Yanga ni mwendo wa dozi mpaka Polisi

Wednesday June 22 2022
FULL PIC
By Thobias Sebastian

Mabingwa wa Ligi Kuu NBC Yanga imeendeleza rekodi ya kucheza mchezo wa mzunguko 28, bila kupoteza baada ya kuifunga Polisi Tanzania mabao 2-0 kwenye mchezo wa leo.

Mchezo huo uliochezwa kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa na Yanga kuibuka na ushindi kwa mabao mawili ya yaliyofungwa na Feisal Salum dakika 12 pamoja na Chiko Ushindi dakika 17.

Kutokana na matokeo hayo Yanga imeendelea kusalia kileleni mwa msimamo wa Ligi baada ya kufikisha pointi 70 wakati Polisi Tanzania wao kwa matokeo hayo wamesalia nafasi ya saba kwenye msimamo.

Kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi baada ya mechi kumalizika kwa timu yake kupata ushindi amesema wameendelea kuwa na umakini mkubwa licha ya kutwaa ubingwa kabla ya mchezo wa leo.

Nabi amesema wangeanza kucheza kwa kujiachia zaidi linaweza kutokea jambo baya na wakashindwa kufanya vizuri kwenye fainali ya kombe la ASFC.

“Siyo rahisi kucheza mechi kama ya Polisi Tanzania huku tukiwa na wachezaji ambao akili zao walikuwa na uhakika tayari tumeshatwaa ubingwa wa ligi,” amesema Nabi na kuongeza;

Advertisement

“Ukitoa mpira wa Chiko Ushindi tumepiga mipira mingi ambayo haikulenga lango, tumefanya mabadiliko ya wachezaji si kitu kibaya kutokana na kupata matokeo mazuri."

“Tulitaka kufanya mabadiliko makubwa zaidi ila uchache wa kikosi ndio maana kuna maeneo hatukubadilisha kama pale kwa kiungo wamejirudia wale wale Khalid Aucho na Salumu Abubakar.”

Kocha msaidizi wa Polisi Tanzania, George Mketo alisema wachezaji wake wamecheza vizuri ila makosa ya kiulinzi haswa kipindi cha kwanza ndio sababu ya kuruhusu mabao mawili.

“Kilicho mbele yetu ni kuhakikisha tunarekebisha makosa ya leo ili kushinda michezo miwili iliyokuwa mbele yetu na kupata pointi zote sita,” amesema Mketo na kuongeza;

“Kipindi cha kwanza tulifanya makosa hayo ya kiulinzi ila kipindi cha pili tuliboresha ndio maana hatukuruhusu bao lolote."

“Ukomavu na uzoefu kwa wachezaji wengi wa Yanga pengine ulikuwa sababu ya kutuwahi kipindi cha kwanza na kupata hayo mabao ila wachezaji wangu wote wamecheza vizuri.”

Advertisement