Yanga kuwakosa nyota watatu kesho ikiivaa Gwambina

WAKATI Gwambina wakijiandaa kinidhamu na kujilinda wakiamini ndiyo silaha katika mchezo wa kesho Aprili 20 saa 1 usiku, kwa upande wa Yanga watawakosa nyota watatu katika mchezo huo.

Yanga atakuwa mwenyeji wa Gwambia Uwanja wa Benjamin Mkapa wakitoka kupata matokeo mchezo uliopita dhidi ya Biashara huku Gwambina wao wakitoka kupoteza dhidi ya KMC.

Kocha wa Gwambina Mohamed Badru amesema lengo ni kushinda mchezo wao na Yanga, lakini anaheshimu ukubwa wao kwa kuamini wanaweza kupambana kwenye njia nyingi akiamini uchanga wa timu yake sio sababu ya wao kupoteza.

"Ila wakija kwa kutubeza hawatahamini matokeo lakini wakituheshimu mchezo utakuwa laisi ila tunataka kuvunja mwiko wa kutofungwa,Yanga ina wachezaji wazuri hivyo tutahakikisha hatuchezi kwa kuzuia na vijana wangu nimewataka wacheze kwa nidhamu ya hali ya juu,"amesema.

"Yanga ni timu kubwa natakiwa kuongeza ufanisi wa nidhamu katika mchezo huo, hata kikosi kitakachocheza na Yanga hata wachezaji wangu watakuwa na uwezo binafsi zaidi kesho mnaweza kuona sura tofauti kabisa,"

Kwa upande wake Nahodha wa Gwambina Paul Nonga amesema, kwa upande wao wachezaji wamejiandaa vizuri kukabiliana na mchezo wa kesho dhidi ya Yanga.

Amesema wanahitaji matokeo katika mchezo huo na wao kama wachezaji watahakikisha wanaingia kwa nidhamu na makosa waliyoyafanya katika mchezo uliopita wameyafanyia kazi zaidi yasijirudie katika mchezo huo.

Kwa upande wao Yanga kupitia kwa Kaimu Kocha Mkuu wa Yanga Juma Mwambusi amesema, kikosi chake kipo tayari kwa mchezo huo.

"Hatuwezi kuwabeza Gwambina, ni mchezo mgumu sana kwetu sote, ligi msimu huu imekuwa na ushindani zaidi, na sisi Yanga tunapambana zaidi kuhakikisha tunapata matokeo kesho,"

Mwambusi amesema atawakosa nyota watatu katika mchezo wao wa kesho ambao ni Mapinduzi Balama, Feisal Salum na Yassin Mustapha ambao wanamajeraha.

Kwa upande wake Nahodha Msaidi wa Yanga Haruna Niyonzima amesema, wanawaheshimu Gwambia kwa kuwa ni mchezaji muhimu kwa timu zote hivyo hata wao watajitahidi kupambana kupata matokeo.

"Ni mechi ngumu sana kwetu sote na itakuwa na ushindani kwetu sote wawili, hata sisi wachezaji tunawaheshimu sana Gwambina," amesema.