Ouma azililia pointi tatu

Muktasari:
- Tangu Ouma akabidhiwe kikosi hicho kinachoshika nafasi ya nne na pointi 53, ameiongoza timu hiyo katika mechi 12 za Ligi Kuu Bara, ambapo kati ya hizo ameshinda sita, akitoa sare mbili na kupoteza nne, huku akifunga mabao 18 na kuruhusu 11.
KOCHA wa Singida Black Stars, raia wa Kenya, David Ouma amesema licha ya kikosi hicho kupoteza kwa kuchapwa bao 1-0 na Simba, ila amewapongeza wachezaji wa timu hiyo kwa jinsi walivyopambana, huku akililia penalti mbili za wazi.
Akizungumza na Mwanaspoti baada ya mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, Mwenge jijini Dar es Salaam, Ouma alisema hawakupoteza kutokana na makosa yao, isipokuwa penalti mbili walizonyimwa ndizo zilizoamua kupoteza pointi tatu.
“Kuna muda tunapoteza na unakubaliana na matokeo lakini ukiangalia kama tungepewa penalti mbili za wazi alizoangushwa mshambuliaji wetu, Jonathan Sowah huenda tungeshinda, kiukweli imetuumiza sana ila nawapongeza wachezaji,” alisema Ouma.
Kocha huyo alisema wachezaji walitimiza majukumu yao ipasavyo, huku akiwataka kujipanga kwa ajili ya mechi ya kesho ya Kombe la Shirikisho la (FA) hatua ya nusu fainali itakayopigwa kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa Babati mkoani Manyara.
Katika mechi sita za Singida Black Stars ilizocheza dhidi ya timu zilizopo nafasi tatu za juu, imeshinda moja tu ambayo ni dhidi ya Azam FC bao 1-0, Aprili 6, 2025, ikiwa ni kisasi baada ya kuchapwa mzunguko wa kwanza mabao 2-1, Novemba 28, 2024.
Kwenye mechi nne zilizobakia mbali na hiyo ya Azam FC ya Novemba 28, 2024, ilichapwa na Yanga bao 1-0, Oktoba 30, 2024, ikachapwa tena kwenye marudiano mabao 2-1, Februari 17, 2025, kisha ikapoteza dhidi ya Simba bao 1-0, Desemba 28, 2024.
Baada ya hapo, Singida ikachapwa tena na Simba bao 1-0, la Steven Mukwala dakika ya 43, akipokea pasi ya nyota wa kikosi hicho, Jean Charles Ahoua, hivyo imepata pointi tatu tu kati ya 18, wakati ilipocheza na timu tatu zilizokuwa juu yake.
Ouma alianza kuiongoza timu hiyo Februari 4, 2025, baada ya aliyekuwa kocha mkuu wa kikosi hicho, Miloud Hamdi aliyetambulishwa Desemba 30, 2024, kuondoka kikosini hapo na kujiunga na mabingwa watetezi wa Ligi Kuu, Yanga anayoendelea kuifundisha sasa.
Hamdi mwenye uraia pacha wa Algeria na Ufaransa akiwa na leseni A ya UEFA, aliondoka Singida bila ya kuiongoza katika mechi yoyote, ambapo alijiunga nayo ili kuchukua nafasi ya Mbelgiji Patrick Aussems aliyeondoka Novemba 29, 2024.
Tangu Ouma akabidhiwe kikosi hicho kinachoshika nafasi ya nne na pointi 53, ameiongoza timu hiyo katika mechi 12 za Ligi Kuu Bara, ambapo kati ya hizo ameshinda sita, akitoa sare mbili na kupoteza nne, huku akifunga mabao 18 na kuruhusu 11.