Yanga: Daima mbele, hatubahatishi

Wachezaji wa timu ya Yanga wakishangilia kwa pamoja ishara ya kutiana moyo
WAANDISHI WETU KIRAKA Haruna Niyonzima 'Fabregas' na kocha wake, Ernest Brandts wamesisitiza kwamba sasa Yanga inateleza tu na wako vizuri wala hawabahatishi. Fabregas amesema kichapo cha bao 1-0 walichoipa Azam Jumamosi iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa kilisababishwa na udhaifu wa safu ya ulinzi ya Azam. Haruna alisema kutokuwepo kwa mabeki waliosimamishwa kwa tuhuma za rushwa, Aggrey Morris na Erasto Nyoni kulimpa urahisi kwani wachezaji hao wamekuwa kikwazo kila timu hizo zinapokutana. "Morris na Nyoni ni mabeki ambao walikuwa wagumu kuona mpira ukipita," alisema mchezaji huyo ambaye anacheza pia kama kiungo wa kushoto na kuongeza pia kuwa: "Bao limekuwa muhimu kwangu, lakini nakuambia ni maalumu kwa mke wangu, Naila." "Kabla ya mechi nimemwambia mke wangu natamani sana nifunge bao na usiku kabla ya kulala tulikuwa tunafanya maombi sana kuona tunafanikiwa,"alisema Fabregas. "Kweli Mungu amejibu imekuwa kweli na ndivyo nami ninavyomzawadia zawadi hii mke wangu spesho Naila,"alisisitiza Fabregas nyota tegemeo wa timu ya taifa ya Rwanda 'Amavubi'. Bao hilo ni kama dhahabu kwani lilikuwa linahitajika na timu zote mbili kwa kuwa Azam ndio wapinzani wao wakuu na ushindi kwa timu yoyote ungekuwa na maana kubwa katika kulisaka taji la Ligi Kuu. Kwa sasa Yanga inaongoza ligi kwa pointi 39 wakiwa mbele ya Azam kwa pointi tatu zaidi. Azam inashika nafasi ya pili kwa pointi 36 wakati Simba iko nafasi ya tatu ikiwa na pointi 31. Mashabiki Ukiacha mechi ya watani, Simba na Yanga hakuna mchezo ambao umeingiza mashabiki wengi kama ilivyokuwa kwa Yanga na Azam FC uliopigwa Uwanja wa Taifa wenye uwezo wa kubeba mashabiki 60,000 walioketi. Jumla ya mashabiki 39,315 waliingia kushuhudia mchezo huo kwa viingilio tofauti na kuingiza Sh 240 milioni. Kila timu imetia mfukoni Sh 58.7 milioni ikiwa ni sehemu ya mgao wa mapato ya mlangoni waliyopata katika mechi hiyo iliyomalizika kwa Yanga kuibuka na ushindi wa bao 1-0. Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limethibitisha kwamba hakuna mechi nyingine ya ligi ambayo imeingiza mashabiki wengi uwanjani kama ilivyokuwa kwa Yanga na Azam FC. Bao la ushindi KIUNGO Haruna Niyonzima 'Fabregas' alifunga bao la 'kideoni'. Bao hilo lilikuwa hivi; Niyonzima alipokea mpira kutoka kwa beki wa kushoto, Oscar Joshua akiwa hatua tano kutoka mstari wa katikati ya uwanja na kukimbia nao kuelekea lango la Azam. Mnyarwanda huyo alipiga pasi kwa straika Jerry Tegete aliyekuwa kwenye msitu wa mabeki wa Azam nje kidogo ya eneo la penalti. Tegete alichofanya ni kutuliza na kuhama eneo hilo bila mpira. Mabeki wa Azam, Mkenya Jockins Atudo na David Mwantika walihama na Tegete na kutoa mwanya kwa Niyonzima kuunasa tena mpira huo kiulaini. Kiungo huyo alitisha kama atapeleka mpira huo kwa winga wa kulia Simon Msuva. Lakini, ghafla alibadilisha mwelekeo na kupiga shuti maridadi upande wa kulia wa kipa Mwadin Ally aliyeruka bila mafanikio. Hakuna aliyejua kama atapiga shuti. Wengi walidhani atatoa tena pasi kwa Tegete au Msuva ambaye alikuwa katika nafasi nzuri ya kupokea mpira huo. Hilo ni bao la kwanza la Niyonzima tangu msimu huu uanze. Pia, ni bao lake la tano kwa Yanga katika misimu miwili ya ligi aliyocheza. Yondani na Bocco Yanga imekutana na Azam FC mara nane tangu mwaka 2010. Mara sita kwenye Ligi Kuu Bara msimu wa 2010/11, 2011/12 na 2012/13. Pia, timu hizo zimekutana katika mechi ya fainali Kombe la Kagame mwaka jana na Kombe la Mapinduzi 2011. Katika mechi hizo, Yanga imeshinda nne, sare moja na kupoteza tatu. Straika John Bocco ndiye muuaji mkubwa wa Yanga. Nyota huyo ametikisa nyavu za Yanga mara nne kati ya saba. Lakini, Yondani anaweza akawa alisoma vyema alama za nyakati na kuwa makini na Bocco kwa dakika zote 90. Mlinzi huyo alifanikiwa kwa kiasi kikubwa kumficha Bocco ambaye aliambulia kupiga shuti moja hafifu kwenye lango la Yanga na vichwa viwili vilivyokwenda fyongo. Baada ya Bocco kukwaa kisiki hicho, dakika ya 34 aliamua kutumia nguvu kumsukuma kipa Ally Mustapha 'Barthez'na kufunga bao ambalo mwamuzi Hashim Abdallah wa Dar es Salaam alilikataa.