Yanga, Hospitali za Aga Khan zaja na sapraizi kwa mashabiki

Muktasari:
- Klabu ya Yanga imechukua hatua ya kusaini mkataba na Hospitali za Aga Khan wakati huu ambao klabu hiyo ikitarajiwa kuadhimisha miaka 89, huku taasisi hiyo ya Aga Khan, ikitimiza miaka 95 tangu kuanzisha kwake Tanzania..
KLABU ya Yanga imesaini mkataba wa miaka miwili na Taasisi ya Aga Khan kwa hospitali zake kuiwezesha kupatiwa matibabu kwa wachezaji, viongozi, wafanyakazi na mashabiki kwa gharama nafuu.
Hatua hiyo imekuja wakati huu klabu hiyo ikitarajiwa kuadhimisha miaka 89, huku taasisi hiyo ya Aga Khan, ikitimiza miaka 95 tangu kuanzisha kwake Tanzania, ikihusisha ushirikiano huo na Yanga ambao imeitaja ni bora kwenye soka huku Aga Khan ikijikita kwenye huduma bora za afya kwa wagonjwa inayowahudumia.
Makubaliano hayo yamefanyika leo ikiwa ni klabu ya pili kufanya hivyo baada ya Azam FC kufanya hivyo mwaka jana na mashabiki watapata punguzo kwenye matibabu kama watakuwa na kadi zitakazowawezesha kupata huduma kwa gharama nafuu.
Mtendaji Mkuu Taasisi za Huduma za Afya Aga Khan Tanzania, Sisawo Konteh amesema ushirikiano baina ya taasisi hiyo na Yanga utawanufaisha mashabiki wa Yanga ambao ni wengi nchini na wachezaji kuwa na afya njema.
"Kama mashabiki wakiwa na afya nzuri, klabu pia itakuwa na afya na kama wakiwa hawana afya na klabu haitakuwa na afya na uongozi utakazingatia ushirikiano unaokwenda mbali zaidi ya soka, ni uongozi wenye mipango mizuri," alisema Konteh.
Rais wa klabu hiyo, Hersi Said amesema lengo la makubaliano hayo ni kuhakikisha mashabiki na wanachama wao wananufaika na huduma bora za hosipitali hiyo, ingawa nembo ya hospitali hiyo haitakuwa katika jezi zao.
Ameeleza faida watakazozipata mashabiki hao ni kwenye matawi ya hospitali hiyo yaliyo karibu nao na watapata punguzo kutokana na uwezo wa kiuchumi wa eneo husika.
"Tumeona ni muhimu kujenga afya bora kwa kuwa na programu maalumu kwa wananchi, lakini hata kwa wachezaji na ukizingatia maendeleo ya kimichezo yanategemea sana afya bora," amesema na kuongeza.
"Mwanachama mwenye kadi hai wa Yanga atapata punguzo la bei. Aga Khan ina vituo vya afya katika maeneo mbalimbali sawa na uwezo wa watu katika eneo husika."
"Wanachama wasihofie gharama na waende kutibiwa ili kupata matibabu ya uhakika, hii ni faida kubwa ambayo wanaipata, kwani tunajenga thamani ambayo wametupatia kwa kuiamini timu yao, ndiyo maana hatukutaka iishie kwa viongozi na wachezaji tu," alisema Hersi.
Msemaji wa Yanga, Ali Kamwe alisema,"Ada ni Sh24,000 kwa mwaka na kwa hiyo wanachama wanaweza kupata kadi halali ya uanachama jambo ambalo litawapa kibali cha kupata punguzo hilo."
Kutokana na hili, Yanga itakuwa na wanachama wengi zaidi watakaojisajili tofauti na majirani zao Azam kwani kati ya timu hizi mbili Wanajangwani ndio wanaongoza kwa kuwa na mashabiki wengi zaidi.
Hata hivyo, Azam iliishia kuwapatia matibabu wachezaji na wafanyakazi jambo ambalo Yanga wamewapiku kwa kwenda mbali zaidi kwa kuwahusisha mashabiki.