Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Yanga ndani mtiti nje mtiti utaipenda

Muktasari:

Tayari Yanga imeshasajili wachezaji watano wapya Tariq Seif, Adeyum Saleh, Haruna Niyonzima, Ditram Nchimbi na Yikpe Gnamien, huku wakiwa mbioni kumalizana na nyota wengine wawili akiwamo Mkongo, Owe Banyanga Ituku anayesubiri kuanguka saini tu.

SUALA la matokeo ni jambo jingine, lakini kwa namna mabosi wa Yanga walivyokiboresha kikosi chao kupitia dirisha dogo litakalofungwa wiki ijayo, imewafanya mabingwa hao wa kihistoria wa Tanzania kuwa moto nje na ndani na wapinzani wao waanze tu kujipanga.
Ujio wa nyota kadhaa ndani ya kikosi cha Yanga, umekifanya kiwe kipana kinachowapa nafasi makocha wao kuamua watumie wachezaji gani, kwani wanaoanza na wale wanaobaki benchi wote wanaonekana kuwa moto uleule unaounguza.
Tayari Yanga imeshasajili wachezaji watano wapya Tariq Seif, Adeyum Saleh, Haruna Niyonzima, Ditram Nchimbi na Yikpe Gnamien, huku wakiwa mbioni kumalizana na nyota wengine wawili akiwamo Mkongo, Owe Banyanga Ituku anayesubiri kuanguka saini tu.
Usajili huo umeifanya Yanga iwe na jumla ya wachezaji 33, wanaoweza kutengeneza vikosi vitatu ambavyo kati ya hivyo vyote imara na vinaweza kufunga katika mchezo wowote ule ambao watakutana nao.
Kwa aina ya wachezaji walionao, Yanga inaweza kuanza na kikosi cha kwanza cha wachezaji hawa: Farouk Shikhalo, Paul Godfrey, Adeyum Saleh, Lamine Moro, Kelvin Yondani, Abdulaziz Makame, Deus Kaseke, Haruna Niyonzima, Ditram Nchimbi, Tariq Seif na Patrick Sibomana.
Lakini pia inaweza kupanga mziki wake ukiwajumuisha Metacha Mnata, Juma Abdul, Ally Mtoni ‘Sonso’, Moustapha Seleman, Ali Ali, Papy Tshishimbi, Mrisho Ngassa, Feisal Salum, David Molinga, Yikpe Gnamien na Mapinduzi Balama ‘Kipenseli’.
Achana na vikosi hivyo unaambiwa bado Yanga ina majembe mengine matata baadhi walikipiga juzi kwenye mechi ya Kombe la Mapinduzi na kushinda mabao 2-0 dhidi ya Jamhuri ya Pemba.
Kikosi cha tatu cha Yanga kinatengenezwa na kipa Ramadhani Kabwili, Jafary Mohammed, Mharami Issa ‘Marcelo’, Cleofas Sospeter, Andrew Vincent, Said Juma, Juma Mahadhi, Raphael Daud, Said Mussa, Owe Banyanga na Gustapha Saimon.

KASHASHA AICHAMBUA
Mchambuzi wa masuala ya soka nchini, Alex Kashasha alisema licha ya Yanga kuonekana kukitanua kikosi chake, lakini haiwezi kuwa na uhakika wa kuja kunufaika nao kama ilivyo matarajio ya wengi.
Kashasha alisema kwa muda mrefu klabu za soka nchini zimekuwa na utamaduni wa kufanya usajili kila msimu kuanzia dirisha kubwa na dogo ila wachezaji wengi wanaosajiliwa ni wale ambao huja kutokuwa na msaada.
Kashasha alisema Yanga imesajili wachezaji watano hadi sasa, lakini mpaka dirisha likifungwa watakuwa wamesajili wasiopungua saba, ila kati ya hao haoni kama wote wanaweza kuwa na umuhimu katika timu kutokana na kutokuwa na muda wa kutosha wa kuwafuatilia.
“Maana ya kuwa na kikosi kipana kuona kila mchezaji katika timu ana uwezo sawa na mwenzake, ila ukiangalia wachezaji wapya waliosajiliwa Yanga na waliokuwepo ndani ya timu uwezo wao haufanani kabisa, ingawa kwa mashabiki wanaona tofauti,” alisema.
“Ndani ya Yanga kuna wachezaji wasiozidi 18 wanaotumika mara kwa mara,  wengine wamekuwa wakikaa benchi muda mwingi jambo linalowafanya licha ya kuwa na vikosi vitatu, ila hawana msaada labda makocha wabadilike.
“Kwa maana hiyo, nyota wa kigeni waliosajiliwa Yanga huenda wakaongeza wingi wa wachezaji na kufanya timu hiyo kuwa na wachezaji wengi lakini wakashindwa kufanya vizuri, labda kama watawatengea muda wa kutosha na kuwafuatilia wanaweza kuingiza kitu katika timu na tafsiri ya kuwa na kikosi kipana ikawepo.”
Naye nyota wa zamani wa Yanga na Kocha Msaidizi wa sasa wa Serengeti Boys, Maalim Saleh ‘Romario’, alisema anaona makocha wameongezewa mzigo tu, kwani wengi hawatatumika kwenye mashindano.
“Naamini kila mchezaji atapambana kupata nafasi na mwishowe mzunguko utawagusa wachache na hapo upana hautakuwa na maana kwani kitapatikana kikosi kimoja tu cha kuchezaji licha ya kuonekana kwa sasa wana vikosi vitatu vikali,” alisema Romario.