Che Malone, Inonga yawakuta Simba

Muktasari:

  • Pawasa ambaye alifanya makubwa ndani ya timu hiyo ikiwemo kuwa kwenye kikosi kilichoiondosha Zamalek ya Misri kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2003, amesema Simba inamkosa beki mwenye sifa ya kucheza mtu wa mwisho.

Kwa namna Simba ilivyokuwa rahisi kuruhusu mabao msimu huu ndani ya Ligi Kuu Bara, beki wa zamani wa timu hiyo, Boniface Pawasa amesema msimu ujao lazima uamuzi mgumu ufanyike wa kusajili beki mwingine mwenye uwezo wa kuituliza safu hiyo ya ulinzi kwa maana, waliopo wameshindwa kutimiza majukumu yao.

Pawasa ambaye alifanya makubwa ndani ya timu hiyo ikiwemo kuwa kwenye kikosi kilichoiondosha Zamalek ya Misri kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2003, amesema Simba inamkosa beki mwenye sifa ya kucheza mtu wa mwisho.

Katika kikosi cha Simba, Henock Inonga na Che Malone Fondoh, ndiyo mabeki wa kati wanaocheza mara kwa mara, hivyo Pawasa amebainisha mabeki hao wote wana aina moja ya uchezaji, hivyo lazima asajiliwe mwingine ambaye atacheza na mmoja kati ya hao.

Rekodi zinaonyesha, katika mechi 21 za ligi Simba ilizocheza kabla ya kukutana na Namungo, imeruhusu mabao 21, wastani wao ni kuruhusu bao moja kila mechi. Ukiangalia timu za nne bora kwenye msimamo, Simba ndiyo imeruhusu mabao mengi, inafuatiwa na Coastal Union (18), Azam FC (16) na Yanga (12).

"Ukiangalia mabeki wa kati wa Simba, Che Malone na Inonga wote hawawezi majukumu ya kuwa mtu wa mwisho, kila mmoja anatamani kwenda mbele kushambulia, hilo ni tatizo la kwanza," alisema Pawasa na kuongeza.

"Wanatakiwa kuboresha eneo hilo kwanza kwa sababu timu lazima iwe na mtu wa mwisho ambaye jukumu lake kubwa ni kuiongoza safu ya ulinzi."

Pawasa alibainisha, mbali na mabeki wa kati, pia pembeni kuna shida kwa sababu Shomari Kapombe na Mohamed Hussein 'Tshabalala' wamekuwa wakitumika kwa muda mrefu, hivyo wamechoka na wanahitaji kupumzishwa.

"Kapombe na Tshabalala wamechoka, hivyo timu inatakiwa kuboreshwa eneo la pembeni kwa kutafuta mabeki ambao wana uwezo wa kuwapa changamoto waliopo.

"Pia waboreshe eneo la kipa kwa sababu timu kama Simba, mhimili mkubwa ni eneo hilo, simaanishi waliopo ni wabaya, bali soka la sasa linahitaji makipa wa kisasa zaidi ambao wanaweza kuanzisha mashambulizi," alibainisha Pawasa.

TAKWIMU ZIPOJE?
Miongoni mwa vitu vinavyoangaliwa ili kuona uimara wa timu ni namna safu ya ulinzi inavyofanya kazi, katika hilo, Simba inaonekana msimu huu kuna tatizo.

Kikosi cha kwanza cha timu hiyo, ukiangalia safu yake ya ulinzi mara nyingi huundwa na mabeki Shomari Kapombe, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, Henock Inonga na Che Malone Fondoh. Golini anakuwepo Ayoub Lakred au Ally Salim, hiyo ni baada ya Aishi Manula kutokuwa fiti.

Ukiangalia katika mabao 21 ambayo Simba imeruhusu msimu huu, ni mabao manne pekee unaweza kusema yamefungwa kutokana na juhudi na mbinu za wapinzani, yaliyobaki yote ni makosa ya safu ya ulinzi.

Katika hayo makosa, Che Malone anaongoza kwa kufanya mara tano, anafuatia Kapombe (4), huku Tshabalala na Ally Salim kila mmoja akifanya makosa matatu kama ilivyo kwa Inonga. Hapa kuna uchambuzi wa makosa hayo katika kila mechi.

CHE MALONE & TSHABALALA
Katika mchezo ambao Simba ilishinda mabao 4-2 ugenini dhidi ya Mtibwa Sugar, Agosti 17, 2023, mabao mawili yaliyofungwa na wenyeji yalitokana na makosa ya safu ya ulinzi ya Simba.

Simba walipata mabao mawili ya haraka dakika ya 2 na 5, lakini wakajikuta wakiruhusu mabao mawili dakika ya 20 na 22, yote yakifungwa na Matheo Antony.

Bao la kwanza lililofungwa na Matheo, lilitokana na Che Malone kupokonywa mpira kirahisi na Nashon Naftal ambaye alirudisha shambulizi langoni mwa Simba, likazaa bao.

Muda mchache mbele, Simba ikaenda kushambulia, Mtibwa wakafanya shambulizi la kushtukiza, Matheo Anthony akaipokea pasi akitumia makosa ya Tshabalala aliyepanda mbele bila ya tahadhari, anafunga.

CHE MALONE
Licha ya Simba kushinda mabao 3-1 ugenini dhidi ya Tanzania Prisons, lakini Che Malone alifanya tukio ambalo liliwafanya Simba kuruhusu bao la mapema dakika ya 12 kupitia Edwin Balua, kabla ya kurekebisha makosa yao.

Mchezo huo uliopigwa Oktoba 5, 2023 kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya, ulishuhudiwa bao la Tanzania Prisons likitokana na makosa ya Che Malone aliyekwenda kucheza faulo wakati wa kuzuia shambulizi nje kidogo ya eneo la hatari, ikapigwa faulo ya moja kwa moja mpira ukajaa wavuni.

ALLY SALIM
Hii ni mechi ya tatu ambayo Simba inashinda, lakini safu ya ulinzi inaendelea kufanya makosa na kuwaruhusu wapinzani kupata bao.

Oktoba 8, 2023 katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Liti, mkoani Singida, wenyeji Singida Fountain Gate walijikuta wakilala kwa mabao 2-1 mbele ya Simba, lakini bao lao lilikuwa ni kama zawadi kutoka kwa kipa wa Simba, Ally Salim.

Hiyo ilitokana na kipa huyo kushindwa kuokoa vizuri shuti lililopigwa na Duke Abuya, mpira ukabaki eneo la hatari, baadaye Deus Kaseke akaweka mpira kambani. Kumbuka bao hilo lilikuwa la kusawazisha, kabla ya baadaye Simba kufungua bao la ushindi.

ALLY SALIM
Ally Salim anafanya kosa lingine kama lile la kupangua mpira na kumfikia mpinzani anayeuweka mpira kambani. Safari hii ilikuwa ni Simba 2-1 Ihefu, mechi ikichezwa Oktoba 28, 2023 Uwanja wa Mkapa, Dar.

Shuti kali linatua mikononi mwa Ally Salim, anapangua mpira na kuangukia miguuni mwa Ismail Mgunda, anafunga kirahisi.

SIMBA 1-5 YANGA
Mchezo huu uliochezwa Uwanja wa Mkapa, Novemba 5, 2023, unaweza kusema mabao yote waliyoruhusu Simba yalitokana na makosa ya safu yao ya ulinzi.

Bao la kwanza, Kennedy Musonda anaruka kichwa katikati ya Kapombe na Che Malone, anafunga. Mabeki hao walishindwa kujipanga vizuri kumzuia mtu mmoja.

Baadaye Maxi Nzengeli anapita bila ya kupingwa katikati ya Kapombe na Che Malone akiiwahi pasi ya Aziz Ki, anafunga.

Aziz Ki anapokea pasi katikati ya Fabrice Ngoma, Kapombe na Inonga, anafunga. Shambulizi hilo lilianzia mbali pale Kiungo wa Yanga, Pacome Zouzoua alipochukua mpira akiwa eneo lao, anakimbizwa kivivu na Sadio Kanoute, anatoa pasi kwa Clement Mzize ambaye anawahadaa Tshabalala na Che Malone, anamuachia Aziz Ki, anafunga.

Mzize tena anamtoka Che Malone, kisha Tshabalala anamsindikiza mpaka kwenye boksi, anatoa pasi kwa Maxi, anafunga bao la nne.

Bao la nne linaanzia pale Inonga anabutua mpira mbele bila ya utaratibu mzuri, unamfikia Joyce Lomalisa ambaye anatoa pasi kwa Aziz Ki, anamuachia Maxi anaingia kwenye boksi, Inonga anacheza faulo, inakuwa penalti ambayo Pacome anafunga bao la tano.

KAPOMBE
Sare ya bao 1-1 kati ya Simba dhidi ya Namungo mchezo ukipigwa Uwanja wa Uhuru Novemba 9, 2023, kosa la Kapombe kuvunja mtego wa kuotea, linawafanya Namungo kupata bao la kuongoza kupitia Reliants Lusajo.

AYOUB
Desemba 23, 2023, matokeo yalikuwa KMC 2-2 Simba mechi ikichezwa Uwanja wa Azam Complex, katika mabao mawili ya Wazir Junior, moja lilitokana na kipa Ayoub Lakred kupangua shuti ambalo mwisho wa siku mpira ukatua miguuni mwa mfungaji, akaweka ubao sawa. Kabla ya hapo, Simba ilikuwa mbele kwa mabao 2-1. Mechi ikaisha 2-2.

KIBU DENIS
Ni mara moja pekee imetokea Kiungo mshambuliaji kufanya kosa lililozaa bao kwa Simba, huyu si mwingine bali ni Kibu Denis aliyefanya hivyo wakati Simba ikifungwa 2-1 na Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro, Machi 6, 2024. Katika mchezo huo, Simba hawatamsahau Samson Mbangula ambaye alifunga mabao yote mawili.

Bao la kwanza, Simba wanaanzisha kona fupi, Kibu anachelewa kutoa pasi, anapokonywa, inapigwa ‘counter attack’, Mbangula anafunga. Baadaye Inonga, Ngoma na Kennedy Juma, wanashindwa kumzuia Mbangula ambaye anaingia ndani ya boksi na kufunga.

ALLY SALIM
Safari hii Ally anashindwa kuicheza krosi katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Liti, Singida Aprili 13, 2024, matokeo mwisho yalikuwa Ihefu 1-1 Simba.

Krosi iliyopigwa na Elvis Rupia, Ally anapishana na mpira unaomkuta Duke Abuya, anafunga bao la uongozi kwa Ihefu. Baadaye Simba wanasawazisha.

HUSSEIN KAZI & TSHABALALA
Katika dabi mbili za Kariakoo ambazo Simba imepoteza msimu huu ndani ya ligi, mabao yote yametokana na makosa ya walinzi. Ukiachana na ile ya kwanza 5-1, safari hii walipofungwa 2-1, walinzi tena wamefanya yao.

Bao la kwanza, Kiungo Babakar Sarr anampa pasi beki wa kati Hussein Kazi akiwa pembeni ya uwanja, anashindwa kufanya uamuzi wa haraka, Aziz Ki anauchukua mpira na kukimbilia kwenye boksi, Kazi anakuja kwa nyuma na kucheza faulo, mwamuzi anafunika penalti, Aziz Ki anafunga.

Pasi ndefu ya Khalid Aucho, inamfikia Joseph Guede ambaye anatumia makosa ya Tshabalala aliyeshindwa kuondoka kwenye mtego wa kuotea waliouweka, anawaadhibu.