Yanga: Mnachonga sana, nyie tukutane kimataifa

Muktasari:

Yanga wamesikia kishindo cha Simba mjini Dodoma baada ya kutwaa kombe la FA juzi Jumamosi. Sasa Viongozi wa Yanga wametia neno namna hali halisi itakavyokuwa kuanzia Februari mwakani...

KATIBU Mkuu wa Yanga na kocha wa zamani wa Taifa Stars, Boniface Charels Mkwasa, amesema kitendo cha Simba kutwaa taji la FA, kutaongeza hamasa ya ushindani wa kujua nani anaweza kufika mbali zaidi kimataifa.

Mkwasa alielezea kwamba hamasa hiyo itatokana na  mashabiki wa Simba na Yanga, ambao wanatambiana nani atakuwa mwamba kuhakikisha anakuwa na mafanikio ya kimataifa.

“Itategemeana Yanga na Simba nani atapangiwa mechi ngumu ama rahisi, jambo hili litaamsha ushindani wa hali ya juu kwa mashabiki hapa nchini, ukichukulia Simba, wamesota ndani ya miaka mitano bila mafanikio ya ligi ya ndani,”alisema

Licha ya Mkwasa, kukiri kwamba kutakuwepo kwa ushindani mkali kwa pande hizo mbili, alitamka kuwa Yanga inapaswa kupewa heshima yake kutwaa ubingwa mara tatu mfululizo jambo ambalo si jepesi kabisa.

“Heshima ya Yanga, kutwaa ubingwa wa kihistoria itabakia pale pale ingawa ikianza michuano ya kimataifa itategemeana na mwanzo wa mechi tutakazopangiwa zitakuweje baina ya watani wetu Simba,” alisema.

Kuhusu maandalizi ya michuano ya Sport Pesa ambapo Yanga watacheza na Tusker ya Kenya, Mkwasa alisema kikosi kipo salama mkoani Arusha ambako kinafanya mazoezi na kujipima kwenye mechi za kirafiki.

Majeruhi kuitesa Yanga

Kocha Msaidizi wa Yanga, Juma Mwambusi amesema kikosi chake  kinakabiliwa na majeruhi wengi kuelekea katika michuano ya SportPesa inayoanza Juni 5.

Mwambusi alisema kuwa kutokana na matatizo hayo, asilimia kubwa ya wachezaji wanapata nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza hawakuweza kusafiri na wenzao waliopo Arusha kwa ajili ya mchezo wa kirafiki dhidi ya AFC.

“Wachezaji walikuwa wanafanya kazi kwa ajili ya kutetea timu na taifa lao ndio maana baada ya kumaliza ligi kuu wakapewa muda wa kupumzika hasa wale ambao, wamecheza chezo nyingi kama mnavyojua hatukuwa na muda wa kupumzika kabisa,” alisema Mwambusi.