiji hilo.

Palace iliyopo nafasi ya 14 inapambana kuhakikisha inabaki Ligi Kuu England kwa msimu ujao kwani licha ya nafasi iliyopo hawana uhakika wa asilimia mia kwamba watabaki.

Kwa sasa wana alama 33 na tofauti yao na Luton iliyopo nafasi ya 18 ni alama nane ambazo zinaweza kufutika ndani ya mechi tatu tu kati ya tano zilizosalia.

West Ham ambayo ipo hatua ya robo fainali ya Europa League mchezo huu kwao pia ni muhimu kwani wanapambana kuhakikisha wanafuzu michuano ya Ulaya kwa msimu ujao.

BOCA JUNIORS VS RIVER PLATE

Ni tafsiri halisi ya dabi. Inahitaji kuwa na moyo wa chuma ukiwa mchezaji ama hata shabiki kukanyaga uwanjani wakati timu hizi mbili zinacheza, lakini mashabiki wa soka wa Argentina wenyewe wameshazoea.

Polisi, moshi na kila aina ya matukio yenye kuashiria vurugu , huwa yanatokea katika mechi hii.

Mwaka 2018, mechi yao ilighairishwa baada ya kuibuka kwa vurugu ndani na nje ya uwanja polisi walitumia nguvu ya ziada kuhakikisha wanalinda wachezaji na kutuliza ghasia.

Ni mara chache sana mechi hii kumalizika kwa usalama, tena hususani inapochezwa nyakati za usiku.

Timu hizi zinakutana kwa mara yapili ndani ya mwaka huu katika Ligi Kuu Argentina na mechi yakwanza ilimalizika kwa sare ya bao 1-1. Mechi hii itapigwa kesho kuanzia saa 3:30 usiku.