Yanga: Simba jidanganyeni tu

Sunday May 16 2021
yanga pic
By Khatimu Naheka

YANGA wapo kimya wakisikilizia uamuzi ya Serikali na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) juu ya lini litarudiwa pambano baina yao na watani wao Simba, lakini hapohapo wakashusha ujumbe mzito kwenda kwa Wekundu hao.

Yanga imesema wala hawajawakimbia Simba na kwamba, walichotaka kuonyesha ni kutamani kuona kanuni za soka zinafuatwa na kama watu hawaamini ipo siku watakutana na Wekundu hao.

Kauli hiyo imetolewa na Mshauri wa uongozi wa Yanga, Senzo Mazingisa ambaye ameliambia Mwanaspoti kwamba haikuwa sawa kwao kucheza mchezo huo na baadaye wakafuata uamuzi wa uongozi mkuu wa klabu kusimama katika muda wa awali.

Alisema Yanga ina kikosi cha kushindana na Simba wakati wowote na wakapata matokeo mazuri kwa kuwa wanajua ubora halisi wa Simba na jinsi ya kupambana nao.

Senzo ambaye aliwahi kufanya kazi Simba kabla ya kutua Yanga, alisema siku watakayokutana na Simba kukiwa na mazingira mazuri ya kanuni kufuatwa watapambana.

“Yanga haiwezi kuikimbia Simba, hilo haliwezekani, ila katika soka ni muhimu kanuni zikafuatwa, hiki ndicho uongozi wa juu wa klabu uliamua kusimamia,” alisema Senzo.

Advertisement

“Yanga ilikuja uwanjani na ikawasubiri Simba, hiyo sio timu ambayo imemkimbia mwenzake, kukimbia tusingekuja, najua hii mechi itakuja kurudiwa au kukutrana katika mashindano yoyote.

“Tuna kikosi ambacho kinaweza kupambana na Simba na tukapata matokeo mazuri, tumefanya hivyo mara mbili msimu huu, tuliwakosa mchezo wa kwanza pia watu wasisahau tumeshinda mbele ya Simba msimu huu.”

Alisema kwa sasa wanaendelea kuona matunda ya mabadiliko ya benchi la ufundi ambapo mabadiliko ya ubora yanaendelea kuchomoza katika kikosi chao.

Advertisement