Yanga raha sana

Muktasari:
KAMA kila kitu kitakwenda sawa, huenda Yanga wakapiga miruzi ya kitajiri sana msimu ujao kutokana na miamala itakayoingia kwenye akaunti za klabu na kufanya maisha yao ya furaha zaidi.
KAMA kila kitu kitakwenda sawa, huenda Yanga wakapiga miruzi ya kitajiri sana msimu ujao kutokana na miamala itakayoingia kwenye akaunti za klabu na kufanya maisha yao ya furaha zaidi.
Habari ya mjini kwa sasa ni mkataba wenye thamani ya jumla ya Sh 41 bilioni ambao Yanga imesaini juzi na Kampuni ya Azam Media wa haki za maudhui ambao utaanza kufanya kazi rasmi msimu ujao.
Kwa kuanzia Yanga itaingiza kiasi cha Sh 2.4 bilioni kwa msimu wa 2021/2022 ambacho itakuwa ikilipwa kila mwezi kiasi cha Sh200 milioni, fedha ambayo itakuwa inaongezeka kila msimu.
Tathmini iliyofanywa na Mwanaspoti mara baada ya Yanga kusaini mkataba huo, imebaini kuwa timu hiyo kwa msimu ujao tu inaweza kuvuna kitita kikubwa cha fedha kinachoweza kuvuka zaidi ya Sh11 bilioni ambazo zitaifanya iwe na jeuri katika usajili kwa kuvuta mastaa wa bei mbaya na kulipa mishahara yao.
Pia itajenga miundombinu ya kisasa pamoja na kuzisimamia na kuziendesha vyema timu zote ambazo ziko chini ya klabu hiyo kuanzia ile ya wakubwa hadi za vijana na ya wanawake.
Kiasi hicho cha fedha ambacho Yanga inaweza kukusanya msimu ujao, kitatokana na fungu watakalovuna kwenye udhamini, mauzo ya bidhaa za klabu hiyo pamoja na makusanyo kutoka kwa Wanachama.
SH8.2 BILIONI ZA UDHAMINI
Fungu kubwa la fedha kati ya hizo Sh 11 bilioni ambazo huenda Yanga ikakusanya, linatokana na mikataba mbalimbali ya udhamini ambayo klabu hiyo imeingia.
Kati ya Sh11 bilioni, kiasi kikubwa cha fedha kinatokana na udhamini ambacho kitakuwa ni takribani Sh8.2 bilioni sawa na asilimia 74.55 ya fungu zima la fedha ambalo klabu hiyo inaweza kuingiza.
Yanga itavuna fedha nyingi zaidi kutoka kampuni ya Azam Media ambazo ni takribani Sh 6.4 bilioni.
Katika fedha hizo kutoka Azam Media, Sh 2.4 bilioni zitatokana na mkataba ambao umesainiwa juzi lakini pia itapata kiasi cha Sh3 bilioni kutoka kampuni hiyo kama itatwaa ubingwa wa Ligi Kuu au kumaliza katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi.
Kuna Sh500 milioni ambazo Yanga itapata kutoka Azam Media kwenye fungu la udhamini wa haki za matangazo ya Ligi Kuu lakini kama itatwaa ubingwa, itapata bonasi ya Sh 500 milioni kama mkataba wa udhamini wa urushaji wa matangazo ya Ligi Kuu msimu ujao baina ya Azam Media na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) unavyoelekeza.
Ukiondoa fedha hizo, Yanga pia itapata kiasi cha Sh1 bilioni kutoka kampuni ya ubashiri wa matokeo ya michezo ya Sportpesa ikiwa ni utekelezaji wa mkataba baina yao utakaofikia ukingoni mwakani.
Kuna kiasi cha zaidi ya Sh400 milioni ambacho Yanga itapata kutokana na mikataba miwili ya udhamini kutoka Kampuni ya GSM ambapo wa kwanza ni ule wa mauzo ya jezi ambapo inapata mrabaha wa Sh1,300 kwa kila jezi moja inayouzwa na fedha nyingine itapata kupitia mkataba na kampuni ya uuzaji wa magodoro ya GSM Foam.
Fedha nyingine ambazo Yanga itapata ni Sh300 milioni kutoka kampuni ya Taifa Gas lakini pia itavuna kiasi cha Sh100 milioni kutoka Kampuni ya Watercom ikiwa ni fungu la udhamini wa matangazo ya maji ya Afya.
WANACHAMA, MASHABIKI SH2.9 BILIONI
Ikiwa mambo yataenda kama yalivyopangwa, wanachama na mashabiki wa Yanga watachangia kiasi cha zaidi ya Sh 2.9 bilioni kama mchanganuo wa bajeti ya klabu hiyo kwa msimu ujao unavyoainisha.
Katika bajeti hiyo iliyopitishwa kwenye mkutano mkuu wa Yanga uliofanyika Juni 27, klabu hiyo imepanga kuvuna kiasi cha Sh2.04 bilioni kutokana na ada za wanachama kwa mwaka lakini pia imepanga kukusanya kiasi cha Sh350 milioni kupitia mauzo ya bidhaa mbalimbali zenye chapa ya klabu hiyo.
Yanga pia imepanga kukusanya jumla ya Sh 565 milioni kutokana na mapato ya milangoni katika mechi zake za mashindano mbalimbali msimu ujao.
CHENJI YA Sh3 BILIONI
Kiujumla kama mambo yataiendea vyema Yanga, itaweza kubaki na chenji ya Sh 3 bilioni kiasi ambacho kitabakia baada ya matumizi ya fedha hizo zote ambazo inaweza kukusanya msimu ujao.
Kwa mujibu wa bajeti ya klabu hiyo, Yanga imepanga kuwa na matumizi ya jumla ya Sh 8 bilioni kwa msimu ujao hivyo kama wakiingiza kiasi hicho cha Sh11 bilioni, watabakia na kiasi cha Sh 3.1 bilioni baada ya matumizi yao yote.
USAJILI, UENDESHAJI BIL 8
Katika mkutano huo mkuu uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa DYCC, Dar es Salaam hivikaribuni, Yanga ilitangaza na kupitisha bajeti ya Sh 8 bilioni kwa ajili ya msimu ujao wa 2021/2022.
Yanga imetenga kitita kikubwa cha fedha takribani Sh 4.9 bilioni ambacho kitatumika kwa usajili na ulipaji wa mishahara kwa wachezaji, maofisa wa benchi la ufundi na maofisa wengine wa klabu.
Haiishii tu katika kusajili bali pia Yanga katika kuhakikisha inaongeza morali ya nyota hao itakaowasajili, imetenga kiasi cha zaidi ya Sh 854 milioni kwa ajili ya bonasi kwa wachezaji wake.
Lakini pia imetenga kitita cha zaidi ya Sh201 milioni kwa ajili ya usafiri wa timu kwa safari za ndege za ndani na nje ukizingatia msimu ujao watashiriki mashindano ya klabu Afrika.
VIONGOZI WATAMBA
Mwenyekiti wa Yanga, Dk. Mshindo Msolla alisema mkataba huo una tija na jambo la msingi ni mashabiki na wanachama wa timu hiyo kuwapa thamani wadhamini
“Wito wangu kwa wanachama, mashabiki na wapenzi wa Yanga kiujumla niseme tu haya mambo sio rahisi, hayaji tu hivyo tuthamini sana masuala haya tunayofanya na tutatoa elimu ili tufahamu wajibu wetu,” alisema Dk. Msolla
Mshauri wa klabu ya Yanga, Senzo Mazingisa alisema Yanga inapaswa kujivunia na kukuza nembo yake
“Jambo la msingi ni kuheshimu mikataba. Tunatakiwa kujipanga katika namna ambayo mdhamini yoyote wa Yanga anapata thamani kubwa. Kubwa zaidi tunapaswa kuheshimu makubaliano na washirika wetu kwa sababu wanatupa kiasi kikubwa cha fedha,” alisema Mazingisa.