Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Yanga noma, yaifumua Majimaji na kurejea kileleni

Muktasari:

Ushindi huo umeiwezesha Yanga kurejea kileleni ikiiengua Azam

YANGA imerejea kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara baada ya kuifumua Majimaji ya Songea kwa mabao 5-0, lakini gumzo kubwa ni kasi ya ufungaji ya straika, Amissi Tambwe.

Tambwe alifunga mabao matatu ‘Hat Trick’ katika pambano hilo la Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam na kufikisha mabao 13 akimkimbia Hamis Kiiza wa Simba mwenye mabao 10.

Hat Trick hiyo ni ya pili msimu huu na ya saba kwake tangu aanze kucheza soka Tanzania mwaka 2013 na kumfanya aweke rekodi ambayo huenda ikachukua muda mrefu kufikiwa.

Ushindi huo umeiwezesha Yanga kurejea kileleni ikiiengua Azam iliyochukua uongozi wa ligi hiyo kwa muda baada ya juzi Jumatano kwa kupata ushindi mjini Tanga dhidi ya Mgambo JKT. Timu zote zina pointi 39 baada ya kushuka uwanjani mara 15 kila moja, lakini uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa unawabeba vijana wa Jangwani.

Yanga ilianza pambano hilo kwa kasi na dakika ya tano tu, Thabani Kamusoko, akafunga bao kiufundi akimalizia pasi na Deus Kaseke. Bao hilo lilidumu hadi mapumziko licha ya kuwepo kwa kosa kosa pande zote.

Kipindi cha pili, Yanga ilitandaza soka la kuvutia lililosisimua wengi na kufanikiwa kuandika bao la pili lililofungwa na Donald Ngoma katika dakika ya 47, kabla ya Tambwe kufunga mabao yake katika dakika 57, 72 na 85 na kuipa Yanga ushindi mnono msimu huu na pia kufuata nyayo za Simba kuipa kipigo kikubwa Majimaji baada ya miezi michache kuicharaza 6-1.

Kwa Hat Trick hiyo Tambwe alipewa mpira baada ya mechi.   

Katika michezo mingine,  Mwadui FC ikiwa nyumbani mjini Shinyanga, iliitambia Kagera Sugar kwa mabao 2-1. Mabao yake yalifungwa na Jerry Tegete na Nizar Khalfan wakati la wageni lilifungwa na Babu Ally.

Jijini Tanga, vibonde African Sports walilazimisha sare ya 0-0 na Mtibwa Sugar.

Yanga: Deo Munishi, Juma Abdul/Said Juma, Oscar Joshua, Vincent Bossou, Kelvin Yondani, Salum Telela, Simon Msuva/Issofou Boubacar, Thabani Kamusoko, Donald Ngoma/Paul Nonga, Amissi Tambwe na Deus Kaseke.

Majimaji: David Burhan, Alex Kondo, Bahati Yusuf, Mpoki Wakinyuke, Sadiq Gawaza, Lulanga Mapunda/Kennedy Kipepe,  Peter Mapunda/Hassan Hamis, Peter Maona/ Godfrey Taita, Marcel Bonaventure, Sixmund Mwakasega na Frank Sekule.