Yanga kamili gado

Muktasari:

  • Pacome alikuwa Ufaransa na timu ya taifa ya Ivory Coast ambayo ilicheza mechi mbili za kirafiki za kimataifa, japo mwenyewe aliishia benchi na alitua juzi usiku na kupokewa na beki Yao Kouassi, tayari kwa kasi ya kuikabili Mamelodi waliotua saa 1 usiku wa jana kutoka Afrika Kusini baada ya kutanguliza nyota saba waliokuwa, Bafana Bafana.

KAMBI ya Yanga imenoga baada ya nyota waliokuwa timu za taifa, akiwamo Pacome Zouzoua kurejea na moja kwa moja kuungana na wenzao kujiandaa na mechi ta robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Mamelodi Sundowns.


Pacome alikuwa Ufaransa na timu ya taifa ya Ivory Coast ambayo ilicheza mechi mbili za kirafiki za kimataifa, japo mwenyewe aliishia benchi na alitua juzi usiku na kupokewa na beki Yao Kouassi, tayari kwa kasi ya kuikabili Mamelodi waliotua saa 1 usiku wa jana kutoka Afrika Kusini baada ya kutanguliza nyota saba waliokuwa, Bafana Bafana.


Mastaa walioshuka juzi ni kipa namba moja Ronwen Williams, Grant Kekana, Aubrey Modiba, Teboho Mokoena, Themba Zwane, Terrence Mashego na Thapelo Morena baada ya kukodishiwa ndege na klabu wakitokea Algeria na usiku wa jana msafara mzima wa timu hiyo ulitua na dege jingine.


Lakini kwa upande wa Yanga ni kwamba mbali na Pacome, lakini nyota waliokuwa timu za taifa akiwamo kipa Diarra Djigui, Stephane Aziz KI, Kennedy Musonda, kipa Aboutwalib Mshery na Bakar Mwamnyeto waliokuwa Taifa Stars nao wameshatimba kambini kuungana na wenzao mazoezini.


Yanga itavaana na Mamelodi kesho Jumamosi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kuanzia saa 3:00 usiku kabla ya kwenda kurudiana wiki ijayo jijini Pretoria, Afrika Kusini na mshindi wa jumla atasonga nusu fainali kucheza ama na Esprance ya Tunisia au Asec Mimosas ya Ivory Coast.


Waliokuwa majeruhi kama Kibwana Shomari, Khalid Aucho, Zawadi Mauya wanaendelea na tizi wakati Yao akiendelea kuwa chini ya usimamizi wa kocha wa viungo, Yossouf Ammar ili kuona kama anaiwahi mechi hiyo ya kesho.


Aidha, Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe aliweka wazi ishu ya beki wa kati, Ibrahim Bacca kuwa huenda akakosa mechi ya kesho kutokana na kuwa na kazi za njano tano na kufafanua mwamba yupo uwanjani kama kawaida.


Kamwe alisemani kweli Bacca ameonyesha kadi tano katika mechi sita za makundi za Yanga, lakini tatu alizopewa mechi za awali za makundi alitumika kwa kukosa mechi ya nyumbani dhidi ya Medeama ya Ghana na zile mbili alizopata mbele ya CR Belouizdad na Al Ahly zimefutwa kwa Yanga kutinga robo.


“Mashabiki wasiwe na hofu, mie ndiye Ofisa Habari wa Yanga, kama Bacca au mchezaji yeyote angekuwa na tatizo la kukosa mchezo, ningewafahamisha, “ alisema Kamwe akihojiwa na kituo kimoja cha redio kuhamasisha mchezo huo unaokuwa wa tatu kwa timu hiyo kukutana na Mamelodi.


Awali zilishakutana katika mechi mbili za raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa msimu wa 2001 na Yanga kufungwa jumla ya mabao 6-5, ikipasuka 3-2 ugenini na kutoka sare ya 3-3 nyumbani.