Yanga baba lao, Mayele apiga hat-trick

Yanga baba lao, Mayele apiga hat-trick

YANGA imetuma salamu kibabe kwa wapinzani wao wajao St. George ya Ethiopia na Al Hilal ya Sudan baada ya kuitupa nje Zalan ya Sudan Kusini kwa jumla ya mabao 9-0.
Mabingwa hao wa Ligi Kuu NBC 2021/22 wameendeleza ubabe wake mbele ya Zalan FC ya Sudan Kusini leo baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 5-0 katika mechi iliyopigwa kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa.
Mabao matatu ya Fiston Mayele huku Farid Musa na Aziz Ki wakifunga moja moja na kuhitimisha ushindi huo ulioiwezesha Yanga kusonga mbele kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika wakisubiri mshindi kati ya St. George kesho dhidi ya Al-Hilal ya Sudan.
Yanga ndio waliouanza mchezo kwa kasi wakiishambulia kwa nguvu Zalan dakika ya 6 beki wao wa kushoto Joyce Lomalisa anamwekea pasi safi Fiston Mayele akaingia nao mpira kwa kasi lakini shuti lake linatoka nje kidogo chini.

Dakika ya 10 Mayele tena anapokea pasi ya kiungo wake Salum Aboubakar'Sure boy' akiwa katika eneo zuri lakini anapaisha juu.

Nafasi bora zaidi kwa Yanga ilikuwa dakika ya 18 Lomalisa anampiga pasi ndefu Azizi KI akiwa katika umbali mzuri na mabeki wawili wa Zalan anakimbia nao mpaka kwa kipa wa Zalan Majok Majok lakini anashindwa kufunga unatoka nje kidogo.

Zalan wakitengeneza nafasi ya kwanza dakika ya 22 mshambuliaji wao Akhot Wiir anaharibu kufunga kwa Tik tak anapaisha juu kidogo akipokea pasi ya John Malok.
Yanga waliendelea na makosa ya kama mchezo wa ugenini ya kupoteza nafasi dakika ya 30 Aziz KI alipoteza nafasi ya wazi akiwa uso na lango la Zalan kipa na mabeki wakiwa wameanguka anapiga shuti linagonga mwamba na kurudi uwanjani.

Mayele naye aliendelea na makosa hayohayo akipokea pasi ndefu kutoka kwa Lomalisa lakini shuti lake linatoka nje kidogo akiwa uso kwa uso na kipa Majok.

Mpaka mapumziko hakuna timu iliyopata bao huku Yanga ikipoteza nafasi nyingi za kufunga.

Kipindi cha pili Yanga walirejea na mabadiliko wakimtoa kipa wao Djigui Diara aliyepatwa na maumivu dakika za mwisho za kipindi cha kwanza akaingia Aboutwalib Mshery.

Dakika ya 47 Yanga wakafanikiwa kupata bao la kwanza likifungwa kwa shuti na Farid akipokea krosi safi ya Moloko.
Dakika ya 57 Azizi KI anasahihisha makosa yake akiifungia timu yake bao la pili kwa shuti lililomshinda nguvu Majok aliyeshindwa kuudaka vizuri mpira uliojaa nyavuni.

Zalan ilionekana kucheza kwa kujilinda zaidi baada ya kuona mashambulizi ya Yanga yanawazidia hali iliyowafanya wasimamishe mshambuliaji mmoja tu juu.

Dakika 60 Fiston Mayele alifunga bao la tatu kwa Yanga na kuufanya uwanja ulipuke kwa shangwe za kelele kutoka kwa mashabiki waliohudhuria uwanjani.
Mayele yule yule dakika ya 62 alipachika bao la nne baada ya Aziz Ki kupiga mpira mrefu upande wa kushoto kwa Joyce Lomalisa ambaye alikimbia na kupiga krosi iliyoingia ndani ya boksi na kuunganishwa kwa mguu na Mayele.
Muuaji kutoka DR Congo, Mayele akapiga tena bao lake la tatu kwa mchezo 'Hat-trick' huku likiwa bao la tano kwa timu yake, akimalizia krosi ya Moloko.
Hiyo inakuwa ni Hat-trick ya pili kwa Mayele katika mchezo wa pili dhidi ya Zalan ambapo awali wakati wakishinda 4-0 alifanya kama hivyo.

Baada ya bao hilo Zalan wakafanya mabadiliko matatu kwa pamoja wakiwatoa John Malok, Tethloach Koang, Abraham Madol wakiingia Mosses Paul, Peter Mareu na Yuol Chol.

Yanga nao dakika ya ya 87 wakafanya mabadiliko matatu wakiwatoa Mayele, Feisal waliopata maumivu wakiingia Heritier Makambo na Denis Nkane huku baadaye wakiwatoa Azizi KI na Lomalisa nafasi zao zikichukuliwa na David Bryson na Ibrahim Bacca.

Dakika ya 90 Wiir anapoteza nafasi ya wazi akiunasa mpira baada ya mabeki wa Yanga kutegeana shuti lake linagonga mwamba na kurudi uwanjani likakutana na kipa Diarra na kuudaka mpira huo.

Mpaka dakika 90 za mchezo zinakamilika Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 5-0 na kuing'oa Zalan kwa jumla ya mabao 9-0 kufuatia ushindi wa kwanza wa mabao 4-0 ugenini.
Kikosi cha Yanga ni; Djigui Diarra/Mshery,Kibwana Shomari, Joyce Lomalisa/Bryson, Dickson Job, Yannick Bangala, Feisal Salum/Ibrahim Bacca, Salum Aboubakar, Stephanie Aziz KI/Denis Nkane, Jesus Moloko, Fiston Mayele/Makambo, Farid Mussa.

Kikosi cha Zalan ni; Majok Majok, Mario Majok, Anyak Majok, Jirkuei Kedit, Peter Manyiel, Kaman Chut, John Malok/Yuol Chol, Akhot Wiir, Tethloach Koang/Peter Mareu, Madut Thiik, Abraham Madol/Mosses Paul